David Ouma afunguka Singida BS kupotezea Muungano

Muktasari:
- Singida ilitupwa nje ya mashindano hayo na mabingwa wa Zanzibar, JKU kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 2-2 mechi iliyochezwa juzi Alhamisi, licha ya kuanza kutangulia kupata mabao mawili kupitia kwa Victorien Adebayor na Idd Khalid.
BAADA ya kuaga mapema michuano ya Kombe la Muungano inayofanyika Pemba, Zanzibar, kocha wa Singida Black Stars, David Ouma amewataka wachezaji kusahau kilichopita na kuelekeza macho kwenye ligi na Kombe la F, ambako bado wanayo nafasi.
Singida ilitupwa nje ya mashindano hayo na mabingwa wa Zanzibar, JKU kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 2-2 mechi iliyochezwa juzi Alhamisi, licha ya kuanza kutangulia kupata mabao mawili kupitia kwa Victorien Adebayor na Idd Khalid.
Ouma hakuficha hisia zake kuhusu kutolewa mapema, akisema: “Nimeumizwa sana na matokeo haya, hasa ukizingatia tulikuwa mbele. Lakini sasa ni muda wa kujipanga na kuangalia yale yaliyo mbele yetu. Tunapaswa kuchukulia hili kama funzo muhimu kwa safari yetu kwenye ligi na Kombe la FA.”
Kwa sasa, Singida wamesalia na mechi tatu za Ligi Kuu Bara pamoja na nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba. Katika msimamo wa ligi, Singida inashika nafasi ya nne kwa alama 53 ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Azam iliyo ya tatu na alama 54 na mabosi wa klabu wanasisitiza lengo ni kumaliza ligi nafasi ya tatu ili kukata tiketi ya CAF.
Kwa mujibu wa ratiba timu hiyo itakutana na Simba ndani ya siku tatu. Mei 14 iatacheza dhidi ya Simba katika ligi kisha Mei 16 zitavaana tena kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Ushindi katika moja au zote unaweza kuwa chachu ya kuamsha morali ya kikosi hicho. Baada ya hapo itaenda Dodoma Mei 21 kuvaana na Dodoma Jiji kabla ya kuhitimisha nyumbani kuvaana na Tanzania Prisons, Mei 25.