Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hesabu za Taifa Stars AFCON 2027

STARS Pict

Muktasari:

  • Mchezo huo wa Kundi L, utakuwa wa kwanza kwa Taifa Stars katika kampeni hiyo, ingawa tayari imekata tiketi ya kushiriki fainali hizo kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda.

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo itaanza safari ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kuikabili Guinea-Bissau mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, huku ikibeba dhamira ya kuanza kampeni hiyo kwa ushindi.

Mchezo huo wa Kundi L, utakuwa wa kwanza kwa Taifa Stars katika kampeni hiyo, ingawa tayari imekata tiketi ya kushiriki fainali hizo kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda.

Pamoja na hilo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, amesema tiketi waliyonayo haitapunguza ushindani wala umuhimu wa mchezo wa leo.

Gamondi amesema Taifa Stars imejiandaa kuingia uwanjani kwa mtazamo wa timu inayotafuta ushindi, akisisitiza kuwa mechi hizo hazipaswi kuchukuliwa kama za kirafiki kwa sababu Tanzania tayari imefuzu.

STAR 01

“Hata kama tumeshafuzu, hatutaichukulia mechi hii na ile ya Madagascar kama mechi za kawaida. Tunataka kucheza kwa bidii na kushinda,” amesema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina aliongeza kuwa, kwake dakika 90 za mchezo huo zinapaswa kuwa za ushindani, huku akimtaka kila mchezaji kujituma na kuepuka makosa ambayo yanaweza kuamua matokeo ya mchezo.

“Kwangu hii sio mechi ya kirafiki. Ni dakika 90 za kujaribu kushinda. Baada ya kushinda au kufungwa, hiyo ni historia nyingine. tunalipwa kwaajili ya kushinda sio kufungwa,” amesema.

Gamondi amewataka wachezaji kuwa makini kwa dakika zote, akisema tofauti katika mechi za aina hii inaweza kuamuliwa na jambo dogo, hivyo hawatakiwi kupoteza umakini.

“Hakuna nafasi ya kufanya makosa. Tunahitaji kuwa makini wakati wote wa mchezo,” alisisitiza Gamondi.

STAR 02

Mchezo huo pia unampa Gamondi nafasi ya kuendelea kujenga kikosi kitakachoiwakilisha Tanzania katika fainali za AFCON 2027, huku akitumia mechi za ushindani kuwajenga wachezaji, kuimarisha muunganiko wa timu na kuendeleza utamaduni wa kutafuta ushindi.

Miongoni mwa sura mpya zinazovuta macho katika kikosi hicho ni mshambuliaji Bernard Kamungo, ambaye amejiunga na taifa Stars kwa mara ya kwanza.

Kamungo, anayekipiga FC Dallas ya Marekani, ameitwa katika kikosi hicho huku akiwa miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars.

Mbali na Kamungo, Taifa Stars imeingia kambini ikiwa na mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na wale wanaoendelea kujenga nafasi zao katika timu ya taifa, huku baadhi ya nyota wanaocheza nje ya nchi wakijiunga na kikosi kadiri maandalizi yalivyoendelea.

Kwa upande mwingine, Guinea-Bissau nayo imewasili Tanzania ikiwa na lengo la kuanza kampeni yake kwa matokeo mazuri, jambo linalotarajiwa kufanya mchezo wa leo kuwa na ushindani mkubwa tangu mwanzo.

Taifa Stars inatarajiwa kutegemea faida ya kucheza nyumbani pamoja na msukumo wa mashabiki wa Zanzibar katika kusaka ushindi.

Baada ya mchezo wa leo dhidi ya Guinea-Bissau, Taifa  Stars itaelekea Morocco kwa ajili ya mchezo wake wa pili wa Kundi L dhidi ya Madagascar, utakaochezwa Septemba 29, nchini humo.

STAR 03

Kuhusu mechi hizo mbili, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, amesema upinzani watakaoupata dhidi ya Guinea Bissau na Madagascar utatoa picha ya maandalizi ya Taifa Stars kuelekea fainali hizo.

Msuva, anayeichezea Newroz ya Iraq, amesema michezo hiyo ina umuhimu mkubwa kwao kwa sababu inawapa nafasi ya kujipima na kuona namna wanavyoweza kukabiliana na ushindani mkubwa wa Afcon.

“Mechi hizi ni muhimu sana kwetu kwa sababu zinatupa picha ya namna tulivyojiandaa na tunataka kufanya nini kuelekea Afcon. Tunahitaji kucheza kwa umakini, kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyataka,” amesema Msuva.

Mshambuliaji huyo mwenye uzoefu mkubwa wa Taifa Stars, ana rekodi ya kucheza mechi 80 za kimataifa za FIFA akiwa amefunga mabao 25, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa katika kikosi hicho.

Msuva pia amekuwa sehemu ya kikosi cha Tanzania katika fainali za Afcon zilizopita, akiwamo kwenye timu iliyoshiriki michuano ya mwaka 2019, 2023 na 2025 huku uzoefu huo ukiwa sehemu muhimu ya mchango wake kwa Stars.

Akiwa katika soka la kulipwa nje ya Tanzania, Msuva amepitia ligi za mataifa mbalimbali zikiwemo Morocco, Saudi Arabia na Iraq, ambako ameendelea kujenga uzoefu wa kucheza katika mazingira tofauti ya ushindani.

“Kuwa wenyeji ni jambo kubwa na ni heshima kwa Tanzania, lakini hilo pekee halitoshi. Lazima sisi wachezaji tujiandae vizuri, tujenge morali na kila mchezo tucheze kwa malengo makubwa,” amesema.

Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, katika fainali ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza kwa ushirikiano wa nchi hizo tatu za Afrika Mashariki kuanzia Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027.