Corazone: Kucheza Simba lazima upambane
Muktasari:
- Corazone alijiunga na Simba mwaka 2022/23 alipotoka kucheza soka la kulipwa nchini Ureno katika klabu ya Atletico Ouriense.
KIUNGO wa Simba Queens, Vivian Corazone, amesema ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho ni changamoto inayomfanya azidi kupambana ili kuendelea kupata nafasi ya kucheza na kuboresha kiwango chake.
Corazone amesema kucheza katika timu yenye malengo makubwa kama Simba kunahitaji kujituma, nidhamu na maandalizi mazuri.
“Nimejiandaa vizuri kwa ajili ya msimu huu na ushindani uliopo ndani ya timu unatupa sababu ya kuongeza juhudi. Kama wachezaji wageni, tunapaswa kupambana zaidi ili kuonyesha uwezo wetu na kusaidia timu kufikia malengo yake,”€ amesema kiungo huyo raia wa Kenya.
Aliongeza kutwaa Kombe la Ngao ya Jamii kumewapa morali kubwa kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake unaotarajiwa kuanza Oktoba 28, akiamini kuanza kwa mafanikio hayo ni muhimu katika kujenga kujiamini na kuongeza hamasa ya kutafuta mataji mengine.
“Kombe hili tulilolipata linatupa morali kubwa ya kuanza msimu tukiwa mabingwa. Hilo linazidi kutuongezea hamasa na ushindani kwa sababu tunajua tunatakiwa kuendelea kufanya vizuri ili kutetea heshima ya timu,” amesema Corazone.
Kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza eneo la kati akisaidia ulinzi na mashambulizi, amekuwa miongoni mwa wachezaji wenye kiwango bora katika kikosi cha Simba Queens kutokana na mwendelezo wa kiwango chake tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Gaspo Women FC ya Kenya.
Corazone alijiunga na Simba mwaka 2022/23 alipotoka kucheza soka la kulipwa nchini Ureno katika klabu ya Atletico Ouriense.