Marefa Tanzania watoswa Afcon 2025

Muktasari:
- Fainali za Mataifa Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17) 2025 zitafanyika Morocco kuanzia Machi 30 hadi Aprili 19, 2025.
Tanzania haitokuwa na refa katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji walio chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17) 2025 zitakazofanyika Morocco baadaye mwezi huu.
Katika orodha ya mwisho ya marefa 45 walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha fainali hizo mwaka huu, hakuna jina la refa wa kati wala msaidizi kutoka Tanzania.
Kama ilivyo kwa Tanzania, Kenya nao hawajabahatika kuwakilishwa na refa kwenye fainali hizo huku Rwanda, Sudan, Uganda na Djibouti zikipata fursa hiyo muhimu kwa upande wa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Orodha ina marefa 17 wa kati, 18 wa pembeni na 10 ambao wataongoza teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR).
Marefa 17 wa kati ni Vincent Kabore (Burkina Faso), Patience Rulisa na Alinę Umutoni (Rwanda), Barbosa Lenine (Cape Verde), Fleury Moukagny (Gabon), Asamoah Collins (Ghana), Josiano Elivas (Madagascar), Abdulwahid Huraywida (Libya), Hamza Elfariq (Morocco), Sadou Ali (Niger), Keren Yocette (Shelisheli), Lucky Kasalirwe (Uganda), Brighton Chimene (Zimbabwe), Karboubi Bouchra (Morocco), Amedome Vincentia (Togo) na Ghada Mehat (Algeria).
Marefa wasaidizi 18 ni Alao Salim (Benin), Sawadogo Levy (Burkina Faso), Dirir Robleh (Djibouti), Mwanya Mbilizi (DR Congo), Birama Kone (Mali), Abdessamad Abertoune (Morocco), Ousmana Aboubakar (Niger), Didier Ishimwe na Alice Umutesi (Rwanda) na Luis Ferreira (Sao Tome).
Wengine ni Cledwin Baloyi (Afrika Kusini), Jermoumi Fathia (Morocco), Nancy Kasitu (Zambia), Nafissatou Yekini (Benin), Asma Feriel (Algeria), Hannah Moses (Liberia), Tabara Mbodj (Senegal) na Mireille Kanjinga (DR Congo).
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutokuwa na refa kwenye fainali za Afcon U17 baada ya kufanikiwa kupeleka marefa katika awamu tatu mfululizo zilizopita za mashindano hayo yanayofanyika kila baada ya miaka miwili.
Awamu iliyopita, refa aliyeiwakilisha Tanzania alikuwa ni Ahmed Arajiga na kabla ya ya hapo mwaka 2019, refa wa kati Jonesia Rukyaa na msaidizi, Mohamed Mkono walichezesha fainali hizo.
Katika fainali za mwaka 2017 za Afcon U17, Tanzania iliwakilishwa na refa msaidizi Frank Komba.