Prime
Dakika za jioni kwa kina Metacha, hatuna ubinadamu tena
METACHA Mnata kuna kosa alifanya katika pambano la Singida Big Stars dhidi ya Yanga. Kosa ambalo mchambuzi akikaa katika kochi anaweza kulichambua vizuri tu. Yanayobakia baada ya hapo unawaachia watu wa benchi la ufundi na mashabiki wa mpira.
Metacha alipanga ukuta wake vibaya wakati Alain Okello akikaribia kupiga mpira wa faulo. Kwanza kabisa alikaa nyuma ya ukuta wake. Pia eneo ambalo Okello alipitishia ukuta wake Metacha alipaswa kuweka mtu mwingine. Angeweka mtu kisha akarudi upande wa kushoto katika eneo ambalo hakukuwa na ukuta.
Okello angepaswa kufanya kazi ambayo ilikuwa inafanywa na kina David Beckham. Alipaswa kuupitisha mpira juu ya ukuta. Wataalamu wachache ambao wangeweza kuupitisha mpira kwa chini. Hata hivyo, wenzetu huwa wanachukua tahadhari kwa kumweka mchezaji mmoja anayelala chini ya ukuta. Hata hivyo Okello hakuwa na kazi ngumu. Aliupitisha mpira kando ya ukuta. Kitu cha kushangaza Metacha alikuwa hapo hapo.
Nisingemlaumu Metacha kama angekwenda ule upande mwingine wa ukuta. Alikuwa hapo na akafungwa hapo hapo. Ni makosa ya kimchezo. Makipa wengi huwa wanafanya makosa hayo. Tatizo hatujui kama wanafanya kwa makusudi au kwa kutojua. Ni kama makosa ya wanadamu wengine katika kazi zetu.
Benchi la ufundi liliamua kumtoa nje Metacha ambaye aligoma kwa dakika kadhaa kutoka uwanjani. Aliondoka uwanjani baada ya kubembelezwa na wenzake na hapo hapo akaifikia simu yake katika vyumba vya kubadilishia nguo na kufuta utambulisho wake kama mchezaji wa Singida Big Stars katika mitandao yake ya kijamii. Hasira tu kama hasira za mwanadamu mwingine.
Inawezekana dhamira yake ilikuwa inamwambia hakufungisha bao kwa makusudi. Inawezekana dhamira yake pia ilimwambia hakuona kosa lolote alilofanya kuelekea katika bao la Okello. Hata hivyo, mabadiliko ya kocha wake na benchi la ufundi nayo yanatuachia maswali mengi. Kwamba wanahisi Metacha aliwafungisha kwa makusudi?
Au kwamba hakuwafungisha kwa makusudi lakini alifanya uzembe kwa kosa la kimchezo ambalo wamekuwa wakijaribu kulisahihisha katika uwanja wa mazoezi kila kukicha. Vyovyote ilivyo mashabiki wa mpira wetu kwa dakika hizi za lala salama lazima watajikita katika hisia hizi za kwanza. Kwamba Metacha alikuwa amefungisha kwa makusudi. Mashabiki hawahitaji uchambuzi wangu wa kimchezo wa namna ambavyo Metacha alikuwa amefungwa.
Nadhani hata benchi la ufundi la Singida Big Stars halihitaji uchambuzi wangu wa kitaalamu wa kosa la Metacha ambalo pia limewahi kufanywa na makipa mbalimbali. Tunaamini kwamba hakuendana na suluhisho la msingi la namna ya kukabiliana na mpira ule. Tupo katika mechi za mwisho mwisho za msimu na tunarudi kule kule ambako huwa tunakuwepo wakati ligi inapokaribia kufika tamati.
Siku moja kabla ya kosa la Metacha kipa wa Coastal Union naye alionekana mzembe kwa kuruka kwa chini wakati mpira wa Libasse Gueye ulipokwenda kwa juu. Na sasa hatujadili tena ubinadamu wa makipa. Akili yetu inatupeleka moja kwa moja kwamba makipa wanahongwa. Upande mmoja utasema kipa kahongwa. Upande ambao umefaidika utazungumzia uhodari wa mpigaji.
Sasa zimebakia mechi chache ligi kumalizika. Suala la rushwa linazungumzwa bila ya hofu. Kawaulize watu wa benchi la ufundi wa Singida. Hisia zao zitakuwa Metacha amewauza. Basi. Hawaamini amefanya kosa la kizembe kwa bahati mbaya kwa mujibu wa kazi yake. Kuna makocha wanawaadhibu wachezaji wao papo kwa papo kwa mujibu wa makosa yao lakini wanaamini wachezaji wamekuwa wakifanya uzembe na siyo suala la rushwa.
Ndiyo, mchezaji anafanya makosa ambayo yanajirudia mara kwa mara na kocha anaamua kumuweka benchi na hata kumuuza. Hata hivyo, kocha anaamini zaidi katika makosa ya kimsingi ya mchezaji na siyo mchezaji amechukua rushwa au vinginevyo. Sisi hatuna ubinadamu katika hilo hasa katika dakika hizi za msimu. Ingekuwa mechi ya kwanza ya msimu tungeamini katika uzembe wa kawaida wa mchezaji. Dakika hizi za lala salama hatuamini katika uzembe wa kawaida.
Siyo Metacha tu. Tulipofika hata mwamuzi akikosea kibinadamu tunaamini amehongwa. Kuanzia sasa hakuna cha msalie mtume. Hatuna muda wa kufanya tafakuri ya kisayansi ya kosa la mwamuzi. Ni suala la kuamini mwamuzi ameohongwa au kipa amehongwa au mchezaji aliyesababisha penalti ameohongwa. Kwa nini tumefika hapa? Hauwezi kulaumu sana wenye hisia hizi kwa sababu haya mambo yapo katika mpira wetu.
Ni kama Yanga walivyokataa kwenda katika vyumba vya kubadilishia nguo pale uwanja wa Isamuyo na wakaamua kwenda katika nyumba ya jirani. Walihofia nini? Walihofia watani zao walikuwa wamechezea chumba chao. Sio kwamba Yanga ni wajinga. Walihofia kitu ambacho kipo. Sasa hivi haya mambo yanazungumzwa kwa uwazi zaidi tofauti na zamani. Mpira wetu tunasema umekua lakini kuna makandokando mengi kando yake.
Makandokando ambayo yanatia aibu kuyazungumza kwa mgeni aliyetoka mbali kuja kushuhudia mechi za ligi yetu. Kuna vitu akiambiwa hawezi kuamini. Ni sawa na mgeni ambaye alikwenda kushuhudia pambano la Yanga dhidi ya Singida Big Stars. Akiambiwa Metacha aliondolewa uwanjani kwa sababu ya tuhuma za kufungisha makusudi anaweza asiamini. Yeye ataamini kocha alimtoa uwanjani kwa sababu alifanya makosa ya msingi ya kazi yake bila ya kuwa na dhamira mbaya.
Sijui ni lini tutaondokana na hali hii lakini inatia aibu. Tunazungumza kuhusu rushwa na kupuliza dawa za ovyo katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa uwazi kabisa. Wala hakuna kificho. Kitu pekee ambacho wahusika watajitetea ni kukwambia ukalete ushahidi. Basi. Na kwa sababu hilo haliwezekani kiurahisi basi tutaendelea tu na maisha haya kwa muda mrefu.
Mitandao ya kijamii nayo imeupeleka mpira wetu katika presha kubwa. Upinzani ni mkubwa na tunalazimika kushinda kwa gharama yoyote ile. Kisa? Tukishindwa wale jamaa wa upande wa pili wataongea sana. Ni kama ambavyo Yanga waliungwa mkono kwa juhudi zote na mashabiki zao wakati walipogomea kuingia katika vyumba vya Isamuyo. Mashabiki wakachanga shilingi milioni 30 za faini ya bodi ya ligi.
Waliamini sare yao dhidi ya mtani ilitokana na maamuzi ya viongozi wao kutoipeleka vyumbani timu yao. Mashabiki wanaamini bora maamuzi ya viongozi wao kuliko kelele ambazo zingekuwepo mtaani kama wangefungwa na mtani. Siku hizi, kuliko wakati mwingine wowote ule presha imekuwa kubwa katika simu kuliko mitaani.
Tusubiri kuona mwisho mechi za mwisho za msimu zitakwendaje. Sidhani kama akina Metacha watakuwa salama. Sidhani kama waamuzi watakuwa salama. Kila kosa ambalo watalifanya tutaliangalia kwa upande ule mwingine mwingine. Hatutaliangalia katika upande wa kibinadamu. Ndivyo ulivyo mpira wetu. Hata hivyo haya mambo yapo. Yanafanywa.