Prime
Siri ya basi jipya na kitendawili cha uwanja Simba
SIMBA imeitoa tamko kuhusu hatma ya ujenzi wa uwanja mpya wa klabu hiyo, ikithibitisha kupokea mitazamo mbalimbali, huku ikieleza maamuzi ya mwisho yatafanywa na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema hawajapokea taarifa yoyote ya mtu anayetaka kujenga uwanja, lakini kuna mjadala wa ndani kuhusu mahali pa kujenga uwanja huo.
Magori amesema katika mjadala huo, baadhi ya wadau wa klabu wamependekeza uwanja ujengwe Bunju, kwa kuwa eneo hilo linafaa kwa ujenzi. Hata hivyo, wengine wamekuwa na mawazo tofauti.
“Baadhi ya mawazo yameonyesha uwanja ujengwe eneo tofauti na Bunju, ambalo litakuwa rahisi kufikika kwa mashabiki kutoka sehemu mbalimbali. Hata hivyo, wapo waliopendekeza Bunju ibaki kuwa sehemu ya kisasa kwa ajili ya mazoezi ya Simba,” amesema Magori.
Aliongeza: “Hatujapokea taarifa kuna mtu anataka kujenga uwanja. Bunju, ukiangalia pale, kuna maboresho yanayofanywa kila wakati. Bodi tutakutana kuamua kwa sababu kuna mawazo mbalimbali: je, tujenge uwanja Bunju, au tujenge uwanja mahali pengine na kutafikika kirahisi? Je, Bunju ibakie kama eneo maalumu la mazoezi ya timu na tutatafuta eneo jingine kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya?”
Pia Magori amesema mashabiki wanapaswa kuelewa changamoto za kufikika Bunju:
“Kuna mawazo tofauti kuhusu matumizi ya Bunju. Je, tukijenga uwanja pale, watu watafika wakiwa na urahisi? Mashabiki wengine wa Simba wapo Mbagala; umbali hadi Bunju ni mkubwa. Je, wataweza kufika? Mitazamo hii itajadiliwa na Bodi ya klabu kabla ya kufanya maamuzi.”
“Bodi itayachambua yote na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu eneo ambalo uwanja mpya utajengwa, huku ikizingatia afya na masilahi ya mashabiki na klabu. Wakati ukifika, tutawatangazia kila kitu.”
Aidha, Magori aliwahakikishia mashabiki kwamba ahadi za mzabuni wa jezi za klabu, Jayrutty, zinaendelea kutekelezwa, huku baadhi zikiwa tayari zimeanza kutimizwa ndani ya mkataba wake.
“Ahadi zote zitatimizwa. Mchezaji amesajiliwa, tulimwambia asajili Ino Loemba katika dirisha dogo. Tulipokuwa tunapanga bajeti yetu, hatukuwa na fedha za kutosha, lakini tulimwambia kwenye ahadi yako ya kusajili mchezaji mmoja kila mwaka, hebu msajili Loemba, akafanya hivyo. Ahadi zake zinatekelezeka kwani mkataba ni wa miaka mitano. Kadri tunavyotekeleza, tunategemea ndani ya muda wa mkataba huu yote yatakamilika. Kwa mfano, ahadi ya basi lazima itolewe mara moja si kwamba itolewe kila mwaka. Ikiwa atatoa Aprili, Mei, Juni au Julai, hakuna shida. Muhimu ni atatoa ndani ya muda wa mkataba wake wa miaka mitano. Tunaamini basi litafika na fedha za uwanja zitatumika, yote aliyoyaahidi yatafikiwa kwa sababu tuna mkataba wa miaka mitano naye.”
Ufafanuzi huo wa Magori unakuja wakati mzabuni huyo tayari ameshaleta basi hilo la kisasa aina ya Irizar, kama alivyokuwa ameahidi kwa ajili ya kikosi cha klabu na sasa lipo kwa wataalam wakuweka nembo za klabu hiyo.