Salum Chuku ndiyo basi tena

Muktasari:
- Chuku ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti amesema hali yake inaendelea vizuri na anaendelea na matibabu kwa matumaini ya kurejea uwanjani akiwa imara zaidi, ingawa amekiri haitakuwa kwa kiwango cha juu na inahitajika uvumilivu mkubwa.
BEKI wa Tabora United, Salum Chuku atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu kuuguza majeraha ya goti aliyoyapata katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara wakati akiichezea timu hiyo dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Chuku ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti amesema hali yake inaendelea vizuri na anaendelea na matibabu kwa matumaini ya kurejea uwanjani akiwa imara zaidi, ingawa amekiri haitakuwa kwa kiwango cha juu na inahitajika uvumilivu mkubwa.
"Si rahisi kukaa nje ya uwanja muda mrefu, hata hivyo, bado nina imani na matibabu yangu na wataalamu wanaonishughulikia," alisema na kuongeza,
“Licha ya maumivu ya mwili, maumivu ya kiakili pia yalikuwa makali. Nilikumbwa na wasiwasi."
Chuku anaamini nyota wenzake wa timu hiyo watapambana kuhakikisha inamaliza nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na hadi sasa baada ya mechi 16 imefikisha pointi 25 na iko nafasi ya tano."Kama ilivyo kwa kila mchezaji ambaye ana umoja na timu yake, mimi pia ninaendelea kuwa na matumaini na wachezaji wenzangu. Hata kama sitakuwa uwanjani, nafahamu tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata matokeo mazuri," amesema Chuku na kusisitiza mafanikio ya timu hiyo yanategemea mshikamamo na juhudi za kila mchezaji.