Pipino ampa tano Mkude
Muktasari:
- Aliifafanua kauli yake kwamba uwepo wa wachezaji wa kigeni na wazawa wenye uzoefu mkubwa katika timu hiyo, kumemjenga kuwa mshindani na kuamini msimu huu utakuwa bora kwake.
NAHODHA msaidizi wa Singida Black Stars, Ahmed Bakari Pipino amesema kwa ushindani uliopo katika timu hiyo, umeendelea kumjenga na kupanda levo za kiuchezaji, huku akimsifu kiungo wa zamani wa Simba na Yanga Jonas Mkude.
Aliifafanua kauli yake kwamba uwepo wa wachezaji wa kigeni na wazawa wenye uzoefu mkubwa katika timu hiyo, kumemjenga kuwa mshindani na kuamini msimu huu utakuwa bora kwake.
Pipino anayemiliki bao moja hadi sasa alisema:"Nimeanza vizuri, natarajia utakuwa msimu wenye manufaa ya juu, baada ya kujiunga na SBS najiona kuna utofauti kutokana na kujifunza vitu vingi kutoka kwa wachezaji mbalimbali.
Aliongeza:"SBS imeshiriki michuano mbalimbali ya kimataifa, hiyo ni fursa kwangu kuendelea kujifunza levo za kiushindani, zitakazonisaidia kutimiza ndoto za kucheza nje."
Kabla ya kiungo mkabaji Khalid Aucho kuondoka nchini baada ya kucheza Yanga na SBS,alikuwa ni mchezaji ambaye Pipino anamtazama kama mfano wa kuigwa ila kwa sasa anawataja Himid Mao wa Azam na Jonas Mkude aliyejiunga na Mashujaa.
"Mkude na Mao ukiwatazama uchezaji wao kuna kitu kikubwa kiufundi najifunza kutoka kwao, hawatumii sana nguvu bali akili, kujua ni wakati gani wanaweza wakafika kuipokonya mipira kwa wapinzani na muda gani wa kupiga pasi," alisema ambaye msimu uliyopita kabla ya kujiunga na SBS aliwahi kutakiwa na Simba, Yanga na Azam FC wakati anaitumikia KMC.