Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yabaki Kigali, Barker aendelea na kazi ya kujenga kikosi

Muktasari:

  • Simba ilimaliza ushiriki wake kwenye mashindano hayo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa mwisho wa Kundi B uliochezwa Uwanja wa Amahoro lakini pointi tano ilizokusanya hazikutosha kuifikisha hatua inayofuata.

KIGALI: LICHA ya safari ya Simba SC kwenye Kombe la CECAFA Kagame 2026 kufikia tamati  baada ya kushindwa kufuzu hatua ya nusu fainali, kikosi hicho kitasalia Kigali, Rwanda kwa ajili ya kuendeleza maandalizi ya msimu ujao wa 2026/27.

Simba ilimaliza ushiriki wake kwenye mashindano hayo kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa mwisho wa Kundi B uliochezwa Uwanja wa Amahoro lakini pointi tano ilizokusanya hazikutosha kuifikisha hatua inayofuata.

Baada ya kuondolewa, benchi la ufundi la Simba limeamua kutumia muda uliobaki Kigali kama sehemu ya maandalizi zaidi kuelekea ratiba kubwa inayosubiri mbele, ikiwemo Simba Day, mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu ya NBC.

Kocha wa Simba, Steve Barker amesema licha ya kutofuzu, mashindano hayo yametoa nafasi muhimu kwa timu yake kupata dakika za ushindani na kufanyia kazi maeneo mbalimbali kabla ya msimu kuanza.

"Tumerejea kambini baada ya mapumziko, tulianza mazoezi tarehe 23 na kwa kweli tumekuwa pamoja kwa takribani wiki moja tu. Nimeridhishwa na tulipo, lakini pia nafahamu bado kuna kazi kubwa ya kufanya ndani ya muda mfupi," alisema Barker.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema baada ya mchezo dhidi ya Singida, mipango yao ni kuendelea kutumia siku zilizopo Rwanda kufanya maboresho zaidi ya kikosi na hata kutafuta mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kurejea Tanzania.

"Tutatumia siku hizi kuendelea kufanya kazi, tunatarajia kupanga mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kusafiri. Tunaridhishwa na maendeleo, lakini bado tuna mambo mengi ya kuboresha kabla ya kuanza kwa ligi," alisema.

Simba ilitumia michuano ya Kagame kama sehemu ya kukipima kikosi kipya baada ya kufanya usajili wa wachezaji kadhaa  kuelekea msimu wa 2026/27.

Barker amesema ushindi dhidi ya Singida ulikuwa muhimu kurejesha hali ya kujiamini baada ya suluhu mbili za mwanzo dhidi ya Mogadishu City na Jamus, huku akifurahishwa na namna wachezaji wake walivyotumia nafasi walizopata.

Mbali na hilo, kocha huyo amesema bado anaendelea kuunganisha wachezaji wapya na mfumo anaoutaka, akiamini kadri muda wa mazoezi utakavyoongezeka ndivyo kiwango cha timu kitakavyopanda.

Kwa sasa Simba itaendelea kuwa Kigali wakati mashindano ya Kagame  yakiendelea huku wakitarajiwa kuwa na mechi hiyo ya kirafiki kati ya Jumatatu au jumanne kabla ya kurejea Tanzania.