Baro aitaka tena Tuzo ya Kipa Bora
Muktasari:
- Amesema nguvu na jitihada kubwa anayoifanya kwa msimu huu ni kurejesha heshima hiyo, ndio sababu ya kupambana kwake.
KIPA wa KVZ, Hamad Ubwa ‘Baro’, amesema anahitaji kutwaa tena Tuzo ya Golikipa Bora msimu wa 2026-2027 kama alivyofanikiwa hilo msimu uliopita.
Amesema nguvu na jitihada kubwa anayoifanya kwa msimu huu ni kurejesha heshima hiyo, ndio sababu ya kupambana kwake.
Baro amesema, kitendo cha kucheza bila ya kuruhusu bao dhidi ya Mlandege, timu aliyoitumikia msimu uliopita kimezidi kumuongezea kujiamini licha ya kwamba alikuwa na presha kubwa.
“Nilikuwa nahofia sana kuruhusu bao dhidi ya Mlandege, hivyo nina furaha. Nahitaji kuendelea kufanya vizuri kubeba tena tuzo ya kipa bora niliyochukua msimu uliopita,” amesema.
Septemba 23, 2026, KVZ iliichapa Mlandege mabao 2-0 katika mwendelezo wa Ligi Kuu Zanzibar, mechi iliyochezwa Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja ambapo Baro alikabiliana na timu aliyoitumikia msimu uliopita.
Baro ambaye hadi sasa amefanikiwa kuwa na cleansheet mbili katika mechi nne alizocheza, alibeba Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Zanzibar ambapo alimaliza msimu na cleansheet 12.