Uhamiaji mechi 6 bila ushindi zamuibua kocha
Muktasari:
- Mara ya mwisho timu hiyo kupata ushindi ilikuwa Aprili 2, 2026 ilipoifunga Junguni mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba. Tangu hapo, imekuwa ikipoteza na kuambulia sare.
UHAMIAJI ni miongoni mwa timu zilizoanza msimu wa 2025-2026 kwa kasi zaidi lakini upepo umegeuka ghafla baada ya kucheza mechi sita bila ushindi, huku kocha wa kikosi hicho, Abdul Saleh akitaja sababu.
Mara ya mwisho timu hiyo kupata ushindi ilikuwa Aprili 2, 2026 ilipoifunga Junguni mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba. Tangu hapo, imekuwa ikipoteza na kuambulia sare.
Matokeo ya mechi sita ilizoshindwa kupata ushindi mfululizo yapo hivi; Chipukizi 2-1 Uhamiaji, Zimamoto 1-1 Uhamiaji, Kipanga 0-0 Uhamiaji, JKU 1-1 Uhamiaji, Mlandege 2-0 Uhamiaji na KVZ 1-0 Uhamiaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh amesema morali ya wachezaji imeshuka sana tofauti na ilivyokuwa awali.
Amesema, amefanya kila jitihada kuwarudisha wachezaji hao kwenye njia sahihi ya kutafuta matokeo mazuri lakini wakifika uwanjani wanafanya wanavyotaka wao.
“Morali ya wachezaji imeshuka ndio maana hata kiwango chao sio kizuri kama ilivyokuwa mwanzo licha ya kuwaweka sawa lakini bado hawajawa tayari,” amesema.
Pia kocha huyo amesema mpangilio wa ratiba kwa sasa sio mzuri kwani mechi zinakuwa mfululizo wakikosa muda mzuri wa mapumziko.
Amesema, katika hali kama hiyo, sio rahisi kwa wachezaji kufanya vizuri ndio maana wanapitia kipindi kigumu. Kocha huyo amesema bado hawajakata tamaa kwani wanataka kuendelea kupambana kumaliza nafasi nne za juu ambapo sasa Uhamiaji ni ya sita ikiwa na pointi 42.