Ronaldo Delima amiliki timu Hispania

Muktasari:
- Gwiji huyo wa soka wa Brazil, anakamilisha taratibu za kisheria baada ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo na baada ya hapo atakuwa ndiye Rais na mtendaji wa klabu hiyo.
Madrid, Hispania. Mshambuliaji wa zamani wa Inter Milan, Barcelona na Real Madrid ya Hispania, Ronaldo Nazario de Lima, amekamilisha taratibu za kuwa mmiliki mpya wa klabu ya Real Valladolid ya Ligi Kuu Hispania.
Gwiji huyo wa soka wa Brazil, anakamilisha taratibu za kisheria baada ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo na baada ya hapo atakuwa ndiye Rais na mtendaji wa klabu hiyo.
Hatua hiyo imefurahiwa na mashabiki wa soka nchini Hispania kutokana na ukweli kwamba gwiji huyo wa Brazil mwenye miaka 42, analijua soka kwa kiwango kikubwa na alikuwa akitumiwa kutoa mchango mkubwa wa ushauri kwenye klabu ya Real Madrid.
Ronaldo, amenunua hisa zilizowekwa sokoni na Rais wa Real Valladolid, Carlos Suarez, aliyekuwa akimiliki asilimia 66 ya hisa na jana Jumatatu nguli huyo wa soka wa Brazil alikamilisha taratibu za kibenki na kulipa Euro 30 milioni.
Baada ya kukamilisha taratibu hizo za ununuzi, Ronaldo alisema atajitahidi kuipa mafanikio timu hiyo akawaomba mashabiki kuiunga mkono ili kuhakikisha itapiga hatua kisoka, akisema kwa upande wake atahakikisha hawi kikwazo kwa namna yoyote ile.
“Ninafuraha sana kwamba hatimaye nimekamilisha ndoto zangu za muda mrefu kumiliki timu, hili ni swala ambalo nimekuwa nikiliota kwa muda mrefu, ninahitaji sapoti ya mashabiki nia yangu ni kujenga timu ya ushindani,” alisema Ronaldo.
Alisema baada ya kuweka sawa baadhi ya mambo ataitangaza bodi yake na menejimenti itakayofanya kazi ya kuanza kuisuka timu hiyo kuwa ya kupigania ubingwa.
Ronaldo alisema hilo halitakuwa la muda mfupi lakini pia halitachukuwa muda mrefu sana kama mashabiki wataiunga mkono kikamilifu.
Aidha mshambuliaji huyo amewakaribisha mashabiki wa timu hiyo kutoa maoni yao kuhusu nini kifanyike ili timu hiyo ianze mwanzo mpya wa mafnikio ya kisoka na kiuchumi akisema Real Valladolid, ni timu yao na kwa pamoja wanaweza kuifikisha mbali.
Klabu ya Real Valladolid ilirejea Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ Juni mwaka huu baada ya kushukwa miaka minne iliyopita ma inadaiwa kuwa na madeni yanayofikia Euro 25 milioni.
Suarez, aliyeiongoza klabu hiyo hiyo kwa miaka 17 na alisema anafurahi kuona timu hiyo imepata muwekezaji mpya ambaye ni mwanasoka na mtu mwenye mtazamo wa kisasa kuhusiana na uongozi wa soka.
“Ingawa nilipanga kuziuza hisa zangu lakini nilikuwa nikihofia juu ya mtu atakayeinunua Real Valladolid, sikutaka kumpa mtu atakayeshindwa kuiendesha tamaa yangu ni kuona timu inaendelea na siku moja kuwa bingwa wa Hispania, alipopatikana Ronaldo sikujiuliza mara mbili nilimuuzia hisa zangu kwa moyo mweupe,” alisema Suarez.
Mfanyab iashara huyo alisema atakabidhia kila kitu kwa Ronaldo nay eye atabakia kwenye klabu kama kiongozi wa heshima na shabiki mkubwa lakini sio kama mmiliki kama ilivyokuwa zamani.
Ronaldo aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa Dunia mara mbili alicheza La Liga kwa misimu sita msimu wa 1996-97 aliichezea Barcelona na kati ya 1997 akahamia Real Madrid hadi 2003.
Meya wa mji wa Valladolid, Oscar Puente, alifurahishwa na ujio wa Ronaldo, akisema amefurahi kupita maelezo na kwamba atatoa kila aina ya msaada utakaohitajiwa na mwanasoka katika mambo ya utawala ili kuhakikisha timu hiyo inapiga hatua katika medani ya soka la Hispania.
Hii itakuwa klabu ya pili kumilikiwa na Ronaldo, awali alinunua Fort Lauderdale Strikers ya Florida, Marekani, iliyoanziwa mwaka 2006 lakini miaka miwili baadaye akaiunza kutokana menejimenti kushindwa kuisimamia kama alivyokuwa akitaka.