Straika wa mabao Uganda awindwa Azam FC
Muktasari:
- Taarifa kutoka Uganda, zinaeleza mabosi wa Azam FC wameanza kuangalia uwezekano wa kumpata mshambuliaji huyo aliyemaliza mfungaji bora kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kuifungia KCCA mabao 14, akionyesha kiwango kizuri cha kuvutia kikosini.
MATAJIRI wa jiji Azam FC wameanza mchakato wa kuboresha safu yao ya ushambuliaji wakiwa mbioni kuipata saini ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda, Ivan Ahimbisibwe 'The Hunter', anayecheza KCCA ya Uganda.
Taarifa kutoka Uganda, zinaeleza mabosi wa Azam FC wameanza kuangalia uwezekano wa kumpata mshambuliaji huyo aliyemaliza mfungaji bora kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kuifungia KCCA mabao 14, akionyesha kiwango kizuri cha kuvutia kikosini.
Hata hivyo, taarifa hizo zinaeleza mshambuliaji huyo ni pendekezo la Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge ingawa bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya timu hizo mbili, kwa lengo la kuipata saini yake ili kukitumikia kikosi hicho.
Gazeti hili linafahamu timu hiyo inataka kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji baada ya washambuliaji msimu huu kushindwa kufunga mabao ya kutosha na kumtegemea zaidi kiungo wao Feisal Salum kufunga.
Mshambuliaji Jephte Kitambalaa Bola amefunga mabao sita katika Ligi Kuu, wakati Jean-Jacque Ngita (mabao nne) huku Nassor Saadun muda mwingi akiwa nje kwa majeraha.
Katika Ligi Kuu ya Uganda, Ahimbisibwe alimaliza kinara wa mabao baada ya kufunga 14, akiwazidi kiungo mshambuliaji wa Vipers ambaye ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa msimu wa 2025-2026, yaani (MVP), AbdulKarim Watambala aliyemaliza na 12.
Watambala alishinda Tuzo hiyo kutokana na kiwango bora alichokionyesha na Vipers, akiwashinda Frank Ssebufu na Raymond Barasa Mangoli wanaocheza wote SC Villa, Ivan Ahimbisibwe wa KCCA na Ambrose Kigozi anayecheza kikosi cha Entebbe UPPC.
Nyota wengine aliowapiga bao Ahimbisibwe katika vita ya ufungaji bora ni Ambrose Kigozi anayechezea kikosi cha Entebbe UPPC aliyefunga pia 12, Patrick Kaddu wa Kitara FC na Usama Arafat wa Vipers SC, ambao kila mmoja wao amefunga mabao 10.
Kwa msimu wa 2025-2026, Ahimbisibwe aliiwezesha KCCA FC kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Uganda na pointi zake 62, baada ya kushinda mechi 19, sare tano na kupoteza sita, nyuma ya mabingwa Vipers SC iliyomaliza kinara na pointi 67.