Okello akabidhiwa medali ya ubingwa Vipers
Muktasari:
- Wiki chache zilizopita, Mwanaspoti liliripoti kuwa Okello alikuwa miongoni mwa wachezaji watakaopewa medali za ubingwa huo kutokana na mchango wake katika kampeni ya Vipers ya msimu wa 2025/26.
AKIWA kambini na timu ya taifa ya Uganda (Uganda Cranes), kiungo mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello amekabidhiwa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Uganda baada ya kuhusika katika mafanikio ya Vipers kabla ya kuhamia Jangwani.
Wiki chache zilizopita, Mwanaspoti liliripoti kuwa Okello alikuwa miongoni mwa wachezaji watakaopewa medali za ubingwa huo kutokana na mchango wake katika kampeni ya Vipers ya msimu wa 2025/26.
Kabla ya kuondoka klabuni hapo wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi Januari, Okello aliichezea Vipers katika mechi kadhaa za ligi na kufunga mabao matatu yaliyoisaidia timu hiyo kujijengea msingi wa kutwaa taji hilo.
Baada ya kuondoka Uganda, Okello alisajiliwa na Yanga na haraka akawa mmoja wa nyota muhimu wa kikosi hicho. Tangu atue Ligi Kuu Bara, kiungo huyo ameonyesha kiwango bora kwa kufunga mabao 11 na kutoa asisti saba, rekodi inayomfanya kuwa mmoja wa wachezaji hatari zaidi kwa sasa.
Medali hiyo ilikabidhiwa kwa nyota huyo kabla ya Uganda kuondoka kuelekea Marrakech, Morocco ambako itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa katika kalenda ya FIFA. Uganda itaanza kwa kuvaana na Tanzania Juni 5, 2026 kabla ya kukutana na Madagascar katika mchezo mwingine.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa medali hiyo, Okello hakuficha furaha yake huku akiwashukuru viongozi wa Vipers kwa kutambua mchango wake katika safari ya ubingwa wa timu hiyo.
"Ninawashukuru sana familia yangu ya kwanza, Vipers. Nimefurahi na nina shukrani kubwa kupata medali hii. Nawashukuru rais wa klabu, benchi la ufundi na makocha wote kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu mwanzo wa msimu hadi kufikia mafanikio haya," alisema Okello.
Nyota huyo aliongeza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja za kila aliyekuwa sehemu ya kikosi hicho na kwamba anajivunia kuwa sehemu ya historia ya ubingwa huo licha ya kuondoka katikati ya msimu.
"Najua haikuwa safari rahisi lakini mlifanya kila mmoja wetu ajisikie fahari. Kama mchezaji nina furaha kuona juhudi zetu zikitambuliwa na mwisho wa siku tumefanikiwa kuipa furaha familia ya Vipers," alisema.
Okello pia alimpongeza rais wa klabu hiyo, Dr. Lawrence Mulindwa kwa kuendelea kutoa mazingira bora kwa wachezaji na benchi la ufundi jambo ambalo limekuwa chachu ya mafanikio ya Vipers katika misimu ya karibuni.
"Ninatoa shukrani maalum kwa rais wa klabu kwa namna ambavyo amekuwa akiwapa wachezaji sapoti na kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kufanya kazi yao uwanjani. Hayo ndiyo mambo yanayosaidia timu kufikia malengo makubwa," amesema kiungo huyo.
Kupokea medali hiyo kunamaanisha Okello ataingia kwenye rekodi za msimu huu akiwa miongoni mwa wachezaji wachache waliobeba mafanikio katika ligi mbili tofauti za Afrika Mashariki, akichangia ubingwa wa Vipers nchini Uganda huku pia akiwa sehemu muhimu ya mbio za Yanga katika mashindano ya ndani Tanzania.
Kwa sasa nyota huyo anakabiliwa na majukumu ya timu ya taifa ya Uganda ambayo inatumia mechi za kirafiki dhidi ya Tanzania na Madagascar kujiandaa kwa mashindano na ratiba za kimataifa zijazo.
Baada ya kumaliza majukumu yake katika timu ya taifa ya Uganda, Okello atarejea Yanga akiwa na kazi ya kuisaidia timu hiyo kutimiza lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Kiungo huyo anawania taji lake la kwanza la ligi nchini Tanzania tangu atue Jangwani mwezi Januari.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 60, ikiwazidi watani zao Simba kwa pointi mbili huku Simba ikishika nafasi ya pili. Huku zikiwa zimesalia mechi tano kabla ya pazia la msimu kufungwa.