Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu mkeka umetiki, Orlando yamvutia kasi

Muktasari:

  • Fadlu ambaye alitambulishwa ndani ya Simba Julai 5, 2024 akitokea Raja Casablanca ya Morocco akiwa kocha msaidizi, alipewa mkataba wa miaka miwili kuliongoza benchi la ufundi la Msimbazi ambapo tayari anaelekea kuumaliza mmoja, na kubaki mwingine.

UNAWEZA kusema ni kama mkeka wa Fadlu Davids umetiki kwani ubora aliouonesha hadi sasa ndani ya Simba, umewafanya Wasauzi wenzake, Orlando Pirates kuanza hesabu za kumrudisha kikosini kwao.

Fadlu ambaye alitambulishwa ndani ya Simba Julai 5, 2024 akitokea Raja Casablanca ya Morocco akiwa kocha msaidizi, alipewa mkataba wa miaka miwili kuliongoza benchi la ufundi la Msimbazi ambapo tayari anaelekea kuumaliza mmoja, na kubaki mwingine.

Wakati anatua Simba ilionekana hatakuwa na maisha marefu, lakini amekuwa miongoni mwa makocha watatu pekee walioanza na timu mwanzo wa msimu na kuendelea kuwepo. Wengine ni Mecky Maxime (Dodoma Jiji) na Ahmad Ally (JKT Tanzania). Timu zingine 13 zimebadilisha makocha.

Kocha huyo kabla ya kutua S aliwahi kufundisha soka Afrika Kusini katika timu za Maritzburg United, Orlando Pirates, Chippa United na Royal AM FC.

Fadlu anayeiandaa Simba Jumapili hii kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, ameonekana kuwa mtu sahihi kwenda kuiongoza Orlando Pirates ambayo inajiandaa kwa maisha mapya msimu ujao bila kocha wa sasa, Jose Luis Riveiro, raia wa Hispania anayetajwa kwenda Saudi Arabia baada ya mkataba wake kumalizika Juni 30 mwaka huu.

Kabla mambo hayajaharibika, Simba imerudi mezani kukaa na kocha huyo kwa ajili ya kumuongezea mkataba  ili kuendelea na mradi wa kujenga timu imara.

Simba inajipanga kumpa mkataba mrefu zaidi Fadlu kutokana na kupata taarifa hizo za Orlando Pirates kumuweka kwenye orodha ya makocha watatu mmoja kwenda kuziba nafasi ya Riveiro.

Ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, limepitishwa azimio kwamba Fadlu anatakiwa kuendelea kwa misimu miwili zaidi kukiongoza kikosi hicho kufuatia baadhi ya klabu kuanza kumtolea macho.

“Tulishapitisha hilo kwenye vikao vya bodi, na hata Mwenyekiti wa Bodi Mo Dewji alisema mchakato wa kumbakisha zaidi utafanyika, ndio maana unaona anaendelea kufanya hesabu za maboresho ya kikosi chetu kwa msimu ujao,” alisema bosi mmoja wa Simba.

“Hapa kati tulipata wasiwasi tulipofika katikati ya msimu kuna ofa zilikuja lakini kocha mwenyewe akaonyesha heshima kwa klabu kwa kuamua kubaki akifurahia mradi ambao tunakwenda nao na utulivu tunaompa.”

Uamuzi wa Simba kutaka kumpa mkataba mwingine Fadlu kabla ya huu kumalizika ni kufuatia klabu hiyo kuondokana na utaratibu wao wa kutimua makocha mara kwa mara.

“Miaka ya nyuma tulikuwa na mabadiliko ya makocha mara kwa mara lakini sasa tumebadilisha hilo ndio maana unaona hata hawa makocha wetu wanahusika moja kwa moja kwenye uendeshaji wa soka la vijana ili kuwakuza wachezaji wadogo iwe rahisi kuingia kwenye kikosi cha wakubwa,” alibainisha bosi huyo.

Orlando na Fadlu waliwahi kufanya kazi pamoja kuanzia Januari 15, 2019 hadi Agosti 17, 2021 akianza kuwa msaidizi wa Milutin Sredojević ‘Micho’ kabla ya baadaye kupewa timu mazima.

Mbali na Fadlu, pia kocha wa makipa wa Simba, Wayne Sandilands kipindi cha uchezaji wake alikuwa kipa wa Orlando, hivyo kama Fadlu ataondoka basi anaweza kuondoka naye kama ambavyo walivyotua Simba.

Fadlu katika msimu wake wa kwanza Simba, ameiongoza timu hiyo kucheza mechi 22 za ligi, ikishinda 18, sare tatu na kupoteza moja, timu hiyo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 57. Kama haitoshi, Simba ipo hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa imefika hapo baada ya kucheza michezo 11, ikishinda saba, ikipoteza mbili na kutoa sare mbili.

Kwa sasa Simba ipo Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch baada ya kushinda nyumbani 1-0, hivyo inahitaji ushindi au sare kufuzu fainali.

Simba chini ya Fadlu, mpaka sasa ina nafasi ya kuchukua mataji matatu inayoshiriki ambayo ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la FA ambalo pia wapo nusu fainali.