Kaizer Chiefs yawinda beki Azam FC
BEKI wa kati wa Azam FC, Yeison Fuentes, ameingia kwenye rada za klabu mbili kubwa za Afrika Kusini zinazotaka huduma yake, huku moja ya timu hizo ikiwa ni Kaizer Chiefs, jambo linaloweza kuibua mjadala kuhusu mustakabali wake ndani ya kikosi cha Azam FC.
Fuentes alijiunga na Azam akitokea Leones ya Colombia, ambako alikuwa na rekodi ya mabao 11 katika mechi 45 za mashindano mbalimbali. Mwaka 2023 pekee alifunga mabao 10 katika mechi 36 za ligi ya daraja la pili nchini humo, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa mabeki waliokuwa na mchango mkubwa wa mabao.
Tangu atue Chamazi, rekodi zinaonyesha amecheza mechi 20, ikiwamo moja msimu wa 2023/24, 16 ule wa 2025/26 na tatu msimu huu wa 2026/27, bila kufunga bao. Katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita alicheza mechi tano.
Msimu huu amekuwa na nafasi chache zaidi, akicheza mechi dhidi ya Coastal Union, Mbeya City na JKT Tanzania. Katika michezo hizo amecheza dakika zote 90.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa tayari klabu hizo zimeanza kufuatilia uwezekano wa kumpata beki huyo raia wa Colombia, ambaye amekuwa sehemu ya kikosi cha Azam tangu Januari 2024.
Hata hivyo, ndani ya Azam kunaonekana kuwa na mitazamo miwili kuhusu hatma ya Fuentes. Baadhi ya mabosi wa klabu hiyo wanamtaka aendelee kubaki kutokana na uwezo wake, lakini kocha Florent Ibenge ndiye mwenye amri ya mwisho kama mchezaji huyo anatakiwa kubaki au kuondoka.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kilisema, “Kuna tofauti ya mtazamo kuhusu mchezaji huyo. Uongozi unaona bado anaweza kuisaidia timu, lakini kwa upande wa benchi la ufundi hakuna msisitizo mkubwa wa kutaka aendelee kubaki. Hilo linaweza kufanya mazungumzo ya kuondoka kwake kuwa rahisi zaidi, kwa kuwa tayari kuna ofa zipo mezani kwetu.”
Kwa upande wa Azam, timu hiyo imeanza vizuri msimu wa 2026/27 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 23 baada ya mechi 10, ikishinda saba, sare mbili na kupoteza mmoja. Imefunga mabao 19 na kuruhusu manane, ikiwa na tofauti ya mabao 11 na kinara wa Ligi ambaye ni Simba yenye pointi 30.