ALIYEKUWA mshambuliaji wa Singida Black Stars, Mossi Ndumumwe raia wa Burundi ambaye kwa sasa anaichezea MC Algiers ya Algeria aliyojiunga nayo Agosti 7, 2026, amesema kwa muda aliyocheza Ligi Kuu Bara, kaviona vipaji vikubwa vya wazawa ambao wakiamua kutoka nje, watafanya makubwa.
Ndumumwe ambaye msimu uliopita alikuwa kinara wa mabao akifunga mara 17 Ligi Kuu Bara aliwataja baadhi yao kuwa ni Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC, Mudathir Yahya, Seleman Mwalimu (Yanga) na Ahmed Bakari Pipino (Singida Black Stars) kuwa wanaweza kwenda nje ya nchi na kufanya mambo makubwa kwa kuwa wana vipaji vikubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti alisema wachezaji hao wanaendeleza viwango vyao na ufundi mwingi uwanjani, jambo analoona wakipata fursa ya kucheza nje majina yao yatakuwa makubwa zaidi.
Data za wachezaji hao aliyowataja msimu uliopita Fei Toto alimaliza na mabao 15, asisti 9 kwa sasa ana bao moja, Mwalimu akiwa Simba alikuwa na mabao tisa, Mudathir mabao tisa asisti tatu kwa sasa ana mabao mawili kwa msimu huu Pipino ana bao moja.
"Kuna wachezaji wengi nimewaona huko Tanzania mbali na hao niliowataja, wakiamua kuthubutu kutoka nje kama sisi ambavyo tumekuja kucheza nchini kwao na tukaondoka basi wataongeza thamani ya CV zao." alisema Ndumumwe na kuongeza;
"Kuna wakati nilikuwa najiuliza changamoto yao ni kitu gani ni kukosa fursa au wameridhika kucheza nchini kwao, maisha ya soka ni ya muda mfupi, wakiona kuna sehemu wanaweza wakapata pesa nyingi wanapaswa kuwa na maamuzi magumu, ni ukweli usiopingika kupata ugumu wa kucheza nje na nyumbani lakini kazi yetu haina makazi maalumu."
Mbali na hilo alisema kinachowasaidia wachezaji wa Tanzania wanabebwa na vyombo vya habari, vinavyozungumza taarifa zao, tofauti na nchi nyingine akitolea mfano kwao Burundi kwamba inakuwa ni nadra sana kuona vyombo vya habari vikizungumza kuhusu wachezaji wa ndani.
"Kuna wakati niliona mtazamo wa wachezaji dhidi ya waandishi sijui inakuwa ni changamoto gani, hawaoni vyombo vya habari vina nguvu ya kuwavusha hatua moja mbele, lakini kwangu naamini kuwa ni daraja muhimu sana." alisema.