Huku ukizubaa tu umeachwa
Muktasari:
- KMC imeanza msimu kwa kasi, ikijivunia safu yake ya ushambuliaji iliyofunga mabao 11 katika michezo mitatu, ikiwa ni ishara ya dhamira ya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara msimu ujao.
LIGI ya Championship msimu wa 2026/27, imeendelea leo Jumamosi kwa michezo mitatu, huku kesho Jumapili vinara wa ligi hiyo, KMC, wakitarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, kuvaana na Bandari Tanzania.
KMC imeanza msimu kwa kasi, ikijivunia safu yake ya ushambuliaji iliyofunga mabao 11 katika michezo mitatu, ikiwa ni ishara ya dhamira ya timu hiyo kurejea Ligi Kuu Bara msimu ujao.
KMC ndiyo timu pekee iliyoshinda michezo yote mitatu ya mwanzo, baada ya kuanza kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mbuni FC ya Arusha, ikaichapa Bigman FC ya Tanga 3-1 na wiki iliyopita kuifunga KenGold FC ya Mbeya mabao 3-0.
Hata hivyo, Bandari Tanzania, ambayo ni miongoni mwa timu mpya katika Championship, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupata pointi nne katika michezo yake mitatu ya kwanza ya ligi.
Timu hiyo ilianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KenGold FC ugenini, ikaichapa Gunners FC ya Dodoma bao 1-0 kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Mbeya Kwanza.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa Bandari Tanzania kucheza nyumbani tangu ipande daraja, jambo linaloongeza hamasa kwa timu hiyo ambayo ilifanya usajili wa nyota kadhaa wenye majina makubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Bandari Tanzania, Habibu Kondo, alisema pointi nne walizokusanya katika michezo mitatu ya ugenini si matokeo mabaya, huku kurejea nyumbani kukiwapa nguvu zaidi ya kupambana.
“Tunahitaji kuonyesha kiwango kizuri mbele ya mashabiki na uongozi wetu kwa ujumla. Tunatambua kiu waliyonayo, hasa ya kuiona timu ikicheza Mtwara, hivyo tuko tayari kutoa burudani nyumbani, licha ya ukweli kwamba ligi ni ngumu msimu huu,” alisema Kondo.
KMC ilishuka daraja baada ya kumaliza nafasi ya 16 ikiwa na pointi tisa katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/26, lakini imeanza Championship kwa kishindo na sasa imejikita kileleni.
Mbali na mchezo huo, leo Jumamosi maafande wa Tanzania Prisons, chini ya Kocha Shadrack Nsajigwa, watakuwa wenyeji wa Songea United kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Prisons, yenye ushindi wa michezo miwili na kipigo kimoja, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Mbuni FC ya Arusha mabao 2-0.
Kwa upande wa Songea United, ambayo bado inatafuta ushindi wake wa kwanza msimu huu, inatoka sare ya bila kufungana na IAA SC ya Arusha.
Nsajigwa anafahamu jukumu lililo mbele yake baada ya timu hiyo kushuka daraja, huku uongozi ukiendelea kuweka imani kwake kuhakikisha Prisons inaanza safari ya kurejea Ligi Kuu.
Mjini Morogoro, mabingwa wa Ligi Kuu msimu wa 1999 na 2000, Mtibwa Sugar, wataikaribisha Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Manungu Complex.
Mtibwa bado haijaanza vizuri msimu huu, ikiwa nafasi ya saba na pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja, sare moja na kupoteza mmoja.
Wakiwa mbele ya mashabiki wao, Mtibwa wanahitaji ushindi ili kuendelea kusaka nafasi ya kurejea kwenye kiwango kilichowawezesha kutwaa ubingwa wa Championship kakika misimu miwili iliyopita.
Mkongwe Juma Liuzio, aliyefunga mabao mawili hadi sasa, ataendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya Mtibwa katika harakati za kusaka pointi tatu.
Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Mtibwa italazimika kuwa makini na mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Abiud Mtambuka, anayesimama kileleni mwa orodha ya wafungaji akiwa na mabao manne katika michezo mitatu.
Mchezo mwingine wa leo utapigwa Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga, ambapo Stand United maarufu ‘Chama la Wana’, itaikaribisha Rhino Rangers ya Tabora.
Stand United, iliyo nafasi ya tano ikiwa na pointi sita, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 na itahitaji ushindi ili kusogea juu zaidi kwenye msimamo.
Rhino Rangers, mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025/26, ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba.
Silaha yao kubwa ni mshambuliaji Zuberi Malila, aliyefunga mabao mawili hadi sasa, huku safu yao ya ulinzi ikiwa haijaruhusu bao katika michezo mitatu iliyopita.
Kesho Jumapili, ligi hiyo itaendelea kwa Kigamboni United, zamani B19 FC, itakayoikaribisha KenGold FC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kigamboni United inarejea uwanjani ikiwa imetoka sare ya bao 1-1 na Gunners FC ya Dodoma, huku ikisaka ushindi wa kujiimarisha kwenye msimamo.
Mapema jana ilichezwa michezo mitatu kwa TMA FC iliyokuwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini, Mbeya kuikaribisha Bigman FC ya Tanga, huku maafande wa Transit Camp ikicheza dhidi ya IAA SC ya Arusha kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam.
Mbuni FC ilikuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini Arusha kuikaribisha Gunners FC kutoka Dodoma iliyotoka sare mbili na kupoteza moja kati ya tatu hadi sasa.
Uhondo mwingine wa ligi hiyo upo katika vita ya kuwania ufungaji bora tayari mshambuliaji Abiud Mtambuka wa Mbeya Kwanza kwanza amefunga mabao manne, akifuatiwa kwa karibu na nyota wawili wa KMC, Ramadhan Hashim, Adam Uledi wote wamefunga mabao matatu kila moja.
Mbali ya hao kuna wakongwe nao hawapo nyuma tayari wameandika majina yao katika ufungaji wakiongozwa na Juma Liuzio wa Mtibwa Sugar amefunga mabao mawili wengine wamefunga bao moja ambao ni Sixtus Sabilo (Bandari TZ), Abrahaman Mussa (Gunners FC) na Shaaban Kisiga (Transit Camp) pamoja na Peter Mwalyanzi (Mtibwa Sugar).