Clara Luvanga aweka rekodi ya uhamisho
Muktasari:
- Mchezaji huyo ambaye alijiunga na timu hiyo wiki iliyopita kwa mkataba wa miaka minne, amehamishwa kwa dau la Euro 1.7 milioni (Sh5.2 bilioni) ambayo imemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi katika soka la wanawake duniani kwa sasa.
UHAMISHO wa mshambuliaji Clara Luvanga kutoka Al Nassr kwenda Washington Spirit ya Marekani umemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi katika soka la wanawake duniani.
Mchezaji huyo ambaye alijiunga na timu hiyo wiki iliyopita kwa mkataba wa miaka minne, amehamishwa kwa dau la Euro 1.7 milioni (Sh5.2 bilioni) ambayo imemfanya aweke rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi katika soka la wanawake duniani kwa sasa.
Kabla ya Clara kuweka rekodi hiyo, uhamisho ghahi zaidi kwa soka la wanawake ulikuwa umeshikiliwa na Grace Geyoro aliyeuzwa kutoka PSG kwenda London Lionesses kwa dau la Euro 1.65 milioni (Sh5 bilioni) Septemba mwaka jana.
Katika orodha ya wachezaji watano ghali wa soka la wanawake duniani, nafasi ya tatu inashikiliwa na Kerolini Nicole ambaye Januari mwaka jana aliuzwa na Manchester City kwenda Barcelona kwa ada ya Euro 1.5 milioni (Sh4.6 bilioni),
Mshambuliaji Felicia Schröder ambaye Juni mwaka huu alijiunga na Real Madrid akitokea BK Hacken ya Sweden kwa dau la Euro 1.5 milioni (Sh4.6 bilioni) uhamisho wake unashika nafasi ya nne kwa thamani kubwa zaidi.
Anayeshika nafasi ya tano kwa uhamisho ghali zaidi katika soka la wanawake ni winga Mmexico, Lizberth Ovalle ambaye Agosti 2025, alijiunga na Orlando Pride ya Marekani kwa ada ya Euro 1.3 milioni (Sh4 bilioni) akitokea Tigres UANL.
Uwezo mkubwa wa Clara Luvanga ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga Princess katika kupachika mabao hapana shaka umechangia kuishawishi Washington Spirit kumwaga fedha kwa ajili ya kumnyakua nyota huyo.
Akizungumza baada ya kuthibitisha uhamisho huo, Luvanga mwenye miaka 21 alisema amefurahishwa na hatua hiyo na yuko tayari kukabiliana na changamoto mpya katika ligi hiyo pamoja na maisha ya soka nchini Marekani.
“Ninafuraha sana kujiunga na Washington Spirit na kukabiliana na changamoto hii mpya katika NWSL. Najua nimewasili wakati msimu tayari unaendelea, lakini ninafuraha sana kucheza katika ligi mpya na nchi mpya,” alisema Luvanga.
Luvanga pia alieleza kuwa Washington Spirit ipo katika nafasi nzuri na analenga kutoa mchango wake kwa timu hiyo katika kipindi kilichosalia cha msimu, hasa kuelekea hatua ya mchujo (playoffs).
“Timu ipo katika nafasi nzuri, na nataka kusaidia kadiri nitakavyoweza kuanzia sasa hadi kwenye playoffs. Go Spirit!” aliongeza nyota huyo ambaye aliwahi kuichezea DUX Logroño ya Hispania.
Luvanga amekuwa miongoni mwa wachezaji bora wa safu ya ushambuliaji katika Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia tangu alipojiunga na Al-Nassr.
Akiwa na klabu hiyo, Luvanga alisaidia Al-Nassr kutwaa mataji matatu mfululizo ya ligi, pamoja na kushinda mataji mengine ya ndani na kikanda, likiwemo Kombe la Wanawake la Saudi Arabia, Super Cup ya Wanawake ya Saudi Arabia na Mashindano ya Klabu za Wanawake ya WAFF ya mwaka 2026.
Msimu wake bora zaidi ulikuwa 2025/26, na alifunga mabao 24 katika mechi 14 za ligi na kutwaa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudi Arabia.
Luvanga pia alionesha uwezo wake mkubwa katika mchezo wa fainali ya Super Cup ya Wanawake ya Saudi Arabia, akifunga hat-trick na kuisaidia timu yake kupata ushindi. Msimu uliopita nyota huyo raia wa Tanzania alimaliza akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia akifunga mabao 24.