Sakata la Dabi: Viongozi Simba wawasili Kwa Mkapa kukutana na Waziri

Muktasari:
- Kikao hiki ni maalumu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambao uliahirishwa siku ya mechi, baada ya Simba kulalamika kuwa walizuiwa na watu waliowataja kama walinzi wa Yanga kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam sehemu ambayo mchezo huo ulitarajiwa kufanyika, Machi 8.
Viongozi wa Simba wamenza kuwasili hapa Uwanja wa Benjamin Mkapa tayari kwa zamu yao ya kufanya kikoa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Palamagamba Kabudi.
Kikao hiki ni maalumu kwa ajili ya kujadili mustakabali wa mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambao uliahirishwa siku ya mechi, baada ya Simba kulalamika kuwa walizuiwa na watu waliowataja kama walinzi wa Yanga kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam sehemu ambayo mchezo huo ulitarajiwa kufanyika, Machi 8.
Msafara wa Simba umeanza na wajumbe wa Kamati ya Utendaji CPA Issa Masoud aliyewasili uwanjani hapa saa 6:48 mchana.
Nyuma yake akafuata mjumbe mwingine Mohammed Nassoro maarufu kwa jina la Mohamed Kigoma aliyefika saa 6:54, mchana.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu aliwasili uwanjani hapo saa 7:24 mchana huku akisema amefika kusikiliza wito wa waziri ingawa hawajui ajenda ya mkutano huo itakuwa nini.
Dakika nne baadaye kundi lingine la viongozi wa wekundu hao wamewasili uwanjani hapa wakiongozwa na Salim Mhene 'Try Again' akiwa pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Dk Seif Muba na Seleman Haroub.
Kwenye msafara huo pia yumo Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba Zubeda Sakuru.