Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taifa stars yapigwa, yaburuza mkia kufuzu AFCON 2027

STARS Pict

TAIFA Stars imeendelea kutokuwa na matokeo mazuri katika kampeni za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Nigeria, matokeo yanayoifanya timu hiyo kuburuza mkia katika Kundi L ikiwa na pointi moja baada ya michezo mitatu.

Nigeria ilianza kwa kasi mchezo huo uliofanyika leo Novemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio uliopo Uyo, na kupata bao la kuongoza dakika ya pili kupitia Alhassan Yusuf aliyemalizia pasi ya Ademola Lookman. 

Hata hivyo, Taifa Stars ilijibu mapigo dakika ya 32 kupitia Alphonce Msanga aliyefunga kwa pasi ya Novatus Miroshi na kuifanya Tanzania kurejea mchezoni kwa kusawazisha 1-1, matokeo yaliyodumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa Stars baada ya Nigeria kuongeza kasi ya mashambulizi na kupata mabao mawili kupitia Tolu Arokodare dakika ya 52 na 60, hivyo kuwapa wenyeji ushindi wa 3-1. 

Ushindi huo ulichangiwa zaidi na uamuzi wa Kocha wa Nigeria, Eric Chelle, kufanya mabadiliko ya haraka mwanzoni mwa kipindi cha pili yaliyoongeza nguvu katika kikosi chake. 

Moses Usor na Tolu Arokodare waliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi za Alhassan Yusuf na Nnadi Tochukwu. Mabadiliko hayo yalikuwa na matokeo chanya, hasa kwa Arokodare aliyefunga mabao mawili. Kabla ya hapo, Simon Moses aliingia dakika ya 45+3 kuchukua nafasi ya Ademola Lookman aliyeumia na kulazimika kufanyiwa mabadiliko ya lazima.

Baadaye Fisayo Dele-Bashiru aliingia dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Akor Adams, kabla ya Semi Ajayi kuingia dakika ya 90+3 kuchukua nafasi ya Ola Aina.

Kwa upande wa Tanzania, benchi la ufundi chini ya Kocha Miguel Gamondi lilifanya mabadiliko matano katika jitihada za kubadili mwelekeo wa mchezo. 

Charles M'Mombwa aliingia dakika ya 56 badala ya Ibrahim Hamad, huku Simon Msuva na Idd Seleman 'Nado' wakiingia dakika ya 66 kuchukua nafasi za Kibu Denis na Cyprian Kachwele. Pia dakika ya 67, Sheikhan Khamis aliingia badala ya Himid Mao. Abdul Suleiman naye aliingia dakika ya 85 kuchukua nafasi ya Antony Mligo. 

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuzuia Stars kuondoka Uyo mikono mitupu ikiambulia kipigo cha pili katika kampeni hiyo ya kufuzu AFCON 2027.

Kipigo hicho kimeifanya Taifa Stars kucheza dakika 270 katika michezo mitatu ya Kundi L bila kupata ushindi wowote, ikiwa imekusanya pointi moja kati ya tisa zilizokuwa kwenye hesabu. Katika michezo hiyo, Tanzania imefunga mabao mawili pekee na kuruhusu sita, ikiwa na wastani wa mabao 0.67 kwa kila mchezo huku ikiruhusu wastani wa mabao mawili. 

Safari yake ilianza kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau, ikafuata sare ya 1-1 dhidi ya Madagascar na sasa kipigo cha 3-1 kutoka kwa Nigeria.

Katika msimamo wa Kundi L, Guinea-Bissau inaongoza kwa pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi sita. Madagascar inashika nafasi ya tatu kwa pointi mbili, huku Tanzania ikiburuza mkia kwa pointi moja. 

Kwa upande wa mabao, Guinea-Bissau imefunga sita na kuruhusu moja, Nigeria imefunga matano na kuruhusu matano, Madagascar imefunga matatu na kuruhusu manne, wakati Tanzania imefunga mawili na kuruhusu sita.

Pamoja na mwenendo huo, Taifa Stars tayari imejihakikishia kushiriki AFCON 2027 zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda. 

Hata hivyo, matokeo ya michezo hii yanaendelea kutoa ujumbe kwa benchi la ufundi kuhusu maeneo yanayohitaji marekebisho, hasa safu ya ushambuliaji na ulinzi, ili timu iwe katika hali nzuri ya ushindani itakapofika kwenye fainali hizo.

Baada ya kipigo hicho cha Uyo, Stars itapata nafasi ya kujiuliza itakapoikaribisha Nigeria Novemba 17, 2026, saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Huo utakuwa mchezo wa marudiano ambao Tanzania itahitaji kuutumia kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita. 

Baada ya hapo, Stars itakuwa na michezo miwili ya mwisho ya kundi hilo, ikianza kwa kusafiri kwenda kucheza na Guinea-Bissau, Machi 24, 2027, kabla ya kumalizia kwa kuikaribisha Madagascar Machi 28, 2027.