Taoussi awapa angalizo mastaa Azam FC

Muktasari:
- Akizungumza baada ya ushindi huo, Taoussi alisema wachezaji wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu ili kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa huo.
BAO la Lusajo Mwaikenda dakika ya 63, limetosha kuipeleka Azam FC hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Muungano inayoendelea visiwani Pemba, baada ya kuifunga KMKM 1-0, huku Kocha Mkuu, Rachid Taoussi akiwapa onyo mastaa wa kikosi hicho.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Taoussi alisema wachezaji wanatakiwa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu ili kutimiza malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa huo.
“Tulicheza na timu imara kwa sababu sio mara ya kwanza kukutana nayo, muhimu kwetu ni kutimiza kile kilichotuleta hapa Zanzibar, ni mashindano magumu sana lakini ni lazima tuonyeshe ukubwa wa kikosi tulichonacho,” alisema Taoussi.
Taoussi alisema baada ya timu hiyo kufika fainali ya michuano hiyo mwaka jana na kushindwa kutwaa taji hilo, safari hii wamejipanga kuandika rekodi mpya, huku akiwataka wachezaji kujua thamani yao na mahitaji ya kikosi hicho kwa wakati huu.
Ushindi kwa Azam FC umeifanya timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ambapo itacheza Aprili 28, dhidi ya JKU iliyoitoa Singida Black Stars kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.
Mbali na Azam FC na JKU zilizofuzu, timu nyingine ni Zimamoto iliyoichapa Coastal Union bao 1-0, ambapo ilikuwa inamsubiri mshindi wa mchezo wa jana kati ya KVZ FC na Yanga, ili kucheza nusu fainali itakayopigwa Aprili 29. Michuano hii inafanyika mwaka wa pili mfululizo kufuatia kufanyika pia 2024, baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka 22, tangu mara ya mwisho ilipofanyika 2002, huku Simba ikiwa ndio bingwa mtetezi wa taji hilo ilipolichukua mwaka jana.
Simba ambayo haishiriki michuano hiyo mwaka huu kutokana na kubanwa na ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilichukua ubingwa huo baada ya kuifunga Azam FC bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho raia wa Senegal, Babacar Sarr.