Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sayansi ya Yao Kouassi imeeleweka, bado Mzize

JICHO Pict


MATUMIZI ya akili ya kawaida sio kitu cha kawaida na wanadamu wengi huwa hawapendi kutumia akili ya kawaida. Wazungu huwa wana msemo wao ‘common sense is not common, why people don’t use it?’.


Nimemwona Yao Kouassi uwanjani hizi siku za karibuni. Nimekumbuka mbali. Nimekumbuka matumizi ya akili ya kawaida ambayo Injinia Hersi Said na genge lake la ‘wahuni’ wametumia pale Yanga katika suala zima la Yao kurudi uwanjani. Wametumia akili nzuri ya kawaida ambayo mpaka sasa hivi wengi hawatumii. Zamani tulikuwa hatutumii kabisa akili hii ya kawaida.


Msimu uliopita Yao alikuwa nje kwa muda mrefu. Na msimu huu Yao amekuwa nje kwa muda mrefu. Majeraha yalimtupa nje ya uwanja lakini Yanga haikumtupa.

Yanga walitumia akili ya kawaida tu. Unampataje mlinzi wa kulia kiurahisi katika bara la Afrika mwenye uwezo wa Yao Kouassi. Sio kitu rahisi sana. Hata hapa nchini kuna walinzi wengi wazuri wa kushoto kuliko wa kulia.

JICH 01

Kuanzia walinzi wazawa hadi wale wa kigeni. Upande wa kushoto kuna watu wengi imara. Mohamed Hussein Tshabalala anaweza kuwa anaongoza lakini kuna Pascal Msindo pale Azam, kuna Nickson Kibabage pale Simba, kuna Chadrack Boka Yanga, kuna Valentin Nouma pale TRA. Huku upande wa kulia kuna uhaba mkubwa. Shomari Kapombe anawaacha wengine mbali.

Shomari anawaacha mbali akina Duchu, Lusajo Mwaikenda na Israel Mwenda. Ni wazuri lakini Shomari ana daraja la peke yake kwa muda mrefu. Huku kushoto pengo sio kubwa sana kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine. Haishangazi kuona huku kulia akina Hersi wakaamua ‘kufa’ na majeraha ya Yao Kouassi. Hawakufanya ujinga. Aliendelea kulipwa mshahara mzuri na kupelekwa hospitali nzuri nje ya nchi kwa ajili ya operesheni na matibabu kwa ujumla.

JICH 02

Akili ya kawaida kabisa ni kwamba Yanga wamekuwa juu katika miaka ya karibuni. Ni kweli pengo la Yao limekuwepo wakati akiwa nje ya uwanja. Usingweza kuliona mpaka aliporudi. Hata hivyo waliendelea kufanya vizuri kwa sababu wana timu nzuri. Hapo ndipo walipoficha mapungufu yao ya kutokuwa na Yao. Na iliwasaidia mpango wao wa kumtibu Yao kimya kimya huku akiendelea kupokea mshahara mzuri.

Labda wangekuwa wapo pabaya wangeamua kuachana naye moja kwa moja na kutafuta beki wa kigeni katika nafasi yake ashindane na Mwenda. Waliamua kutumia akili nzuri ya kuendelea kumtibu Yao. Beki mwingine wa kigeni angeweza kuwa ghali na pia asingekuhakikishia ubora wa Yao Kouassi.

JICH 03

Sio mabeki wengi wa pembeni ambao wanafikia ubora wake. Hakuna ambaye angekuhakikishia ubora wake.

Ndani ya misimu miwili Yanga wangeweza kumleta mchezaji wa kigeni au kuleta wachezaji wa kigeni wacheze katika nafasi ya Yao na wangeweza kugharimu kiasi kikubwa cha pesa kuliko kiasi kilichotumika kumtibu Yao arudi uwanjani. Tumewahi kupotoka mara nyingi katika jambo hili kwa sababu hatukutumia akili ya kawaida.

Zamani timu zetu zilikuwa na ukata. Zisingeweza kumlipa mchezaji mwenye majeraha na zisingeweza kumtibu nje ya nchi. Kuna wachezaji wengi ambao walipotea kwa namna hii. Mchezaji anapata majeraha ambao hapa nchini hayatibiki vema na uwezo wa kumpeleka nje haupo. Maisha yake ya soka yanaishia hapo. Tumepoteza wachezaji wengi mahiri zamani.

Akina Injinia Hersi wamefanya vema kwa sababu kuna aina ya wachezaji ambao unaweza kuwasubiri huku nafasi zao zikiwa zinashikiwa kwa muda. Yao ni aina ya wachezaji hawa. Unajua kabisa ni mchezaji wa daraja gani. Unajua kwamba umri haujaenda. Unaamua tu kumsubiri. Kwanza ni ubinadamu lakini pia mchezaji anakuwa mzalendo kwako pale anaporudi uwanjani.

JICH 04

Mchezaji ambaye hauwezi kumsubiri sana ni yule ambaye kwanza hauna na uhakika na ubora wake, lakini pia kuna wachezaji wengi wenye ubora ambao wanaweza kucheza katika nafasi yake. Kwa mfano, pale pale Yanga hauwezi kupoteza muda kumtibu na kumsubiri Mohamed Damaro arudi uwanjani baada ya kukaa nje kwa muda mrefu. Nafasi yake hata Khalid Habib Idd ‘Gego’ anaweza kuitendea haki.

Mchezaji mwingine ambaye hauwezi kumsubiri ni yule ambaye ana majeraha ya mara kwa mara. Kuna tofauti kati ya mchezaji ambaye anaumia mara moja na kukaa nje muda mrefu na yule ambaye anarudi uwanjani mara kwa mara lakini pia anaumia mara kwa mara. Huyu wa aina ya pili wazungu wanamuita ‘injury prone’. Pale Arsenal waliwahi kuwa na mchezaji kama huyu. Aliitwa Abou Diaby.

Baada ya sayansi hii kufanya kazi kwa Yao Kouassi, sasa ni kuangalia kama inaweza kufanya kazi kwa Clement Mzize. Tungeweza kumjadili Mzize siku nyingine lakini sio mbaya kumjadili leo kwa sababu Yanga wanajaribu kutumia akili ya kawaida ambayo zamani tusingeitumia. Yanga wameingia mitihani miwili kwa Mzize.

Kwanza kabisa waliingia mtihani wa kutakiwa kumuuza kwa pesa nyingi. Waligoma. Yanga waligomea hadi dola 1.5 milioni kutoka kwa Waarabu wa Libya. Baada ya kuushinda mtihani huu wamekumbana na mtihani mwingine wa Mzize. Ameumia kwa muda mrefu sasa. Yanga wamelipia operesheni yake Afrika Kusini na wamemsubiri uwanjani kwa muda mrefu.

Wamemsubiri huku wakiendelea kumlipa mshahara mkubwa. Ni kamari ambayo wanaicheza lakini bado nawapa dhamana Yanga. Unapata wapi kirahisi mshambuliaji kama Mzize ndani na nje ya nchi. Ni mshambuliaji hasa. Ni bora uendelee kumtibu huku ukisubiri arudi uwanjani kuendelea kumalizia pale alipoishia.

Kama washambuliaji wenyewe wanaoletwa ni kama Yikpe au Andy Boyeli basi ni bora kulipia gharama za matibabu ya Mzize ukiwa unajua kitu ambacho anaweza kukupa uwanjani. Ni akili ya kawaida. Unaweza kuhaha kutafuta mrithi wa Mzize baada ya kuamua kumpotezea ajiuguze mwenyewe kisha ashindwe kuendelea kucheza na soka wakati huo huo unatumia gharama nyingi kuchukua wachezaji ambao hauna uhakika nao.

Tumewahi kufanya huko nyuma. Akili hii ya kawaida hata Azam wamekuwa wakiitumia kwa wachezaji wao. Mfano ni Idd Nado ambaye wamemuuguza kwa muda mrefu. Amepona na amewarudishia makali yao. Kuhaha kumtafuta mchezaji kama yeye ni tatizo kubwa. Wazungu wamekuwa wakitumia akili hii kwa muda mrefu.

Inawezekana tumekabiliwa na ukata kwa muda mrefu lakini kwa timu ambazo zinajiweza hii akili ambayo Yanga wametumia kwa Yao ni akili ya kawaida tu hasa kwa nyakati hizi ambazo mpira umepungukiwa vipaji. Kuna wachezaji bora uwauguze wapone kuliko kurukiarukia wachezaji wengine ambao hauna uhakika na uwezo wao na bado utatumia pesa ndefu.