Kipagwile ana deni la dakika 270

Muktasari:
- Kipagwile amesema katika mechi tatu zilizobaki sawa na dakika 270 atapambana awezavyo kwani anatamani kutimiza lengo hilo aliyojiwekea msimu huu.
WINGA wa Dodoma Jiji, Idd Kipagwile baada ya kutikisa nyavu mara sita na kutoa asisti nne Ligi Kuu Bara msimu huu, akihusika na mabao 10 kati ya 30 yaliyofungwa na timu hiyo, amesema bado ana deni la mabao manne afikie lengo.
Kipagwile amesema katika mechi tatu zilizobaki sawa na dakika 270 atapambana awezavyo kwani anatamani kutimiza lengo hilo aliyojiwekea msimu huu.
“Kwa asilimia kubwa nimeweza kufanya kile nilichokuwa nimejipangia mwanzoni mwa msimu, malengo yalikuwa ni kufunga mabao 10, sasa nimeingia kambani mara sita lakini pia nimetengeneza nafasi nne zilizo zaa mabao.
“Naamini kwenye michezo mitatu iliyobaki kama nitapata nafasi ya kucheza naweza kujaribu kuandika rekodi kwa kutimiza malengo yangu japo haitakuwa rahisi lakini naamini katika upambanaji,” alisema mchezaji huyo.
Kipagwile ambaye anashika nafasi ya pili kwa ufungaji kikosini hapo nyuma ya kinara Paul Peter mwenye mabao manane, alisema huu ni msimu wake bora hasa kufunga hivyo anatamani kufikia lengo akitumia kila nafasi atakayoipata.
“Hakuna kinachoshindikana kwenye mpira, mipango sahihi itanifanya nifikie malengo yangu. Natambua mechi zitakuwa ngumu kutokana na mzunguko huu wa lala salama lakini nafasi moja ya dhahabu nikiipata siwezi kuipoteza kirahisi,” alisema.
“Mbali na kujipambania, pia nitahakikisha nasimama kuhakikisha Dodoma Jiji inasonga mbele na sio kuteremka kwenye msimamo, kwa sasa tupo nafasi ya sita, tuna uwezo wa kupaa nafasi moja kutokana na pointi tutakazokusanya kwenye mechi hizo tatu.” Dodoma Jiji ipo nafasi ya sita baada ya kucheza mechi 27, ikishinda tisa, sare saba na vipigo 10, ikikusanya pointi 34. Msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara ilimaliza katika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 30.