Prime
Tuliagiza viberiti kutoka nje, sasa tunaagiza waamuzi
HATIMAYE waamuzi wetu wametufikisha hapa. Waamuzi kutoka Tanzania wametufikisha hapa tulipo. Tunaagiza viberiti kutoka nje. Tunaagiza sabuni kutoka nje. Na sasa tunaagiza waamuzi wa kuchezesha pambano la soka la Simba na Yanga kutoka nje. Tumefikaje hapa? Kuna sababu nyingi.
Pale Unguja mwamuzi wa pambano la watani fainali ya michuano ya Muungano alitoka Kenya. Tusingeweza kumwamini mwamuzi kutoka Pemba, Karatu, Ilala au Lindi. Leo kunatarajiwa kuchezwa pambano jingine la watani na mwamuzi alitarajiwa kutoka Morocco. Kabla ya hapo pambano la mwisho la msimu uliopita mwamuzi wake alitoka katika ardhi ya Mafarao, Misri.
Sasa hivi imeanza kuonekana suluhisho la msingi la mechi hii ni kuleta waamuzi kutoka nchi jirani. Kisa? Kufuta lawama. Kwamba tunawaamini zaidi waamuzi wa nje lakini sababu kubwa ya msingi ya wanaowatafuta waamuzi wa nje ni hawataki lawama, ionekane waliwapanga waamuzi fulani kwa sababu ya masilahi yao.
Hatuwaamini waamuzi wetu kwa sababu mbalimbali. Hadi leo hatujapata majibu ya maswali matatu. Wanahongwa? Wana mapenzi binafsi na timu? Au hawajui sheria? Binafsi naamini waamuzi wetu wanajua sheria. Ukikaa nao meza za baa wanakutajia mambo mengi ya kisheria ambayo unajikuta ukiamini wanajua sheria. Tatizo linabakia pale pale, hatujapata majibu halisi.
Waamuzi kutoka nje hakuna kitu kikubwa wanachotupa zaidi ya imani. Kwamba tunaamini hawawezi Yanga wala Simba. Hapo hapo tunaamini wao ni bora kuliko waamuzi wetu. Siyo kweli. Tukipata majibu ya maswali matatu kuhusu waamuzi wetu nadhani hatuhitaji waamuzi kutoka nje. Kuna mambo mengi.
Kuna waamuzi wetu ambao wanahongwa. Kuna waamuzi wetu ambao wanakosea binadamu. Sioni kama kuna suala la waamuzi wetu kuwa na mapenzi binafsi na hizi timu. Hili la kuhongwa na kukosea kibinadamu ndio kubwa zaidi na mstari mwembamba wanaoupitia ndio ambao umesababisha tulete waamuzi wengi kutoka nje.
Mfano, mwamuzi wa pambano la Singida Big Stars dhidi ya Simba msimu uliopita aliwanyima Singida Big Stars penalti za wazi. Pia tuna waamuzi ambao wamekuwa wakikosea kibinadamu katika mechi kama hizo. Ahmed Arajiga aliwapa Simba penalti fulani msimu huu na wote tuliotazama katika marudio tuliamini Libasse Gueye alimdanganya Arajiga.
Katika hali hii wote tungekuwa Arajiga tungeweka penalti. Hapa unaamini katika makosa ya kibinadamu huku ukizingitia Arajiga hakuwa na msaada wa VAR. Tunapata shida kupita katika mstari huu mwembamba kwamba waamuzi wanahongwa au wana makosa ya kibinadamu. Inavyoonekana wale wanaomini waamuzi wana agenda zao binafsi ni wazi wameshinda.
Waamuzi wetu wameshindwa kutengeneza imani na ndiyo maana tunaleta waamuzi kutoka nje. Inaonekana upande wa wanaoamini waamuzi wanahongwa au wana mapenzi na timu fulani wameshinda. Na sasa tunaleta waamuzi kutoka nje kwa sababu ya sisi kukosa imani na waamuzi wa ndani. Aibu iliyoje. Waamuzi hawa hawa ambao tumekosa nao imani ndio ambao wanachezesha mechi za CAF nje ya nchi na hatusikii kama wamekosea.
Tukubali baada ya ujinga mwingi wa baadhi ya waamuzi sasa hivi tumefika hapa tulipo. Siyo kwamba hatuna waamuzi bora, hapana. Wanajua sheria na wanajua wana uwezo wa kuzitafsiri. Tatizo ni wanaamua kufanya makusudi mambo ambayo wanayafanya. Wakati haya yakitokea tumetoa fursa kwa waamuzi wa nje ambao wana tabia kama za waamuzi wetu kuchezesha mechi zetu.
Haijawahi kufikia mahala pambano muhimu la Ligi Kuu England linahitaji mwamuzi kutoka Hispania au Ujerumani kwa sababu mbili. Kwamba wana hofu kuwa mwamuzi anaweza kuwa mtu wa upande mmoja au anaweza kuwa amehongwa. Ni hivyo hivyo katika nchi nyingine za Ulaya. Pambano la ligi linachezeshwa na waamuzi kutoka taifa husika.
Matokeo yake licha ya kuweka imani yetu kwa waamuzi kutoka nje inaonekana kama tumeanza kujisumbua tu.
Nilimkubali mwamuzi wa nje kutoka Misri aliyechezesha pambano la mwisho la msimu uliopita lakini huyu wa majuzi kutoka Kenya alikuwa kama waamuzi wetu. Aliamua kuacha kadi zake mbili hotelini na kuchezesha pambano letu muhimu.
Unashangaa ni kwa namna gani Mohamed Damaro aliondoka uwanjani bila ya kadi ya njano. Unashangaa namna gani Yusuf Kagoma pia aliondoka uwanjani bila ya kadi. Mchezaji anacheza rafu ya kwanza mbaya, kisha anacheza nyingine mbaya lakini mwamuzi anaamua kuanzisha naye maongezi bila ya kutoa kadi yoyote.
Kuna yule mchezaji ambaye alimvuta Djigui Diarra wakati akijaribu kuanzisha shambulizi. Hakupewa kadi yoyote na mwamuzi. Nadhani mwamuzi kutoka Kenya alikuja na akili ya kumiliki pambano kwa kutoonyesha kadi zozote za ovyo. Alichokosea ni kuna wakati inabidi ufuate sheria siyo hisia. Kuna kadi ambazo zinabakia katika mamlaka ya mwamuzi. Kuna kadi ambazo zinapaswa kuwa kwa mujibu wa sheria.
Ninachohofia ni baada ya mechi za Simba na Yanga baadae tutahamia katika mechi za Simba na Azam au Yanga na Azam. Itafika mahala Azam nao watasema wanahitaji kutoka mwamuzi kutoka nje. Wanaweza kwenda mbali na kudai wapo tayari kulipa hata gharama za mwamuzi husika. Tusiupeleke mpira wetu huko. Kuna mambo lazima yafanyike.
Jambo la kwanza waamuzi wetu waanze kuona aibu na kujirudi. Wapambane kweli kweli kujirudi. Kila siku tutapambana na wageni wanavyojipatia ajira kirahisi nchini. Utafiti unaonyesha wapo wengi wanaopata ajira kutokana na uzembe wetu. Ili la waamuzi ni miongoni ni miongoni mwa mifano dhahiri. Ni uzembe wao ndio ambao umetufikisha hapa.
Lakini kuna sura nyingine. Kwa nini wakubwa wetu, hasa wa Kariakoo, wanahofia sana la weledi wa waamuzi. Wanajua wanachofanya nyuma ya pazia ndio maana wanajua waamuzi wetu wanaweza kutoka na maamuzi yao mfukoni tangu wakiwa nyumbani. Wao wenyewe wana ushuhuda na mambo mengi machafu ambayo wamewahi kuyafanya nyuma ya pazia.
Labda imapokaribia mechi yao huwa wana hofu huenda upanda mwingine ukawa umewazidi kete kuelekea katika pambano husika. Hapo ndipo wote wanapokubaliana acha mwamuzi atoke nje. Wachawi huwa wanajuana. Wachawi huwa hawaaminiani. Nilidhani wao wangesimama kwa sauti moja kutotaka waamuzi watoke nje. Lakini wote wanakubaliana kwa sababu wanajua waamuzi wetu ni wepesi.
Pia kuna jambo jingine. Tuache kuwahukumu waamuzi wetu kwa makosa madogo madogo na kuyakuza. Waamuzi wetu wamekuwa katika presha kubwa kwa sababu tumewaondoa katika ubinadamu wao. Tumewafanya kuwa malaika. Kuna makosa mengi ambayo wameyafanya kwa sababu walihitajika kuchukua maamuzi ndani ya sekunde tano tu. Sisi tuna nafasi kubwa ya kuhukumu makosa yao kwa sababu tunatazama picha za marudio.
Kuna makosa ambayo tunajua mwamuzi ni mpuuzi na amedhamiria kuibeba timu fulani lakini kuna makosa ambayo inabidi tuwe upande wa mwamuzi kuwa alihitaji msaada zaidi katika kuchukua maamuzi. Ndiyo maana wazungu walileta VAR. Tatizo letu kila kosa la mwamuzi tunahukumu alihongwa au ana mapenzi na timu nyingine.
Sasa Tanzania inataka kuagiza kila kitu kutoka nje. Mfano tunaagiza viberiti kutoka China wakati mti wa kiberiti unatoka Mafinga pale Iringa. Ni kama tulivyomuagiza mwamuzi wa majuzi akatuamuliwa mechi pale Unguja wakati ubora wake upo chini dhidi ya waamuzi wetu wengi tu.