Prime
Ishu ya Diarra kuondoka Yanga iko hivi

Muktasari:
- Diarra anamaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu na inadaiwa anajiandaa kuondoka baada ya kupata dili la maana nje ya nchi ambalo mabosi wameridhia, lakini Hamdi amesema hana taarifa, lakini kama kuna ukweli hatakubali aondoke.
MASHABIKI wa Yanga wamekuwa na presha baada ya kuenea taarifa kwamba kipa namba moja Diarra Djigui anajiandaa kuondoka, lakini kocha mkuu Miloud Hamdi ameweka msimamo, huku akiwatoa hofu mashabiki hao.
Diarra anamaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu na inadaiwa anajiandaa kuondoka baada ya kupata dili la maana nje ya nchi ambalo mabosi wameridhia, lakini Hamdi amesema hana taarifa, lakini kama kuna ukweli hatakubali aondoke.
Kocha huyo alisema haitakuwa rahisi kuruhusu Diarra kuondoka mwishoni mwa msimu kama mabosi wa klabu hiyo hawataleta kipa bora mbadala.
Diarra anayeitumikia Yanga kwa msimu wa nne tangu aliposajiliwa kutoka Stade Malien ya Mali amekuwa nguzo imara ya lango la timu hiyo akiisaidia kubeba mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara na matatu ya Kombe la Shirikisho, mbali na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini inaelezwa mkataba wake upo mwishoni na bado hajasaini mpya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema hana taarifa juu ya kipa huyo kuondoka na kama ni kweli bado hayupo radhi kumruhusu, ila kwa sharti la kuletewa kipa mwenye uwezo zaidi ya Diarra, kwani anafahamu soko la makipa lilivyo gumu.
“Kumuachia Diarra sio rahisi kama inavyozungumzwa. Shida ni moja kupata kipa wa aina yake ni kazi ngumu. Kila mtu anafahamu uwezo wake ulivyo msaada ndani ya timu hii,” alisema.
“Naweza kuruhusu aondoke kama tu nitaletewa kipa bora mwenye uwezo mkubwa zaidi yake kwa sababu najua huko nje wapo kina Diarra wachache mno wenye uwezo wa kudaka na kuanzisha mashambulizi kama alivyo yeye.”
Juu ya rekodi ya kipa huyo kwa msimu huu ikionekana kushuka kulinganisha na mitatu iliyopita, Hamdi alisema haangalii sana makosa ya msimu huu, kwani siyo yake pekee bali safu nzima ya ulinzi, hivyo hakuna cha kulaumiwa.

“Msimu huu unaweza kusema haukuwa bora kwa kipa huyo, lakini sijali kuhusu mabao aliyoruhusu kwani yanatokana na safu nzima ya ulinzi na wala hayaondoi ubora wa Diarra. Ni bahati tu Diarra anacheza Tanzania, lakini kwa ubora alionao anaweza kucheza hata Ulaya, hivyo anatakiwa apongezwe sana kwani ameisaidia timu.”
REKODI ZAKE
Safari ya Diarra katika soka ni tamu kwa misimu minne aliyopo Jangwani akicheza mechi nyingi za michuano mbalimbali zikiwamo za ligi na kuipa mafanikuio Yanga ikiwamo medali ya CAF.
Kipa huyo raia wa Mali alitua Yanga msimu wa 2021/22 akitokea Stade Malien ya kwao Mali huku akiwa miongoni mwa makipa bora kikosini huko.
Tangu ajiunge na Yanga ameibuka kuwa shujaa si tu katika Ligi Kuu bali hata michuano ya kimataifa timu yake ikicheza fainali Kombe la Shirikisho, lakini pia ikifika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Achana na ubora wa kikosi cha Yanga, hata hivyo Diarra amethibitisha ubora kutokana na namba alizonazo tangu alipotua.
Hizi hapa ni namba za kipa huyo aliyebakiza mechi nne kumaliza msimu wake wa nne akiwa kipa namba moja kwenye kikosi hicho chini ya makocha Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na sasa Miloud Hamdi.
88
Idadi ya mechi alizocheza akiwa ndani ya kikosi cha Yanga akifungwa mabao 34 pekee kwenye misimu minne aliyocheza hadi sasa akiwa amebakiwa na mechi nne.
Msimu wake wa kwanza 2021/22 Yanga ilifungwa mabao manane, ilhali msimu uliofuata 2022/23 ilifungwa mabao 18, msimu wa 2023/24 iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 wakati msimu huu akiwa na mechi nne mkononi Yanga imeruhusu mabao 10. kwenye misimu hiyo Diarra hajakaa mwenyewe langoni alikuwa anapata muda wa kupumzika kati ya mabao hayo yeye karuhusu 34.

60
Ni idadi ya mechi ambazo hakuruhusu bao ‘clean sheet’ alizonazo hadi sasa ukiwa ni msimu wake wa nne Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Yanga.
Diarra msimu wa kwanza 2021/22 alikuwa na clean sheet 15 na kuibuka kipa bora wa msimu akiondoa ufalme wa Aishi Manula aliyekuwa ananyanyua tuzo akiwa Azam hata alipotua Simba, aliendelea na rekodi hiyo nzuri msimu uliofuata akinyakua tuzo baada ya kuwa na clean sheets 17.
Msimu wa 2023/24 haukuwa mzuri kwake baada ya tuzo hiyo kuchukuliwa na Ley Matampi wa Coastal Union ambaye alifanikiwa kuwa kipa bora baada ya kuwa na clean sheets 15 akimuacha Diarra ambaye alikuwa nazo 14.
Kipa huyo namba moja wa Yanga msimu huu amefikia rekodi ya msimu uliopita kwani kwenye mechi 26 zilizochezwa na timu yake ana clean sheets 14 akiwa amebakiwa na mechi nne mkononi.

UBORA MISIMU MINNE
Tangu atue Yanga, Diarra ameiwezesha kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni misimu mitatu mfululizo na timu yake ipo kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji la ligi.
Pia ameisaida kubeba taji la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili mfululizo na ana tuzo kibao binafsi - kama ya kipa bora alizopata mara mbili misimu miwili mfululizo huku msimu wa tatu akizidiwa na Matampi
Kwa upande wa michuano ya kimataifa ameifikisha Yanga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika wakivaa medali za CAF na wameishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo na kuchaguliwa kwenye kikosi cha michuano hiyo walipotinga hatua hiyo pamoja na kutajwa kuwa kipa bora.
SOKA LA KISASA
Katika soka la kisasa, makocha wengi wanapenda kutumia makipa ambao wanaweza kutengeneza mashambulizi na hii ndio sifa inayombeba Diarra kwani ni mzuri kuanzisha mashambulizi akitumia mguu wake au mikono kurusha mipira.
Diarra ni kipa anayeendana na mabadiliko ya uchezaji wa soka la kisasa kwani ana sifa kubwa inayomfanya aendelee kuwaweka nje makipa wazawa ambao wanacheza nafasi moja ambao ni Abuutwalib Mshery na Khomeini Abubakar.