JKU yaanza kunoga Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- JKU iliyocheza mechi tatu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), imekusanya pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kupata sare moja, haijapoteza huku ikifunga mabao manane na kuruhusu matatu. Timu hiyo ndiyo yenye mabao mengi hadi sasa katika ligi hiyo.
KOCHA MKUU wa JKU, AbdulSaleh Mohammed amesema timu hiyo imeanza kuwa bora baada ya kuifunga Wembe mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja na amefurahi kuvuna pointi tatu za mchezo huo.
JKU iliyocheza mechi tatu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), imekusanya pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kupata sare moja, haijapoteza huku ikifunga mabao manane na kuruhusu matatu. Timu hiyo ndiyo yenye mabao mengi hadi sasa katika ligi hiyo.
Kocha huyo amesema licha ya kuhitaji kushinda mabao mengi zaidi ya hayo, lakini walitambua mechi hiyo haitakuwa rahisi ndiyo maana wawalijipanga mapema kukabiliana na hali yoyote.
"Tulitambua wazi mechi haitakuwa rahisi kwetu, hivyo tulijua watakuja wakiwa wamejipanga na mechi itakuwa ngumu ndiyo sababu ya kuhitaji kufunga mabao mengi," amesema.
Amesema wapinzani wao walitumia mbinu ya kukaa nyuma sana kuanzia katikati ya uwanja, hali iliyowalazimu kutumia maeneo ya pembeni kutengeneza mashambulizi.
Amesema wachezaji wake walijaribu kupiga pasi za kupenya lakini wapinzani walikuwa makini na kubana nafasi ambazo zilikuwa hatari zaidi upande wao.
Kocha huyo amebainisha ugumu zaidi waliupata kutokana na kumkosa mchezaji mzuri wa kumalizia nafasi walizotengeneza, huku akisema hilo ndiyo kosa ambalo wameliona na watalirekebisha kwani mechi zinazofuata hawataki kuona wanapitia hali ngumu.