Eric Nditi : Mtanzania anayesubiri utajiri wa watoto wake wanaochezea Chelsea, Reading England

Adam Nditi (katikati) akimsikiliza kocha wake, Jose Mourinho. Kulia ni Eden Hazard na Kevin de Bruyne
Muktasari:
- Ingawa Adam anaanza kupata mafanikio katika soka akiwa Stamford Bridge, Nditi anakiri kwamba hakumpeleka mwanaye kutoka Zanzibar mpaka London kwa ajili ya kucheza soka na imetokea tu baada ya kinda huyo kuonyesha kipaji ambacho sasa kimebadili mwelekeo wa maisha yake.
MESUT Ozil, Neymar Jr, Kaka na wengineo wanasimamiwa katika maongezi ya mikataba yao na wazazi wao. Hii ni staili inayotumiwa na wazazi wengi barani Ulaya kwa sasa kuwasimamia watoto wao wenye vipaji kwa ajili ya kuchuma pesa na kuwapatia maendeleo watoto wao.
Eric Nditi, kiungo wa zamani wa timu ya Kikwajuni na timu ya taifa ya Zanzibar anaweza kuwa Mtanzania wa kwanza kuwaingiza wanaye katika soko la soka Ulaya ili kuhakikisha wanaibuka wanasoka bora huku yeye akichuma pesa za matunda yake.
Mtoto wake, Adam Nditi ameingia katika kikosi cha kwanza cha Chelsea akipewa jezi namba 47, lakini Nditi amenogewa na mwanzo mzuri wa mtoto wake wa kwanza na sasa amewaingiza watoto wake watatu, Roberto (13) na mapacha wawili, Zion na Paolo (8) katika timu za vijana za klabu ya Reading.
Mwanamke alimpeleka Ulaya
Nditi aliondoka Tanzania mwaka 1995 akizamia nchini Uingereza baada ya kukutana na mrembo wa Kiingereza, Marina ambaye ana asili ya nchi mbili za Italia na England. Alifikia katika Kitongoji cha Basingstoke ambacho anaishi mpaka sasa.
Wakati huo tayari alikuwa ameshaacha mtoto mmoja Zanzibar ambaye ni Adam aliyezaa na mwanamke mmoja wa Kitanzania mwaka 1994 wakati akikaribia kuacha soka katika klabu ya Kikwajuni.
Nditi alikutana na Marina wakati mrembo huyo akiwa Meneja Mauzo wa Kampuni ya Land Rover wakati yeye mwenyewe alishakata tamaa na soka na kuamua kujiingiza katika kampuni ya Mars iliyokuwa inajishughulisha na utengenezaji wa chocolate.
“Niliamua kuachana na soka na sikuja England kutafuta timu. Umri ulikuwa umenitupa mkono kwa hiyo nikajiingiza katika kazi nyingine za kujipatia kipato kwa hiyo soka rasmi niliachana nalo mwaka 1994 nikiwa Kikwajuni,” anasema Nditi.
Hakumpeleka Adam kwa ajili ya soka
Ingawa Adam anaanza kupata mafanikio katika soka akiwa Stamford Bridge, Nditi anakiri kwamba hakumpeleka mwanaye kutoka Zanzibar mpaka London kwa ajili ya kucheza soka na imetokea tu baada ya kinda huyo kuonyesha kipaji ambacho sasa kimebadili mwelekeo wa maisha yake.
“Nilimchukua kwa ajili ya kusoma hilo la mpira lilikuja baada ya scouts (skauti) kumwona akicheza kwenye timu ya mtaani sikuwa na mawazo kama kuna siku angekuwa Chelsea, ilitokea bahati tu maana pia alitakiwa na skauti wa Klabu ya Reading,” anasema Nditi.
Apeleka watoto wengine Reading
Kutokana na kunogewa na mafanikio ya Adam, Nditi anasema alivutika na mpango wa kuwapeleka watoto wake wengine watatu aliozaa na Marina katika timu ya Vijana ya Reading ambayo haiko mbali na nyumbani kwake.
“Wa kwanza ni huyu mkubwa, Roberto. Yeye ni baada ya Adam ingawa mama zao ni tofauti. Huyo anacheza under 14 ya Reading wakati mwingine, naamini lazima atacheza Premier League. Yuko sawa sana,” anasema Nditi.
“Zion na Paolo wana miaka minane, ni mapacha, lakini tayari wako timu ya Reading chini ya miaka tisa. Paolo ni very Skillful wakati Zion anaonekana kuwa beki kwa sababu anatumia sana nguvu. Lazima watacheza Ligi Kuu England,” anasema Nditi.
Nditi anakiri kwamba si lazima kila mzazi apeleke mtoto wake katika shule ya soka bali huwa wanaangaliwa kwanza vipaji vyao na kuchaguliwa.
“Sababu skauti wao walikuja mtaani kuangalia michuano fulani ya watoto wakaona vipaji vyao, wakaomba tuwapeleke kwenye majaribio katika timu zao, tatizo ni mbali kuwapeleka katika timu tofauti. Chelsea iliwataka pacha, lakini tayari nilishampeleka kaka yao, Roberto Reading kwa hiyo ingekuwa ngumu kwangu kupeleka watoto hawa Reading kisha nimpeleke mwingine London. Hata Chelsea walimtaka Roberto lakini imekuwa ngumu kwangu,” anasema Nditi.
Asimamia watoto wake kwa karibu
Tayari Nditi anawasimamia watoto wake kwa karibu. Adam ameshampatia wakala katika kampuni ya uwakala inayotambulika kwa jina la Midas.
Hata hivyo, tayari Adam ameshaondoka nyumbani na anaishi na mastaa wenzake makinda katika nyumba waliyokodiwa na Chelsea karibu na uwanja wa mazoezi wa timu hiyo, Cobham.
Nditi anakiri kwamba ingawa bado Adam ana chumba chake nyumbani kwao, lakini yuko tayari kumruhusu aondoke nyumbani kwake muda wowote na kuhamia kwake kama akiona uamuzi huo utamfaa.
“Mimi sina tatizo, akiamua kuanza kujitegemea anaweza kufanya hivyo wakati wowote na yuko huru, anaweza kuhama nyumbani lakini nitaendelea kumwangalia kwa karibu ili afike katika safari yake,” anaongeza Nditi.
Kama ilivyo kwa wazazi wa wachezaji mahiri katika soka la Ulaya na kwingineko, Nditi amedhamiria kuhakikisha kwamba soka ndio njia pekee kwa watoto wake kuukwaa utajiri na kuitajirisha familia kama inavyotokea katika familia nyingine zenye neema.
“Hicho kitu ninakipangia sana na nina watu wanaojua hayo yote, wapo kwenye shughuli hizo. Ndivyo ilivyo kaka kama hujafanya hivyo ujue hakuna lolote la maana watakalofanya maana huku kila kitu ukitaka kufanya ni uamuzi wako kwahiyo kama haupo karibu yao ujue maamuzi mengine watakayochukua utajijutia maishani,” anasema Nditi.
Adam anamiliki pasipoti ya Uingereza
Wakati kukiwa na utata kuhusu uraia wa Adam, Nditi anakiri kwamba mwanaye anasafiria pasipoti ya Uingereza, ingawa ana kiu ya kuichezea timu ya taifa ya Tanzania ingawa yeye mwenyewe Nditi hajabadili uraia.
“Adam anasafaria pasi ya huku ingawa mimi mwenyewe naupenda uzalendo. Hata hivyo akili yake yote ipo kuichezea Tanzania. Alilazimika kutafuta pasipoti ya huku kwa sababu ya usumbufu aliokuwa anaupata wakati anacheza Academy,” anaongeza Nditi kwamba mwanaye hana habari kwamba kumiliki pasipoti ya Uingereza kunampotezea uhalali wa kuichezea Taifa Stars.
“Yeye hilo halifahamu, anachojua ni kwamba anataka kuichezea Taifa Stars kuliko timu ya taifa ya England,” anaongeza Nditi.
Nditi anakiri kwamba licha ya kupandishwa kikosi cha kwanza huku akipewa mkataba wa kulipwa, lakini Adam hana malipo makubwa kama mastaa wengine wa Chelsea na kwa sasa analipwa kama mfanyakazi wa Chelsea tu, ila atalipwa zaidi baada ya mazungumzo yanayoendelea kati ya wakala wake na Chelsea.
Historia ya Eric Nditi
Nditi alizaliwa miaka 45 iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini kwa kiasi kikubwa amekulia Zanzibar ingawa yeye ni mwenyeji wa Masasi mkoani Mtwara.
“Mama yangu mzazi kazaliwa Pemba, Zanzibar, baba yangu ni mzaliwa wa Masasi, Mtwara lakini mimi nilichukuliwa na mama yangu mdogo nikiwa mtoto mdogo kwenda kuishi naye Zanzibar,” anasema Nditi.
Hataki kuelezea sana historia yake huku akisema kwamba alisoma Shule ya Msingi na Sekondari Zanzibar kabla ya kutimkia Ulaya. Na katika soka la Zanzibar amechezea timu mbili tu za Shangani na Kikwajuni.
Alikuwepo katika kikosi cha Shangani kilichotwaa ubingwa wa Zanzibar mwaka 1993 ingawa pia alitamba katika timu ya taifa ya Zanzibar iliyosheni mastaa kama Dua Said, Riffat Said, Seif Bausi na wengineo.
Nditi ambaye amesema huwa anakuja likizo nyumbani kila mwaka ingawa Adam hajawahi kuja tangu aende England mwaka 2008, amekiri hana maoni mengi na soka la Tanzania ingawa anatamani sana iwepo shule kubwa ya soka nchini.
“Kuhusu soka la nyumbani mimi wazimu wangu ni kuwa na academy kubwa japo moja kwa ajili ya wapenda soka na si ya kuzalisha pesa bali ni vipaji. Nadhani tatizo letu ni menejimenti inakuwa mbovu na wengi hawajui malengo ya academy. Wapo katika soka lakini hawajui lolote kuhusu soka la leo.”