Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fainali ya Maveterani kupigwa Azam Complex

MAVETERANI Pict

Muktasari:

  • Fainali za mwaka huu zitazikutanisha timu nne zilizofanikiwa kupenya hatua za mwisho ambazo ni Yanga Veterans v Raja Veterans, Baruti Veterans na Uhuru Veterans kutoka Kilimanjaro mechi zote zikipigwa kuanzia asubuhi uwanjani hapo.

FAINALI ya Ligi ya Maveterani inatarajiwa kupigwa June 07 Uwanja wa Azam Complex huku viongozi wa Chama cha ligi hiyo wakisisitiza kuwa lengo ni kuendeleza afya, furaha na mshikamano kwa nyota wa zamani wa soka nchini.

Fainali za mwaka huu zitazikutanisha timu nne zilizofanikiwa kupenya hatua za mwisho ambazo ni Yanga Veterans v Raja Veterans, Baruti Veterans na Uhuru Veterans kutoka Kilimanjaro mechi zote zikipigwa kuanzia asubuhi uwanjani hapo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Hashim Abdallah, alisema ligi hiyo imeendelea kuwa daraja la kuwaweka pamoja mastaa waliowahi kulitumikia soka la Tanzania na kuwasaidia kuboresha afya zao.

"Kaulimbiu yetu ni Afya na Furaha. Tunataka wachezaji wa zamani waendelee kufanya mazoezi na kukutana mara kwa mara. Ukiacha kucheza na kubaki nyumbani tu, unajiweka kwenye mazingira yasiyo mazuri kiafya," alisema Abdallah.

SABABU SIMBA, AZAM KUTOKUWEPO
Akijibu kuhusu kutokuwepo kwa Simba na Azam kwenye hatua hiyo, Abdallah alisema Azam iliondolewa hatua za mapema, lakini Simba ilikumbana na changamoto za kifedha zilizowafanya washindwe kusafiri kwenda Tabora kwenye mechi za hatua ya mchujo.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Innocent Njovu, alikiri kuwa changamoto za kiuchumi ndizo ziliifanya timu hiyo kushindwa kuendelea na mashindano hayo.

"Kwa kweli tulikuwa na timu nzuri sana na tuliongoza tangu mwanzo wa ligi, lakini tulishindwa kusafiri kwa wakati kwenda Tabora kutokana na changamoto za kifedha. Kanuni zikafanya kazi yake. Hata hivyo tunaamini msimu ujao tutarudi tukiwa na nguvu zaidi," alisema Njovu.

Akijibu kuhusu sapoti wanayopata kutoka kwa Simba Njovu alisema "Mwanzoni hatukuwa tunapewa sapoti ndio maana umeona changamoto kama hiyo lakini sasa mambo yako shwari na msimu ujao nafikiri ni kuwapelekea tu vitu tunavyohitaji watatusaidia."

Nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar na Yanga, Vincent Peter, ambaye sasa anakipiga Baruti Veterans, alisema ligi hiyo imekuwa zaidi ya mashindano kwani imewasaidia mastaa wengi wa zamani kurejesha urafiki na mshikamano walioupoteza kwa miaka mingi.

"Tumekutana marafiki wengi tuliopoteana nao kwa muda mrefu. Huu ni ushindi mkubwa kwetu. Lakini pamoja na hilo, ninaamini ubingwa utaenda Baruti Veterans," alisema Vincent.

Mbali na kutafuta bingwa wa mwaka huu, waandaaji wameweka wazi kuwa mshindi atazawadiwa seti mbili za jezi, mipira miwili pamoja na medali za dhahabu huku juhudi zikiendelea kutafuta wadhamini watakaoongeza zawadi ya fedha.