Pointi tano zampa nguvu Mgunda

Muktasari:
- Mgunda ameyasema hayo baada ya kukusanya pointi tano kupitia mechi hizo tatu za hivi karibuni akianza na sare ya 1-1 na Pamba Jiji, ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC na sare nyingine ya 2-2 mbele ya JKT Tanzania, akisema zimewapa nguvu na kuamini wataimarika zaidi kabla ya kuvaana na Yanga.
POINTI tano ilizovuna Namungo kupitia mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara, zimempa kiburi kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda aliyesema licha ya kikosi hicho kuyumba mwanzoni, bado anaamini mechi nne zilizosalia kufungia msimu zitawabeba ikiwamo mchezo dhidi ya Yanga.
Mgunda ameyasema hayo baada ya kukusanya pointi tano kupitia mechi hizo tatu za hivi karibuni akianza na sare ya 1-1 na Pamba Jiji, ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC na sare nyingine ya 2-2 mbele ya JKT Tanzania, akisema zimewapa nguvu na kuamini wataimarika zaidi kabla ya kuvaana na Yanga.
Kocha huyo wa zamani wa Coastal Union na Simba, aliliambia Mwanaspoti, anajivunia kikosi hicho kwa namna kinavyozidi kuimarika na kushindana na wengine, licha ya kuwa na makosa mengi eneo la ulinzi aliloahidi kulifanyia kazi kabla ya kurejea katika Ligi ikiwa nyumbani kuivaa Mashujaa.
‘’Huu ni msimu dume sio rahisi, kila timu ni bora hakuna mechi ambayo una uhakika wa kukusanya pointi tatu bila ya maandalizi mazuri, nafurahi wachezaji wangu sasa wanafanya vizuri licha ya makosa madogo madogo yaliyopo ili kupima ubora tutajua dhidi ya Yanga ambayo inaonekana kuwa tishio msimu huu ikishinda kila mchezo,” alisema Mgunda na kuongeza;
“Baada ya kupoteza katika Kombe la Shirikisho dhidi ya Kagera Sugar na ule mchezo wa Ligi dhidi ya Singida Black Stars nilikaa na wachezaji kujua shida ilipo sasa wanafanya kile tunachoelezana lakini bado eneo la ulinzi lina makosa.”
Mgunda alisema ugumu uliopo sasa unawafanya wajipange kwa kila hali ili kujihakikisha wanapata nafasi ya kuicheza tena ligi kwa msimu ujao, licha ya kuwa na mchezo mgumu ugenini dhidi ya Yanga anaoamini ndio utatoa taswira ya Namungo kuwa katika nafasi ipi.
“Hakuna mchezo rahisi kila kitu kinawezekana mbinu na mikakati sahihi inahitajika ili kuweza kuisaidia Namungo kuendelea kubaki msimu ujao, ugumu upo na mikakati inaendelea ili kurekebisha makosa tuliyoyafanya katika mechi zilizopita.”
Kwa sasa Namungo ipo nafasi ya 11 ikicheza mechi 26 na kuvuna pointi 28 wastani ambao ameutaja Mgunda kuwa sio mzuri kwa timu hiyo, japo anakiri ugumu wa ligi umechangia kuwa hapo walipo na kwa kilichobaki ni suala la muda ili kupanda nafasi za juu.