Maajabu ya Ahoua CAF, akifunga tu kuna jambo

Muktasari:
- Ahoua mwenye mabao matatu sawa na Kibu Denis katika michuano hiyo wakiwa vinara wa utupiaji kikosini hapo, maajabu yake ni kwamba akifunga Simba haipotezi mchezo na inashinda 1-0.
MFUNGAJI wa bao pekee katika mchezo wa kwanza ulioipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya Stellenbosch, Jean Charles Ahoua, ana maajabu yake kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Ahoua mwenye mabao matatu sawa na Kibu Denis katika michuano hiyo wakiwa vinara wa utupiaji kikosini hapo, maajabu yake ni kwamba akifunga Simba haipotezi mchezo na inashinda 1-0.
Nyota huyo raia wa Ivory Coast, katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu alianza kufunga katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya Bravos do Maquis, Simba ikashinda 1-0. Mchezo huo ulifanyika Novemba 27, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bao la pili alifunga Januari 5, 2025 dhidi ya CS Sfaxien nchini Tunisia ambapo Simba ilishinda 1-0.
Ahoua akafunga bao la tatu katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza nyumbani dhidi ya Stellenbosch, Simba ikishinda 1-0. Ilikuwa Aprili 20, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Mabao yote hayo, ameyafunga kipindi cha kwanza.
Mbali na kimataifa, pia Ahoua ndiye kinara wa mabao Simba katika Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga 12.
Katika mabao hayo 12 aliyofunga Ahoua kwenye ligi, ni mechi moja pekee dhidi ya Kagera Sugar ndiyo kikosi chake hakijaondoka na clean sheet huku zingine zote alizofunga, dakika tisini zilimalizika bila Simba kuruhusu bao.
Mechi za ligi alizofunga Ahoua ni dhidi ya Fountain Gate (4-0, alifunga moja), Dodoma Jiji (0-1, alifunga bao pekee), Namungo (3-0 alifunga moja), KMC (4-0, alifunga mawili), Kagera Sugar (2-5, alifunga moja), JKT Tanzania (1-0 alifunga bao pekee), Tanzania Prisons (3-0, alifunga moja), Namungo (0-3, alifunga mawili), Dodoma (6-0, alifunga mawili).