Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu aitaja Simba, ataka makombe yote yarudi Yanga

FADLU Pict

Muktasari:

  • Fadlu amesema ameingia Jangwani akiwa na dhamira ya kutetea mataji ya ndani na kupanua mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa, huku akitaka Yanga iendelee kutawala soka la Tanzania na kuandika historia mpya Afrika.

KOCHA mpya wa Yanga, Fadlu Davids, amesema pengo la pointi tano lililopo kati ya timu hiyo na Simba kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu 2026-2027, si kikwazo kwake, akisisitiza kuwa anapenda changamoto na anaamini wanaweza kurejea kileleni.

Fadlu amesema ameingia Jangwani akiwa na dhamira ya kutetea mataji ya ndani na kupanua mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa, huku akitaka Yanga iendelee kutawala soka la Tanzania na kuandika historia mpya Afrika.

"Tukiwa nyuma kwa pointi tano, hiyo ni changamoto, mimi napenda changamoto. Lengo ni kutetea taji la ndani na kisha kuangalia zaidi ya ligi ya ndani ambako Yanga imekuwa ikitawala, ili kujenga jina letu kama moja ya klabu kubwa barani Afrika," amesema Fadlu katika mahojiano maalum na Yanga TV.

Fadlu amesema Yanga haina sababu ya kukata tamaa katika mbio za ubingwa, akieleza kuwa hata kama itashinda mechi zake zote zilizobaki bado inaweza kujikuta nyuma kwa pointi mbili, hivyo itahitaji pia wapinzani wake kudondosha pointi.

"Kwenye ligi, tunaweza kushinda mechi zetu zote zilizobaki na bado tukawa nyuma kwa pointi mbili, hivyo tunatumai wengine watadondosha pointi. Wakishtukiza kudondosha pointi, lazima tuwepo hapo tayari kurudi kileleni."

Ameweka wazi kuwa, malengo ya klabu ni kushindania kila taji lililo mbele yao.

"Malengo yetu ni kutetea Ligi Kuu ya NBC, kubeba Kombe la CRDB, na kutawala Ligi ya Mabingwa Afrika."

Msimu uliopita, Yanga ilipoteza Kombe la CRDB ambalo lilibebwa na Simba baada ya kushinda fainali bao 1-0 dhidi ya Azam. Kabla ya hapo, Yanga ilikuwa bingwa mtetezi na kuishia nusu fainali. Kombe linguine ililolipoteza Yanga ni la Muungano ambalo pia lilichukuliwa na Simba.

Kwa msimu huo 2025-2026, Yanga ilitetea Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na kubeba Kombe la Mapinduzi, makombe ambayo Fadlu anataka msimu huu wayabebe tena likiwemo la CRDB na Muungano, huku kikosi hicho kikianza kutetea Ngao ya Jamii wakati timu ikinolewa na Manqoba ikiifunga Simba.


MOT 01

ROBO FAINALI HAIMTOSHI

Mbali na Ligi Kuu, kocha huyo amesema Yanga haiwezi kuridhika na mafanikio ya kufika hatua fulani kwenye mashindano ya kimataifa, akitaka klabu hiyo iwe na malengo ya kwenda mbali zaidi.

"Klabu kubwa kama Yanga haiwezi kuridhika tu na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Ni nia yetu kuchukua changamoto hii na kuweka alama yetu kwenye mashindano makubwa zaidi Afrika."

Yanga inakabiliwa na changamoto ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa kwenye kundi linalotajwa kuwa gumu kutokana na uwepo wa timu kubwa kutoka Afrika Kaskazini.

Lakini kocha huyo amesema hakuna sababu ya Yanga kujiona dhaifu.

"Watu wanaliita kundi la kifo (likiwa na mabingwa wa Tunisia, Algeria na Misri), lakini sisi ni mabingwa wa Tanzania na hatupaswi hata kwa sekunde moja kujiona wanyonge."

Amesema moja ya kazi zake kubwa ni kubadilisha saikolojia ya wachezaji na klabu kwa ujumla ili waingie kwenye kila mchezo wakiamini wanaweza kushinda.

"Nawafanya wachezaji waamini kuwa nyumbani au ugenini tunaweza kushinda. Lazima tubadilishe saikolojia ya klabu; tusiishie tu kusherehekea kuvuka robo fainali, bali tuwe na nia na hamu ya kubeba kombe kabisa."

Yanga imepangwa kundi B na timu za RS Berkane (Morocco), MC Alger (Algeria) na Club Africain (Tunisia).


MOT 02

FALSAFA YAKE

Kwa mashabiki wanaotaka kujua Yanga yake itachezaje, kocha huyo ameweka wazi kuwa anapendelea soka la kushambulia na kumiliki mchezo.

"Mimi ni kocha ninayependa mpira wa kushambulia. Napenda kucheza kwenye nusu ya uwanja ya mpinzani. Sipendi mipira mirefu ya 50/50, napenda kucheza mpira wa kupita katikati ya mistari na maeneo."

Amesema kwake ushindi ndiyo kitu muhimu zaidi katika mchezo, lakini anaamini njia bora ya kuupata ni kupitia soka la kuvutia na la kushambulia.

"Ushindi ndio sarafu inayokupa mataji, lakini njia bora ya kushinda ni mpira wa kushambulia, kukaba kwa nguvu, umiliki wa mpira wa zaidi ya 60% na kushambulia mfululizo."

Kocha huyo anatambua kuwa timu nyingi za ndani zinaweza kuamua kujihami zinapocheza dhidi ya Yanga, lakini amesema hilo ni jukumu lake kutafuta ufumbuzi.

"Tunajua timu nyingi zitakutana nasi zikiwa zimerudi nyuma sana (low block), lakini ni kazi yetu kuzifungua, kushinda mechi na kuwaburudisha mashabiki. Mashabiki ndio wanahisa wakubwa zaidi wa klabu hii na tunataka wafurahie jinsi tunavyoshinda."

Mbali na hilo, kocha huyo amesema kujiunga na Yanga ni heshima kubwa kwake kutokana na ukubwa wa klabu hiyo, huku akisisitiza kuwa anakutana na timu yenye malengo makubwa kama yale aliyonayo yeye mwenyewe.

"Ni heshima kubwa sana kwangu kujiunga na klabu kubwa kama Yanga. Kocha mwenye matarajio makubwa anakutana na klabu yenye matarajio makubwa, na pamoja tunaweza kutengeneza ushirikiano utakaowezesha kutwaa mataji mengi Inshallah."

Amesema uamuzi wake wa kujiunga na Yanga ulivutiwa zaidi baada ya kuzungumza na Rais wa klabu hiyo, Hersi Said na kuelewa kwa kina mradi unaoendelea kujengwa.

"Rais (Hersi) aliponipigia simu na kunieleza mradi wa klabu, ilinisisimua sana. Ni changamoto, ni enzi mpya, ni kujenga timu, mtindo wa uchezaji na falsafa."


MOT 04

MAJERUHI WAMPA KAZI

Kocha huyo amesema tayari anawafahamu baadhi ya wachezaji wa Yanga kutokana na kucheza dhidi yao na kufuatilia mechi zao, ingawa anaamini kufanya nao kazi moja kwa moja kutamfanya awajue kwa undani zaidi.

"Nawajua wachezaji vizuri baada ya kucheza dhidi yao na kuchambua mechi zao. Unapofanya nao kazi ndipo unagundua ubora wao halisi na nani anayeweza kumudu shinikizo."

Hata hivyo, amekiri kuwa kikosi kina baadhi ya majeruhi wanaoweza kumletea changamoto katika hatua za mwanzo za kazi yake.

"Tuna majeruhi wanaotia wasiwasi: Maxi (Nzengeli) atakuwa nje kwa muda mrefu, Pacome (Zouzoua) amevunjika mguu, Duke (Abuya) na Yao (Kouassi) pia ni majeruhi. Hawa ni wachezaji muhimu, lakini kikosi kina kina cha kutosha."

Amesema kazi kubwa sasa ni kujenga mfumo utakaoendana na wachezaji waliopo huku akisubiri kurejea kwa wale waliopo kwenye matibabu.

"Lazima tutengeneze mtindo wa mchezo ili kupata kilicho bora kutoka kwenye kikosi tulicho nacho sasa wakati tukisubiri wengine warejee, hasa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa."


MOT 05

BENCHI LA ZAMANI NA JIPYA

Katika kuhakikisha anafanikiwa kutekeleza falsafa yake kwa haraka, kocha huyo amesema anaamini umuhimu wa kuchanganya wafanyakazi waliokuwapo klabuni na wale aliokuja nao.

Amesema watu waliokuwapo akimaanisha kipindi cha Manqoba Mngqithi, tayari wana nafasi kubwa kutokana na kuifahamu Yanga kwa undani.

"Katika klabu yoyote unayokwenda, ni muhimu kuwa na wafanyakazi waliopo kwa sababu wanaielewa klabu na wanakupa taarifa za ndani kabisa."

Lakini pia amesema benchi analokuja nalo lina umuhimu mkubwa katika kumsaidia kufikisha haraka falsafa yake kwa wachezaji.

"Kwa upande mwingine, ni muhimu kuja na wafanyakazi wako kwa sababu mpira hauna muda mrefu, inasaidia kufikisha falsafa, mbinu na mtindo wa uchezaji haraka zaidi. Wafanyakazi wangu wanajua nini tunafanya na kwa wakati gani."

Akaweka wazi kuwa njia bora ni kuunganisha pande zote mbili kwa lengo moja la ushindi.

"Ni muhimu kuchanganya wafanyakazi wa zamani na wapya ili kutengeneza timu ya ushindi."


MOT 03

TANZANIA IMEMPA UZOEFU

Kocha huyo amesema safari yake ya awali kwenye soka la Tanzania imemsaidia kujifunza mazingira, changamoto za usafiri pamoja na tofauti za viwanja.

Amesema msimu wake wa kwanza wakati anainoa Simba 2024-2025, haukuwa rahisi kutokana na kutokuyafahamu vizuri mazingira ya baadhi ya mechi za ugenini.

"Msimu wangu wa kwanza nchini Tanzania ulikuwa mgumu kwa sababu hujui viwanja vya ugenini kama Bukoba au Arusha. Sasa ninajua lojistiki zote ikiwemo za kusafiri na nini cha kufanya."

Pamoja na changamoto hizo, amesema Watanzania wamempokea kwa moyo mkubwa na hilo linampa nguvu ya kufanya kazi kwa ari zaidi.

"Watanzania wamenipokea vyema sana... Ukarimu wa Watanzania ni namba moja, pamoja na mradi mkubwa wa Yanga tunaoujenga."


FADL 02

NAFASI YA VIJANA

Kocha huyo pia ameahidi kuwapa nafasi wachezaji vijana wenye uwezo, akisema wao ndiyo msingi wa mafanikio ya baadaye.

"Vijana ndio mustakabali wa baadaye. Lazima uwalee, uwafundishe na uwape kujiamini. Vijana wana mtazamo wa kutohofia."

Amesema tayari ameshuhudia baadhi ya vipaji kwenye mazoezi na ana hamu ya kuviona vikipewa nafasi ya kuitumikia Yanga.

"Napenda kuwapa nafasi vijana, na tayari nimeona vipaji kwenye mazoezi. Ninatazamia kuwaona wakivaa jezi hii kubwa ya Yanga."


FADL 04

DABI YA KARIAKOO HAIMTISHI

Kuhusu Dabi ya Kariakoo, kocha huyo amesema hana hofu na mechi kubwa kutokana na uzoefu wake wa kushiriki katika dabi nyingine zenye presha kubwa.

"Nimeshiriki Dabi ya Kaizer Chiefs dhidi ya Orlando Pirates, na Wydad dhidi ya Raja Casablanca. Dabi ya Kariakoo pia ni mechi kubwa sana."

Amesema uzoefu wake wa soka la Tanzania pia unampa faida ya kuwafahamu vizuri wapinzani wake ambao ni Simba baada ya awali kuifundisha timu hiyo.

"Faida yangu ni kwamba nawajua wapinzani vizuri, najua wapi wana udhaifu na wapi wana nguvu. Hizi ni mechi ambazo lazima tushinde."

Fadlu ambaye wakati yupo Simba alikutana na Yanga mara nne, alipoteza mechi zote na kuruhusu mabao matano, huku upande wake ukiwa haujafunga bao. Katika mechi hizo, mbili za Ngao ya Jamii ambazo zote matokeo yalikuwa 1-0, kisha zingine za Ligi Kuu matokeo yakiwa 1-0 na 2-0.


FADL 03

KUHUSU KAMBI YA ZANZIBAR

Katika kuhakikisha Yanga inakuwa tayari kwa changamoto zinazokuja, kocha huyo amesema maandalizi ya Zanzibar yana umuhimu mkubwa, hasa katika kuzoea mazingira ya hali ya hewa.

"Maandalizi ya Zanzibar ni muhimu sana ili kuzoea hali ya hewa ya joto ya saa 9:00 au saa 10:00 jioni kwa mechi zetu za Ligi Bingwa, ili iwe faida kwetu na mzigo kwa mpinzani."

Amesema kipindi hicho pia kitakuwa muhimu katika kujenga misingi ya timu anayoitaka.

"Huu ni wakati wa kuweka misingi, mtindo wa mchezo na mbinu zetu kwa kina."


FADL 05

UJUMBE KWA MASHABIKI

Katika ujumbe wake kwa mashabiki wa Yanga, kocha huyo amewashukuru kwa mapokezi waliyompa na kuwaomba waendelee kuiamini timu huku wakijenga ndoto kubwa za mafanikio ya Afrika.

"Kwanza kabisa nawashukuru kwa mapokezi mazuri na ushirikiano. Msimu huu tunataka wajivunie timu, wafurahie mpira na wawe na ndoto kubwa za kutawala Afrika. Tuote ndoto kubwa na kuonyesha upendo tele!"

Fadlu ametua Yanga baada ya klabu hiyo kuachana na Manqoba aliyedumu kwa takribani miezi mitatu akitua Julai 2026 na kuondoka Oktoba 2026.