Pamba yammezea mate Lanso
Muktasari:
- Beki huyo aliyejiunga na Singida Black Star kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu, lakini kazi imeonekana kumshinda ndani ya miezi sita pekee, hivyo kuanzisha uwezekano wa kuondoka katika timu hiyo.
WAKATI Singida Black Stars ikifanya tathmini ya kikosi chake kuelekea msimu ujao, beki wa kulia Abdallah Said Ali 'Lanso' ameanza kuingia kwenye rada za Pamba Jiji FC.
Beki huyo aliyejiunga na Singida Black Star kwa kusaini mkataba wa miaka mitatu, lakini kazi imeonekana kumshinda ndani ya miezi sita pekee, hivyo kuanzisha uwezekano wa kuondoka katika timu hiyo.
Taarifa za ndani kutoka Singida zinadai klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kufanya maboresho katika baadhi ya maeneo ya kikosi chake, huku nafasi ya Lanso ikitajwa kuwa miongoni mwa zinazofanyiwa tathmini.
Chanzo hicho kilieleza kuwa beki huyo amekuwa akipambana kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na uwepo wa Andy Koffi ambaye ameonyesha kiwango kizuri na kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Lanso ni mchezaji mzuri, lakini amekutana na ushindani wa nafasi. Uongozi unaendelea kufanya tathmini ya kikosi na uamuzi wowote utakaofanyika utazingatia mahitaji ya benchi la ufundi.
Hata hivyo, wakati Singida ikitafakari mustakabali wa beki huyo, Pamba Jiji imeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha inamnasa haraka iwapo mlango wa kuondoka utafunguliwa.
Inaelezwa viongozi wa Pamba wanaamini Lanso bado ana uwezo wa kucheza katika kiwango cha juu na kwamba changamoto yake imekuwa ushindani wa ndani ya kikosi badala ya kushuka kiwango.
“Pamba wanaamini Lanso bado ana kitu cha kutoa. Wanaona amekosa nafasi zaidi kutokana na ushindani uliopo dhidi ya Andy Koffi, lakini uwezo wake haujapungua. Ndiyo maana wanamfuatilia kwa karibu.
"Benchi la ufundi la Pamba linaona uzoefu wa Lanso unaweza kuwa msaada katika kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo ambayo inataka kuwa na kikosi chenye ushindani msimu ujao."