Prime
Simba na Jonathan Sowah bado mtoto hatumwi dukani
ULIKUWA msemo wa zamani. Mtoto hatumwi dukani. Inamaanisha kwamba mambo ni magumu. Dukani inabidi atumwe mtu mzima kwa sababu jambo akitumwa mtoto anaweza akapoteza njiani.
Jana tumeingia Mwezi Juni na tayari mwaka umegawanyika. Jonathan Sowah hayupo katika kambi ya Simba wakati huu ligi ikiwa imebakiza mechi chache kabla ya kumalizika. Hatujazoea kuona mchezaji ambaye alitua klabuni kama tegemeo akiwa nje ya uwanja kwa muda mrefu namna hii bila ya kuwa majeruhi au bila ya kutumikia kifungo kutoka katika mamlaka za mpira.
Sowah amekaa nje kwa muda mrefu na ninahisi kuna habari ya kutunishiana misuli kati ya pande zote mbili. Haiwezekani. Hii sio hali ya kawaida kwa mchezaji wa Kariba yake aliyesajiliwa kwa mbwembwe na ambaye alionekana angekuwa ongezeko muhimu katika timu.
Upande wa Sowah anaonekana kuwa mchezaji ambaye ana msimamo yake ambayo wakati mwingine unaweza usiiweke mbali sana na utovu wa nidhamu. Kama tuhuma dhidi yake ni za kweli au sio za kweli lakini tumezoea kuona wachezaji, hata kama ni mastaa, wakiomba msamaha na kushikana mikono na viongozi au benchi la ufundi halafu maisha yanaendelea.
Upande huu wa Sowah inawezekana ni aina ya mchezaji ambaye ana kiburi na anaamini katika mipango yake. kwamba kama Simba wanamletea kiburi basi na yeye anaweza kuleta kiburi maradufu kwa sababu wasifu wake wa kufunga mabao upo wazi.
Kwamba anajua kuwa hata leo hii akiondoka zake Simba anaweza hata kubakia hapa hapa katika jiji la Dar es salaam akijiunga na Yanga au Azam. Anaweza pia kuamua zake Kwenda Afrika Kusini akapata timu ya ligi kuu. Anaweza Kwenda nchi nyingi akiwa na video zake mkononi na hawezi kukosa timu.
Katika dunia hii ambayo ina uhaba wa washambuliaji ni rahisi kwa Sowah kupata timu. Hata alipotua Singida Big Stars na kuanza kufunga mabao kwa haraka ilionekana wazi kwamba lilikuwa suala la wiki tu kwa Sowah kwenda timu kubwa. Wakati ule tuliamini kwamba angeenda Yanga kabla mambo hayajabadilika.
Kwa upande wa klabu mara kadhaa tumezoea kuona klabu ikiwabembeleza wachezaji mastaa ili maisha yasonge mbele. Mfano wakati ule kuna wachezaji wengi mastaa walikuwa na tabia za ajabu lakini klabu ziliweza kuwavumilia. Akina Emmanuel Okwi wamewahi kuwa na tabia za ajabu lakini klabu zilishikana nao mikono na kuwavumilia.
Kuna zile nyakati ambazo akina Okwi walikuwa wanachelewa kujiunga na kambi licha ya kutumiwa tiketi lakini klabu zilikuwa zinawavumilia katika staili ambayo wengine tuliamini kwamba kuna baadhi ya wachezaji ni wakubwa kuliko timu.
Hata Clatous Chota Chama ameishi sana kimashaka na uongozi katika utawala wake wa kwanza pale Msimbazi kabla ya kwenda Yanga. Walilazimika kushi naye kwa sababu ya ustaa wake. Katika hili la Sowah Simba wameonekana kugomea utumwa dhidi ya wachezaji mastaa.
Inawezekana kwamba ni kwa sababu Sowah hakutengeneza ufalme wake Simba. Bado alikuwa anajitafuta katika jezi ya Simba. Labda angefanya makubwa katika miezi michache aliyocheza Simba huenda leo hadithi ingekuwa tofauti. Huenda leo angekuwa amewafanya Simba mateka wake.
Inawezekana pia kwamba Simba imemuweka kando Sowah kwa sababu makosa aliyofanya hayasameheki. Hata hivyo tunawakumbuka baadhi ya wachezaji wa hizi timu kubwa za watani ambao waliwahi kufanya makosa makubwa lakini mwisho wa siku walisamehewa.
Lakini pia dunia imebadilika na kuna uwezekano kwamba viongozi nao wamebadilika. Labda viongozi wamegundua umuhimu wa kutoburuzwa na wachezaji. Kama wamegundua hilo pia ni jambo sahihi. Siku hizi wachezaji wanalipwa mamilioni ya fedha n ani matajiri huku mitaani kwetu.
Wanapaswa kuheshimu kazi zao. Kama Simba imerudi katika misingi hii ya watu kuzingatia weledi katika kazi zao ni jambo jema na tumekuwa tukililia kwa miaka mingi. Kila mtu afanye kazi kwa weledi ili tufanikiwe katika mipango yetu.
Lakini kuna uwezekano pia kwamba Simba imepewa kiburi na namna ambavyo inaendelea kufanya vema bila ya uwepo wa Sowah. Kuna kitu kinaendelea kutengenezwa Msimbazi kwa sasa kiasi kwamba hata mashabiki hawaoni sana umuhimu wa Sowah.
Usajili wa akina Aniceth Oura, Libasse Gueye, Nickson Kibabage na kurudi kwa Chama kumeitia timu nguvu kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba Sowah hakumbukwi. Pale Mbele Suleiman Mwalimu amekuwa akifanya vema pia.
Kama Simba ingekuwa ovyo nadhani ingekuwa rahisi kwa mashabiki wake kuhoji kwanini Sowah amekuwa hachezi. Mara kadhaa tumewahi kuona namna ambavyo mashabiki wamekuwa wakisimama nyuma ya mchezaji asiye na nidhamu kwa sababu tu ya tamaa ya kupata matokeo.
Kwa namna Simba inavyosonga mbele bila ya Sowah, kwa namna walivyofanikiwa hadi kuvunja uteja kwa Yanga huku wakiwa na matumaini makubwa ya ubingwa, limekuwa jambo rahisi kwa mashabiki kutowapa presha viongozi kuhusu suala la Sowah.
Vyovyote ilivyo ni kwamba bifu la Sowah na Simba mpaka sasa mtoto hatumwi dukani. Ngoma ni bila bila. Wengi hawafahamu kinachoendelea lakini kwa kusoma picha ya nje tu ni kwamba pande zote mbili zimeonyesha kujaribu kupimana ubavu.
Sikumbuki ni lini mchezaji mzuri kama Sowah aliwahi kukaa nje kwa kipindi kirefu bila ya kucheza katika timu kubwa kama Simba huku akiwa hana majeraha na wala hajafungiwa na mamlaka za mpira. Lazima hizi pande zitakuwa zinapimana ubavu tu.