Minziro aichorea ramani kali Simba
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Bukombe uliopo Geita, Fountain ilitangulia kupata bao lililofungwa na Mnigeria Chukwunonye Obasi kwa penalti dakika ya 42.
KOCHA Mkuu wa Fountain Gate, Fredy Felix ‘Minziro’, amesema sare iliyoipata timu hiyo ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Geita Gold katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa juzi, imeongeza motisha wakati kikosi hicho kikijiandaa kucheza na Simba.
Mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Bukombe uliopo Geita, Fountain ilitangulia kupata bao lililofungwa na Mnigeria Chukwunonye Obasi kwa penalti dakika ya 42.
Wakati Fountain Gate ikiamini mechi hiyo imeisha, wenyeji walijibu mapigo na kutengeneza mashambulizi kipindi cha pili yaliyoleta matunda, baada ya kusawazisha bao lililofungwa na mshambuliaji Yusuph Mhilu dakika ya 63.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Minziro amesema licha ya maandalizi ya muda mfupi, ila wamerudi kufanyia kazi namna ya kucheza na Simba, huku akiamini wapinzani wao wameimarika kutokana na mwenendo wao, japo wasitegemea kukutana na wepesi.
“Tuna siku mbili za maandalizi yetu hadi kufikia mechi ya Simba, mwenendo wetu sio mzuri kwa sababu ya aina ya matokeo tunayoendelea kuyapata, ingawa sare ugenini dhidi ya Geita Gold kuna mabadiliko makubwa ya kiuchezaji,” amesema Minziro.
Minziro amesema kazi kubwa anayopambana nayo ni kuendelea kutengeneza safu bora ya ushambuliaji, japo kwa mechi za hivi karibuni kumekuwa na maendeleo mazuri ya utengenezaji wa nafasi, huku kilichobakia ni namna nzuri ya kuweza kuzitumia.
Fountain Gate FC, imecheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi, tangu mara ya mwisho kwa kikosi hicho kilipoifunga Mashujaa FC bao 1-0, Agosti 18, 2026.
Tangu iliposhinda bao 1-0, Agosti 18, 2026, Fountain Gate imecheza mechi zake saba bila ya ushindi, ambapo kati ya hizo imechapwa nne na kutoka sare tatu, ingawa, kiujumla imeshacheza tisa, ikishinda mmoja tu, sare tatu na kupoteza mitano.
Mwenenddo huo wa Fountain Gate, umeifanya timu hiyo kuburuza mkiani mwa msimamo wa nafasi ya 16 na pointi sita, huku pia ikiwa na safu butu ya ushambuliaji na ya kujilinda, baada ya kikosi hicho kufunga mabao matano na kuruhusu mengine 13.