Siku 408 za Kamungo bila bao Marekani
Muktasari:
- Tangu aanze kucheza MLS, Kamungo amekuwa na nyakati za kukumbukwa, ikiwemo bao lake la kwanza katika ligi hiyo alilofunga Aprili 15, 2023 dhidi ya Real Salt Lake. Bao hilo lilikuwa la ushindi, akifunga dakika ya 88 baada ya kuingia akitokea benchi.
LEO Oktoba 26, 2026 mshambuliaji wa Tanzania, Bernard Kamungo anayekipiga kikosi cha FC Dallas ya Marekani anafikisha siku 408 bila kufunga bao katika ligi hiyo.
Kamungo ambaye huu ni msimu wake wa nne kuitumikia timu hiyo akijiunga nayo mwaka 2023 akitokea North Texas ambako alicheza mechi nne.
Mara ya mwisho mshambuliaji huyo kufunga bao ilikuwa Septemba 13, 2025 ambapo alimaliza msimu wa 2025/26 akiweka kambani mabao mawili kwenye mechi 30, tangu hapo hajafunga akitoa asisti mbili za msimu huu.
Kamungo, aliyezaliwa Kasulu, Tanzania, Januari 1, 2002, amekuwa sehemu ya kikosi cha FC Dallas tangu kupandishwa kutoka North Texas SC mwaka 2022. Kabla ya kujiunga na kikosi cha kwanza, alifanya vizuri akiwa North Texas SC, ambako alifunga mabao 16 na kutoa asisti tano katika mechi 25 mwaka 2022.
Rekodi hiyo inaonyesha alikuwa na uwezo wa kuleta tofauti katika eneo la ushambuliaji kabla ya kuanza safari yake ya MLS.
Tangu aanze kucheza MLS, Kamungo amekuwa na nyakati za kukumbukwa, ikiwemo bao lake la kwanza katika ligi hiyo alilofunga Aprili 15, 2023 dhidi ya Real Salt Lake. Bao hilo lilikuwa la ushindi, akifunga dakika ya 88 baada ya kuingia akitokea benchi.
Tukio hilo lilikuwa mwanzo mzuri wa safari yake katika ligi hiyo, na limeendelea kuwa sehemu muhimu ya historia yake akiwa FC Dallas.