Kabaddi Tanzania yaamkia kwa Nigeria
Muktasari:
- Mbali na ushindi, timu hiyo imetoa mlinzi bora katika mchezo huo ambaye ni Hafidh Ali Hamad na Juma Hamza Sultan akiibuka mshambuliaji, huku wakijinyakulia zawadi ya Rupia 10,000 za India (Sh277,513).
TIMU ya Taifa ya Tanzania kwa mchezo wa Kabaddi, baada ya kuanza mashindano ya Jumuiya ya Madola kwa kichapo, imeshinda pointi 66-17 dhidi ya Nigeria katika mechi ya pili ya mashindano hayo yanayoendelea nchini India.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Msaidizi wa timu hiyo, Abass Khamis Suleiman amesema ushindi huo umekuja baada kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza walipopoteza kwa pointi 48-21 dhidi ya SRI Lanka.
Kocha huyo, amesema walihitaji kupata ushindi katika mchezo wa pili, ndio sababu ya kupambana na kuongeza juhudi ya kufanya vyema.
“Tumepata pointi hizo baada ya kukaa chini na wachezaji kurekebisha makosa ambayo yalitugharimu mchezo wa kwanza,” amesema kocha huyo.
Alifafanua, wachezaji wamekuwa wasikivu na watulivu jambo ambalo limezaa matunda mzuri upande wao na kwa sasa timu inajipanga kwa mchezo ujao kuendelea kufanya vizuri zaidi kwani hilo ndio lengo lao.
Mbali na ushindi, timu hiyo imetoa mlinzi bora katika mchezo huo ambaye ni Hafidh Ali Hamad na Juma Hamza Sultan akiibuka mshambuliaji, huku wakijinyakulia zawadi ya Rupia 10,000 za India (Sh277,513).