Starkie aanza kibabe England
Muktasari:
- Starkie, ambaye alipitia kipindi kigumu msimu uliopita kutokana na majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa msimu mzima hivi sasa ameonekana kurejea kwenye kiwango chake na kuanza kuwavutia mashabiki wa klabu hiyo.
KIUNGO mshambuliaji wa Tanzania, Ben Starkie anayekipiga Truro City FC inayoshiriki Ligi Daraja la Sita England (National League South) ameanza na mguu mzuri kwenye kikosi cha timu hiyo hiyo baada ya msimu jana kukaa nje msimu mzima.
Starkie, ambaye alipitia kipindi kigumu msimu uliopita kutokana na majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa msimu mzima hivi sasa ameonekana kurejea kwenye kiwango chake na kuanza kuwavutia mashabiki wa klabu hiyo.
Hadi sasa, nyota huyo wa Mtanzania tayari ameitumikia Truro City jumla ya mechi 10 katika ligi msimu huu, huku akionyesha mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Alionyesha ubora zaidi alipopachika bao lake la kwanza la msimu katika mchezo wa Kombe la FA (Emirates FA Cup) dhidi ya Merthyr Town FC.
Katika pambano hilo, Starkie alisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0, matokeo yaliyowawezesha kutinga hatua inayofuata ya mashindano hayo kongwe England.
Urejeo wa Starkie si tu kwamba yanawapa matumaini mashabiki wa Truro City, bali pia yanatoa picha nzuri kwa benchi la ufundi la Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ chini ya kocha Miguel Gamondi kuelekea mechi zijazo za kufuzu AFCON, ikizingatiwa kuwa kiungo huyo amekuwa miongoni mwa vijana wenye vipaji vikubwa wanaoitangaza nchi Ulaya.