Simba yatinga nusu fainali Kombe la FA

Muktasari:
- Mabao matatu ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Fabrice Ngoma, Leonel Ateba na Joshua Mutale ndio yaliyohitimisha safari City inayoshiriki Ligi ya Championship ambayo ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mudathir Said katika dakika ya 22 aliyewazidi akili mabeki wa Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.
SIKU chache tu, tangu ilipoweka historia kwa kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba imekuwa klabu ya kwanza msimu huu kufuzu nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuifumua Mbeya City kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mabao matatu ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Fabrice Ngoma, Leonel Ateba na Joshua Mutale ndio yaliyohitimisha safari City inayoshiriki Ligi ya Championship ambayo ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mudathir Said katika dakika ya 22 aliyewazidi akili mabeki wa Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue.
Mfungaji huyo alifumua shuti kali lililoshinda kipa Ally Salim aliyeanzishwa langoni, huku kocha Fadlu Davids akitumia pia wachezaji wengi wanaoanzia benchini.
Baada ya bao hilo, Simba ilijibu mapigo kupitia kwa Ngoma dakika ya 24 aliyeunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Ladack Chasambi, huku Ateba akifunga bao la pili katika dakika ya 30 kabla ya Joshua Mutale kufunga la tatu katika dakika ya 43 na hadi mapumziko matokeo yakawa 3-1.
Kabla ya mechi, timu hizo mara ya mwisho zilikutana katika Ligi Kuu na Mbeya City ilichapwa mabao 3-2 Januari 18, 2023 kupitia kwa Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyefunga mawili na Msenegali Pape Sakho .
Kwa upande wa mabao ya City msimu huo ambao ndio ulikuwa wa mwisho kucheza Ligi Kuu kwani ilishuka kwenda Ligi ya Championshiop, yalifungwa na waliokuwa pia nyota wa timu hiyo, Richardson Ng’ondya na Juma Shemvuni.
Simba, iliingia uwanjani ikiwa na morali baada ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuitoa Al Masry ya Misri kwa penalti 4-1, baada ya sare ya jumla ya mabao 2-2.
Simba ilianza michuano hiyo hatua ya 64 Bora kwa kuitoa Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro kwa mabao 6-0, kisha hatua ya 32 Bora aliinyuka TMA Stars ya Arusha kwa mabao 3-0 na ilipotinga 16 Bora ikainyoa Bigman FC inayoshiriki pia Ligi ya Championship na kuilaza mabao 2-1.
Mbeya City iliingia 32-Bora kwa kuing’oa Azam FC kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1 na kuja kuitupa nje Mtibwa Sugar kwa 2-1.