Kakolanya: Ilikuwa lazima nitue Jangwani

Benno Kakolanya.
Muktasari:
Prisons iliruhusu mabao 22 tu katika mechi zake 30, ikiwa nyuma ya Simba ambayo ilifungwa 17, Yanga (20) na Mtibwa Sugar iliyoruhusu mabao 21.
MAAFANDE wa Prisons-Mbeya imemaliza Ligi Kuu msimu uliopita ikishika nafasi nne katika msimamo, pia ikiwa klabu ya nne kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao langoni mwake.
Prisons iliruhusu mabao 22 tu katika mechi zake 30, ikiwa nyuma ya Simba ambayo ilifungwa 17, Yanga (20) na Mtibwa Sugar iliyoruhusu mabao 21.
Kama ulikuwa hujui ni kwamba kazi kubwa iliyoiweka Prisons katika nafasi hizo baada ya msimu wa 2014-205 kunusurika kushuka daraja ni kipa Benno Kakolanya.
Milingoti mitatu ya wajelajela hao ilikuwa ikilindwa na kipa huyo ambaye, kwa sasa ametimkia Yanga na tayari amepaa na mabingwa hao kwenda Uturuki kuweka kambi ikijiandaa na mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga itaanza kibarua chake cha Kundi A na Mo Bejaia ya Algeria mwishoni mwa wiki hii kabla ya kuisubiri TP Mazembe jijini Dar es Salaam na baadaye kuifuata Medeama ya Ghana katika mechi ya duru la kwanza la kundi hilo.
Mwanaspoti limefanya mazungumzo na nyota huyo aliyeibuliwa na kukuzwa na kituo cha soka cha Mbaspo Academy cha jijini Mbeya baada ya kutua Yanga ikiwa ni siku chache tangu ahusishwe na mabingwa wa zamani nchini, Simba.
Simba ilikuwa ikimsaka kipa huyo kwa udi na uvumba ili kutua Msimbazi, lakini akaipiga chenga ya mwili na kutua Jangwani, lakini mwenyewe amefichua sababu za kuwatema Wekundu wa Msimbazi na kutua Yanga.
SIMBA WENYEWE TU
Kakolanya anasema ni Simba wenyewe wamejichanganya wakati wakimfukuzia.
“Simba walianza kunifuata, lakini wakawa wanaremba sana, Yanga walishtukia dili hilo na kuamua kunifuata kwa kuweka mkwanja wa maana. Wala sifichi kipaumbele kilikuwa Simba kwa kuwa walionyesha nia ya dhati, lakini kilichowaangusha ni dau tu la kunivuta Msimbazi.”
Kakolanya anasema kuwa dau alilolitaka, viongozi wa Simba wakaona kubwa wakati tayari Yanga walishamchombeza na kuafikia dau lake, hivyo kwa yeyote anayejitambua ilikuwa lazima atue Jangwani.
“Ilikuwa lazima nitue Yanga kwa sababu kile nilichokuwa nakitaka walikitimiza na hawakuwa na blahblah,” anasema Kakolanya, aliyesoma Shule ya Sekondari Samora na kuongeza; “Yanga walitimiza mahitaji yangu na ndiyo nilishawishika kwa kuwa soka ni ajira yangu.”
HATISHWI
Kama kuna jambo ambalo Kakolanya anapaswa kulifanyia kazi ni kuhakikisha anapambana kiume ili awapiku Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao wanafanya vizuri kwa sasa.
Hata hivyo, kipa huyo mpya wa Yanga anasema uwepo kwa Barthez na Dida kwake ni changamoto ya kuonyesha uwezo wake na kumshawishi mwalimu ili kumpa nafasi kikosini.
“Kweli makipa waliopo Yanga ni wazoefu zaidi yangu, lakini siwaogopi kwa sababu soka ni mchezo wa hadharani, nikipewa nafasi sitasita kuitumia ili nimshawishi Kocha Hans Pluijm, najiamini naweza na sina sababu ya kuogopa, ila niseme wazi ni makipa ninaovutiwa nao na kuwaheshimu,” anasema.
MATAWI YA JUU
Kama kuna kitu kinamfurahisha Kakolanya kwa sasa ni kujiunga na Yanga ikiwa katika mwenendo mzuri baada ya kunyakua mataji matatu ya ndani na sasa ikicheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Anasema kwa mchezaji yeyote mwenye kuwa na ndoto za mafanikio ni lazima afurahie kucheza klabu kubwa na klabu kama Yanga iliyo matawi ya juu kwa sasa nchini na Afrika Mashariki.
“Yanga iko vizuri na nafurahia kuona ushindani uliopo kwa kila mchezaji kutimiza majukumu yake. Hii itatusaidia kufika mbali zaidi,” anasema Kakolanya anayeitaja mechi ya marudiano ya msimu uliopita dhidi ya Yanga na kuisha kwa sare ya 2-2 kama pambano gumu na lisilosahulika kwake.
WAJELAJELA
Kakolanya ambaye amepanda ndege kwa mara ya kwanza kwenda Ulaya hakusita kuipa tano timu yake ya zamani Prisons kwa kumpa nafasi iliyomfanya afike alipo.
“Haikuwa kazi rahisi kuanza kucheza Prisons, lakini namshukuru Kocha Salum Mayanga, ambaye alinipa nafasi ya kuonyesha uwezo wangu,” anasema.
“Nimeondoka Prisons lakini ilikuwa ni sehemu muhimu kwangu na ninawatakia kheri, nikiamini kile tulichokifanya msimu ulioisha kitaendelezwa msimu ujao hata kama sitakuwa pamoja nao, naamini wanaweza sana,” anasema.
Kokolanya anadhani Prisons haipaswi kupanguliwa kwa kikosi kilichopo, huku akimfagilia Kocha Mayanja kuwa ni bonge la kocha anayejua kuishi na wachezaji na kuwatia ndimu katika kusaka mafanikio.
TAIFA STARS
Kakolanya ni miongoni mwa wachezaji wapya walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichocheza na Misri katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2017.
Kitu hicho kwake kimempa faraja kubwa hata kama hakucheza, lakini anaamini ni mwanzo wa safari yake kimafanikio katika kulitumikia taifa na anasema kila mchezaji ana ndoto ya kuitumikia timu ya taifa lake. Kipa huyo anasema kazi iliyo mbele yake ni kuhakikisha anacheza mara kwa mara hatua itakayompatia fursa ya kudumu na timu ya taifa.
“Nilipoitwa kuitumikia Taifa Stars nilifurahi sana hasa kwa kutimiza lengo hili. Kikubwa ni kuhakikisha nafanya vizuri ili mwalimu aendelee kunipa nafasi.”
PONDAMALI AMPA TANO
Kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’ amekubali usajili wa nyota huyo na kusema;
“Kakolanya ni kipa nzuri kwelikweli, lakini ni lazima apitie mazoezi maalumu ya kumuwezesha kufahamu jinsi ya kufanya mahesabu akiwa langoni na hicho kitakuwa kipimo kikubwa kwake.”
Anasema anaamini kwa umri na kipaji alichonacho kitamfikisha mbali, ila ni vema kupenda kujifunza na kujituma mazoezi na hata akipewa nafasi uwanjani asiichezee kwa sababu Yanga ina makipa bora na ni timu yenye ushindani mkubwa kwa sasa.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz