Simba imefanikiwa kumtega Sowah
Muktasari:
- Adhabu yenyewe ilikuwa ni kufanya mazoezi na kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 cha Simba na kutozwa faini ya fedha kwa kile kilichotajwa kimesababishwa na makosa ya utovu wa nidhamu.
ILE adhabu ambayo Simba ilimpa Jonathan Sowah ulikuwa ni mtego ambao mshambuliaji huyo alipaswa kuushtukia na kufanya uamuzi sahihi.
Adhabu yenyewe ilikuwa ni kufanya mazoezi na kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 cha Simba na kutozwa faini ya fedha kwa kile kilichotajwa kimesababishwa na makosa ya utovu wa nidhamu.
Hata hivyo, Sowah ameikacha adhabu hiyo na kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, mchezaji huyo hivi sasa yupo kwao Ghana akidai hayuko tayari kutekeleza adhabu hiyo ambayo alipewa na uongozi wake.
Kwa jicho la tatu, hapa kijiweni tunaamini katika kinachoendelea hivi sasa, Simba ndio imefanikiwa zaidi kuliko mchezaji huyo ambaye tunaona kama amefanya uamuzi wa hasira.
Inasemekana jamaa alipojiunga na Simba kutokea Singida Black Stars, mkataba wake uliwekwa vipengele kadhaa vigumu ambavyo sio rahisi kuvunjwa na upande wowote hasa vya malipo ya fidia.
Isitoshe hawa wachezaji kutoka nje ya Tanzania huwa wana ujasiri wa kwenda kushtaki katika mamlaka za juu kisoka duniani pindi wanapokuwa na uhakika mikataba yao imevunjwa kiholela.
Sasa adhabu ambayo Simba iliitoa kwa Sowah ukiifanyia tathmini ya kina utabaini ililenga yenyewe kubaki salama mbele ya mchezaji huyo kwa uamuzi wowote ambao angeuchukua baada ya kuadhibiwa.
Kukubali kwenda katika kikosi cha vijana, maana yake Sowah angethibitisha ni kweli amejihusisha na utovu wa nidhamu hivyo msimu ukiisha ingekuwa rahisi Simba kumwacha kwa vile ingesimamia hoja ya utovu wa nidhamu.
Kutojiunga na kikosi chao cha vijana kuna maanisha Sowah ni mtoro kazini hivyo Simba ikivunja mkataba itakuwa salama.