Kikosi kizima kimesepa mwanangu

Muktasari:
Kipindi cha mapumziko ya ligi hiyo, klabu zilikuwa bize kujiimarisha kupitia dirisha dogo la usajili lililofungwa Disemba 15, huku baadhi zikiwatema nyota wake wa kigeni bila kutarajiwa.
LIGI Kuu Bara imeingia ngwe ya pili ambapo mwishoni mwa wiki michezo ya raundi ya 16 ilipigwa kwenye viwanja tofauti. Hii ni hatua ya lala salama na klabu itakayozubaa kidogo tu, lazima ile kwake kwani, ndio mechi zinazoamua ubingwa na klabu tatu za kushuka daraja ili kupisha tatu zitakazopanda Ligi Kuu msimu wa 2017-2018.
Kipindi cha mapumziko ya ligi hiyo, klabu zilikuwa bize kujiimarisha kupitia dirisha dogo la usajili lililofungwa Disemba 15, huku baadhi zikiwatema nyota wake wa kigeni bila kutarajiwa. Katika makala haya tutaona baadhi ya nyota wa kigeni walioondoka na utamu wao ambao wanaweza hata kuunda kikosi kizima na kushiriki pambano lolote na kufanya kweli.
Vincent Angban- Simba
Simba ilimsajili misimu miwili iliyopita akitokea Azam iliyokuwa ikimfanyia majaribio, lakini ikamtolea nje na ndipo Msimbazi ikamdaka fasta. Tangu alipotua Simba ikiwa chini ya Kocha Dylan Kerr mpaka alipoipokea timu Jackson Mayanja na sasa Joseph Omog, kipa huyo alikuwa ndiye chaguo la kwanza huku akionyesha kiwango cha juu. Aliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya mchezaji bora wa kigeni sambamba na kina Donald Ngoma na Thabani Kamusoko. Tuzo hiyo ilienda kwa Kamusoko, lakini Angban alionyesha ni namna gani aliibeba Simba na hata msimu huu katika nusu ya kwanza alifanya kazi kubwa akiisaidia kumaliza kileleni mwa msimamo akiruhusu mabao sita tu katika mechi 15. Vipigo kutoka kwa African Lyon na Prisons-Mbeya vilikuwa majanga kwake, kwani ndio chanzo cha kutimuliwa kikosini na kuletwa Mghana Daniel Agyei.
Joseph Owino- Stand UTD
Beki na nahodha wa zamani wa Simba aliyewahi kukipiga Azam, msimu huu alikuwa na Stand United ambayo ameshindwana naye kimasilahi na kutimkia zake Umangani kukiwa na taarifa ya kwenda Fanja FC.
Uongozi wa Fanja uliamua kuachana na Owino aliyelazimika kurejea kwenye kikosi chake ambacho kilishindwa kumlipa pesa zake za usajili Sh10 milioni. Owino alisaini mkataba wa mwaka mmoja Stand akitokea SC Villa na kucheza mechi kadhaa za ligi hiyo kwa nusu ya kwanza.
Mganda huyo anayemudu beki wa kati na pembeni ameondoka Stand, akiwa bado anahitajika kutokana na uzoefu na umahiri wake uwanjani.
Mbuyu Twite- Yanga
Usajili wake nchini ulikuwa na sintofahamu kwani, Simba iliamini imeshamnasa kabla ya Yanga kuwazidi kete na kumbeba kiraka huyo kutoka FC Lupopo. Tangu Twite alipotua Yanga amekuwa mchezaji muhimu kikosini kwa ubora wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja, lakini pia anasifika kwa umahiri wa kurusha mipira hatari kama umepigwa na mguu vile.
Beki huyo ametemwa na Yanga ili kumpisha Justin Zulu kutoka Zambia, lakini baadhi ya mashabiki hawajaridhika kabisa kutokana na ubora wake. Twite ameondoka na utamu wake kama ambavyo Yanga ilivyomtema Salum Telela mwanzoni mwa msimu huu ambaye kwa sasa anakipiga pale Ndanda FC.
JeanBaptiste Migiraneza- Azam
Licha kufanya vizuri katika timu hiyo tangu alipotua na kuisaidia kuipa Azam taji la Kombe la Kagame mwaka jana kwa kuilaza Gor Mahia ya Kenya, mabosi wa Azam wamemfungia vioo kabisa.
Migi ni moja ya mchezaji bora wa kigeni na alikuwa akitumika katika nafasi tofauti kiungo mkabaji, mshambuliaji na beki wa kati, lakini hakuweza kufua dafu mbele ya Mhispania Hernandez Rodriguez.
Licha ya uwezo huo aliouonyesha tangu alipotua Azam, Hernandez ameona amteme kwani hajaridhishwa na uwezo wake uwanjani hivyo, anakwenda zake Vietnam. Kuondoka kwake kumezua maswali kwa mashabiki wa Azam, kutokana na ukweli Migi alikuwa na mchango mkubwa na hakustahili kutemwa wakati akiwa bado na mkataba.
Pascal Wawa- Azam
Utasema nini juu ya beki huyo wa kati katili na asiyependa mzaha uwanjani?
Pascal Wawa alisajiliwa na Azam akitokea El Marreikh ya Sudan mwaka 2014, chini ya Kocha Joseph Omog anayekinoa kikosi cha Simba kwa sasa, ujio wake uliifanya Azam kuwa na ukuta wa chuma. Alikuwa na mchango mkubwa wakati Azam ikitwaa taji la Kagame Agosti 2, mwaka jana lakini msimu huu ulipoanza alikuwa akisumbuliwa na majeraha hata alipopona hakupewa nafasi na kuamua kurudi zake Sudan katika klabu yake ya zamani.
Kuondoka kwake kumewashtua mashabiki wa Azam ambao, wameishuhudia timu yao msimu huu ikiwa na beki nyanya kabisa.
Kipre Balou- Azam
Alisajiwa wakati mmoja na pacha wake Kipre Tcheche baada ya kuonekana katika mashindano ya Chalenji 2010 yalifanyika hapa nchini. Azam ikawafungia kazi na kuwasajili kwa pamoja mwaka 2011. Licha ya kwamba hakupata mafanikio makubwa kama pacha wake, labda kwa nafasi aliyokuwa akicheza kama kiungo mkabaji, lakini Balou ameisaidia Azam kwa soka lake la nguvu kabla ya majeraha kumpunguza kasi.
Klabu yake imemwacha kama mchezaji huru na hasa baada ya pacha wake kuamua kumtikia zake umangani mapema msimu huu na kuufanya uongozi wa Azam kupata sababu ya kutemana, japo alikuwa akihitajika sana ndani ya kikosi.
Hemed Murutabose- Mbeya
Starika huyu Mrundi Hemed Murutabose ameweka rekodi nchini, licha ya kupewa nafasi mara kwa mara ya kucheza na Kocha Kinnah Phiri, lakini hakuweza kufurukuta akishindwa kufunga bao hata moja. Ndiye mchezaji pekee anayeunda kikosi hiki cha wachezaji wa kigeni akiwa dhaifu, lakini bado yupo kwenye orodha kwani alistahili kuendelea kupewa nafasi zaidi kujifunza soka la Bongo.
Hemed alikuwa akitengeneza nafasi za mabao kwa wenzake waliofunga, japo mwenyewe hakufumania nyavu hata mara moja, ila ndivyo hivyo kaachwa, ili kuwapisha Waganda watatu waliotua kikosini hapo.
Mussa Ndusha- Simba
Kiungo huyo wa Simba alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea DR Congo alipokuwa akiichezea klabu ya FC Renaissance, lakini kuchelewa kwa ITC yake kulimkwamisha kuanza kuitumikia timu hiyo katika Ligi Kuu.
Ndusha alionesha anakitu cha zaida katika mechi ya majaribio Simba dhidi ya FC Leopards ambayo Mnyama alishinda mabao 4-0 na baadhi ya wapenzi wa timu hiyo wakasema hakuna tena tatizo sasa katikati mwa uwanja kwani, Ndusha anaweza akawa usajili sahihi kwao. Hata hivyo, baada ya ITC yake kutua nchini na mashabiki wakiamini ataanza kufanya mambo yake, hasa baada ya kupiga soka la nguvu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar na Polisi Moro timu ikiwa kambini, ametemwa. Ghafla tu viongozi wake wamemtema ili kumpisha James Kotei kutoka Ghana kuja kushika nafasi yake ambaye ameanza kumwagiwa sifa.
Kipre Tcheche- Azam
Nani hajui kazi kubwa ya Kipre Tchetche, raia wa Ivory Coast aliyoifanya Azam tangu aliposajiliwa mwaka 2011? Ndiye aliyekuwa roho ya mashambulizi ya Azam na hata wapinzani wa klabu hiyo kwa sasa wanapumua kukosekana kwake.
Ametwaa tuzo za Mfungaji Bora wakati Azam ikitawazwa mabingwa wapya wa Tanzania msimu wa 2013-2014 kabla ya kutwaa Mchezaji Bora msimu ulioofuata, huku akiifungia timu hiyo mabao muhimu katika ligi na michezo ya kimataifa. Mara baada ya msimu uliopita kumalizika alitimkia kwao kupumzika, lakini hakurudi tena badala yake akaibukia klabu ya Nahda Al-Buraimi ya Oman ambapo, huku nyuma ameichia Azam pengo kubwa kwani haina mfungaji tegemeo kama zamani, kwa vile hata nahodha John Bocco kwa sasa kachuja.
Francesco Zekumbawire- Azam
Straika mwingine wa kimataifa Mzimbabwe, Francesco Zekumbawira aliyekuwa nahodha wa Harare City, alianza kuchanganya kwenye Ligi Kuu, lakini ghafla mabosi wake wamempiga chini licha ya kuwa na mkataba.
Zekumbawire ametoswa pale Azam akiwa na mabao yake matatu, huku akiwa amebakiza mwaka mmoja na nusu wa mkataba alioingia na klabu hiyo.
Pengine kocha Hernandez pia hakuridhishwa na kasi yake uwanjani, lakini bado alionekana ni mchezaji aliyekuwa na kitu ambacho kingeisaidia Azam, hasa ikizingatiwa alikuwa mgeni kama kocha Zeben.
Ya Thomas- Azam
Winga machachari kutoka Ivory Coast, kwa muonekano wake unaweza ukasema ni sharobaro mmoja hivi kaja kuzurula mjini, lakini anapokuwa uwanjani usiombe akutane naye.
Thomas katika mechi zake amekuwa na msaada mkubwa katika kupeleka mashambulizi na kupiga krosi za hatari langoni mwa wapinzani.
Hata hivyo, ametemwa akiwa na bao lake moja ili kupisha majembe wapya kutoka Afrika Magharibi ambao, wameanza makeke yao Chamazi.