Mechi ya Stars, Morocco yafutwa kisa mastaa
Muktasari:
- Mechi ya kirafiki baina ya Taifa Stars na Morocco ilipangwa ichezwe kesho Jumatatu, Oktoba 5, 2026 jijini Tangier, Morocco.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kufutwa kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Morocco.
Mechi hiyo ilipangwa ichezwe Jumatatu, Oktoba 5, 2026 jijini Tangier, Morocco.
Hata hivyo TFF imesema kwamba mchezo huo hautokuwepo kutokana na Taifa Stars kutokuwa na namba ya kutosha ya wachezaji.
“Uamuzi wa kufuta mchezo huo umetokana na ripoti ya madaktari wa Taifa Stars wakati wakielezea hali ya wachezaji waliopo kambini kwenye mji wa Tangier.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wachezaji watano (5) wamepata majeraha ambayo yatawafanya washindwe kucheza mchezo huo dhidi ya Morocco.
“Baada ya kushauriana na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi tumekubaliana kuufuta mchezo huo.
“Taifa Stars ilisafiri na wachezaji 23 pekee kwa mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 dhidi ya Madagascar uliochezwa Meknès, Morocco Septemba 29, 2026 na baada ya mchezo huo walitakiwa kucheza mchezo huo wa kalenda ya FIFA. Tayari wachezaji na benchi la Ufundi wamepewa taarifa ya kufutwa mchezo huo,” imesema taarifa ya TFF.
Kabla ya wachezaji hao watano kuumia, Taifa Stars ilishaondokewa na wachezaji saba ambao wapo njiani kurejea nchini kwa ajili ya kuungana na klabu zao.
Wachezaji hao ni Mudathir Yahya, Selemani Mwalimu, Ibrahim Abdullah na Mohamed Hussein wa Yanga, Nathaniel Chilambo na Morice Abraham wa Simba na Metacha Mnata wa Singida Black Stars.