Simba yarejea, Sven agoma

KIKOSI cha Simba kimerejea mchana wa leo saa 8:30 na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) wakitokea jijini Mbeya ambapo jana Jumapili walicheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Mbeya City ambao na kushinda bao 1-0.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Sokoine na bao la Simba lilifungwa na straika, John Bocco aliyefikisha mabao nane msimu huu na kuwa kinara wa ufungaji mpaka sasa ligi ikiwa inaendelea.
Kikosi hicho cha Simba kilikuwa na wachezaji 21, benchi la ufundi chini ya kocha, Sven Vandenbroeck pamoja na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Ofisa mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez mara baada ya kuwasili kiliunganisha moja kwa moja kambini kwao.

Waandishi wa habari waliokuwa uwanjani hapo walipomfuata Sven ili kupata tathmini yake kwenye mechi na Mbeya City pamoja na mchezo wa ligi unaofuatia dhidi ya KMC siku ya Jumatano aligoma kuzungumza lolote na kueleza kwa ufupi kuwa hana maoni yoyote ambayo anaweza kuyasema.
"Sina maoni yoyote ya kuzungumzia au kujibu masuali yako," Sven alijibu
Simba itacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC na baada ya hapo wataanza maandalizi ya kwenda Zimbabwe ambapo Desemba 23 watacheza mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum ya nchini humo.