Prime
Bosi Takukuru afunguka sakata la kipa Fountain Gate

Muktasari:
- Haule amesema ofisi yao haijapata rasmi malalamiko yoyote juu ya mchezaji huyo, lakini baada ya kusikia mitaaani kuwa kuna mazingira ya rushwa yaliyotumika kwa golikipa huyo hadi kusababisha kufungwa mabao ya uzembe, wameamua kufuatilia.
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Manyara, Bahati Haule, amesema wameanza rasmi kufuatilia sakata la kipa wa Fountain Gate, John Noble aliyesimamishwa na klabu yake kwa tuhuma za kucheza chini ya kiwango dhidi ya Yanga.
Haule amesema ofisi yao haijapata rasmi malalamiko yoyote juu ya mchezaji huyo, lakini baada ya kusikia mitaaani kuwa kuna mazingira ya rushwa yaliyotumika kwa golikipa huyo hadi kusababisha kufungwa mabao ya uzembe, wameamua kufuatilia.
“Ni kweli hata sisi tumesikia kuwa magoli aliyofungwa huyo kipa yalikuwa na utata kwamba bao la kwanza alipigiwa shuti dogo akatema mpira kwa uzembe na goli la pili alirudisha mpira golini,” amesema Haule.
Amesema wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takukuru kifungu cha 15 kilichofanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge mwaka 2024.
“Sheria hiyo imeongezewa suala la kuwa rushwa ya uchaguzi, rushwa michezoni, kamari na michezo ya kubahatisha na mambo ya burudani,” amesema Haule.
Alisema vijana wa Takukuru hivi sasa wapo kazini kuchunguza suala hilo kwani baada ya kusikia taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii wameanza uchunguzi.
Alisema watatoa taarifa rasmi ya suala hilo mara baada ya uchunguzi kukamilika na hatua zaidi kuchukuliwa juu ya suala la mchezaji huyo.
Noble anatuhumiwa kucheza chini ya kiwango katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Aprili 21, 2025 na kuchangia timu yake ya Fountain Gate kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Yanga.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, Noble alianza kikosi cha kwanza lakini baada ya kuruhusu mabao mawili dakika ya 39 na 43, akatolewa, nafasi yake ikachukuliwa na Rashid Parapanda.
Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda ‘Mbuzi’ alisema wamemsimamisha Noble ili kupisha uchunguzi wa ndani ya klabu dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
“Baada ya uchunguzi kufanyika tutakuja kusema majibu ya kile tulichokipata kutokana na tuhuma zinazomwandama, hiyo ndiyo sababu ya kumsimamisha.
“Viongozi wa timu wameshampa barua ya kusimama kuitumikia timu, hatujui atasimama kwa muda gani,” alisema Mbuzi.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Robert Matano, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, alimtuhumu Noble kufungwa mabao ya kizembe.
Matano alieleza kuwa uzembe uliofanywa na golikipa huyo hadi wakafungwa ulisababisha kuwatoa mchezoni wenzake.
HALI ILIVYOKUWA
Bao la kwanza ulikuwa mpira wa kutengwa ambapo Stephane Aziz Ki alipiga krosi iliyogongwa na beki wa Fountain Gate katika harakati za kuokoa mpira ukamfikia Noble ambaye alimtemea Clement Mzize na kufunga bao dakika ya 38.
Tukio la pili ni dakika ya 43, Noble alitoka nje ya 18 akawa anajaribu kumpiga chenga Prince Dube, ndipo akakosa balansi na kujikuta akitoa pasi kwa Aziz Ki aliyeunganisha moja kwa moja hadi nyavuni.
Baada ya kufanya kosa la pili, benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Robert Matano, lilimtoa na kumuingiza Rashid Parapanda.
Baada ya kuwepo kwa tuhuma hizo za kucheza kwa makusudi chini ya kiwango, kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda, amezungumzia makosa aliyofanya Noble akisema: “Nikizungumzia kiwango katika mchezo huo kilikuwa chini, hali hiyo inamshushia heshima kama kipa wa kigeni ambaye anatakiwa afanye zaidi ya kile kinachotakiwa kufanywa na wazawa ndiyo maana mashabiki wamekuwa na wasiwasi naye ingawa kiufundi nikiwa kama kocha naona ni makosa ya kizembe.
“Mfano bao la pili baada ya kutoka ndani ya 18 alipaswa aupige mpira mrefu, sasa akawa anataka apige chenga alirudi nao ndani, wakati anafahamu anacheza na Yanga iliyo na washambuliaji hatari, mechi kubwa za Simba na Yanga ndizo alitakiwa aonyeshe ukubwa wake na ukomavu wa kuibeba timu.”
Naye Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye aliwahi kuwafundisha makipa wa Simba, Idd Pazi alisema: “Mara nyingi nasema sifa za kipa wa kigeni lazima awe na kiwango bora zaidi ya wazawa, mfano bao la pili kulikuwa na haja gani ya kupiga chenga wakati anajua Yanga ina washambuliaji hatari kama siyo kuwataka maneno ya watu kumshambulia.
“Tanzania tuna makipa wazuri zaidi ya hao kina Noble, mfano mzuri huyo Parapanda licha ya kufungwa mabao mawili ila alionesha uhai wa kuwepo golini.”
Kwa msimu huu, Noble amecheza mechi 16, amefungwa mabao 32 kati ya 51 iliyoruhusu timu hiyo, huku akiokoa hatari 22.