Makonda atoa masharti mazito kwa vijana wa Serengeti boys
Muktasari:
- Akizungumza wakati wa mapokezi ya timu hiyo katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere leo mchana, Makonda alisema Serikali imeagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusimamia kwa karibu hatua zozote za usajili zitakazowahusisha vijana hao ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kucheza.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema tayari baadhi ya klabu zimeanza kuvutiwa na nyota wa Serengeti Boys baada ya kiwango walichoonyesha kwenye fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 AFCON U-17, lakini akaonya vipaji hivyo visiharibiwe kwa kuwekwa benchi.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya timu hiyo katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere leo mchana, Makonda alisema Serikali imeagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusimamia kwa karibu hatua zozote za usajili zitakazowahusisha vijana hao ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kucheza.
Makonda alisema tayari kuna timu zimeonyesha nia ya kuwasajili baadhi ya wachezaji waliovutia kwenye mashindano hayo yaliyomalizika nchini Morocco, lakini akasisitiza kuwa masharti ya maendeleo yao lazima yaheshimiwe ili vipaji visipotee mapema.
“Vipo vilabu vimeona uwezo wao, hivyo tumewagiza BMT wawasaidie kwa masharti maalumu. Wakisajiliwa lazima wapate nafasi ya kucheza na si kuwekwa benchi muda wote,” alisema Makonda huku akipigiwa makofi na mashabiki waliojitokeza kuwapokea vijana hao.
Waziri huyo alisema hatua iliyofikiwa na Serengeti Boys ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za TFF katika kuanzisha na kuendeleza akademi za vijana nchini.
Alisema mafanikio hayo ni historia mpya kwa soka la Tanzania, hasa baada ya timu hiyo kufika fainali ya AFCON U-17 na kufuzu Kombe la Dunia la vijana, jambo ambalo limeongeza matumaini ya kuwa na kizazi bora cha wachezaji wa baadaye.
Makonda pia alimpongeza kocha mkuu wa Serengeti Boys, Elieneza Nsanganzelu kwa kazi kubwa aliyofanya dhidi ya timu zenye makocha wenye wasifu mkubwa barani Afrika, akisema uwezo wa makocha wazawa umeanza kuonekana kwenye mashindano ya kimataifa.
“Matarajio ya Watanzania yalikuwa kuona tunaleta kombe, lakini tumepoteza kwa penalti ambazo hazina mwenyewe. Hata mastaa wakubwa duniani wanakosa penalti, hivyo vijana hawa wanastahili pongezi kwa walichokifanya,” alisema.
Aidha, alifichua kuwa Serikali kwa kushirikiana na TFF imepanga kuwapeleka baadhi ya vijana hao katika nchi za Ulaya ikiwamo Ufaransa na Hispania kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi na kuendelea kukomaza vipaji vyao kabla ya mashindano makubwa yajayo.
Kabla ya kuwasili Serengeti Boys, mazingira ya Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere yalitawaliwa na shamrashamra kubwa huku vikundi vya burudani, wapiga ngoma na matarumbeta vikitoa burudani maalumu.
Wimbo wa 'Afande' wa Dogo Paten aliyomshirikisha Zuchu ulitawala eneo hilo, mashabiki wakishangilia huku hata baadhi ya wageni kutoka nje ya nchi wakivutiwa na hamasa iliyokuwa imejaa wakati wa kuwapokea mashujaa hao wa Tanzania.