Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo Yanga, Simba kazi imeanza

Muktasari:

  • Baada ya michezo hiyo mitatu, Simba na Yanga zimekusanya pointi tisa kila moja, huku Azam ikiwa na pointi saba.

RAUNDI tatu za mwanzo za Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027 zimeanza kutoa picha ya aina ya msimu unaoweza kuwa na ushindani mkubwa, hasa kwa vigogo wanne wanaotajwa kuwa na nafasi kubwa katika mbio za ubingwa ambao ni Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars.

Baada ya michezo hiyo mitatu, Simba na Yanga zimekusanya pointi tisa kila moja, huku Azam ikiwa na pointi saba. Kwa Singida Black Stars, mambo yamekuwa tofauti baada ya kujikusanyia pointi nne. Wakati huo huo, Geita Gold na Polisi Tanzania zimekuwa miongoni mwa timu zilizoshangaza wengi katika mwanzo huu baada ya kupanda daraja.

Lakini kati ya vigogo hao, Yanga ndiyo iliyoanza kwa kishindo zaidi, ikiwa na uwezo mkubwa wa kufunga na pia kulinda lango lake. Mabingwa hao wamefunga mabao 11 katika michezo mitatu na kuruhusu mawili pekee, wakiwa na tofauti ya mabao tisa.

Yanga ilianza kwa kuifunga Namungo 3-1, ikaichapa Coastal Union 4-1 kabla ya kumalizia raundi ya tatu kwa ushindi mwingine mkubwa wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Tanzania. Ni mwanzo unaoonyesha wazi kwamba nguvu kubwa ya timu hiyo kwa sasa iko kwenye namna inavyoweza kutengeneza na kutumia nafasi mbele ya lango.

Katika safu hiyo ya ushambuliaji, Peter Shalulile ameshaanza kuonyesha mchango wake akiwa na mabao mawili huku Albert Kangwanda naye akiwa amefunga mawili na kutoa asisti mbili. Hilo limeifanya Yanga kuwa timu yenye wastani mkubwa zaidi wa mabao kwa mchezo kati ya vigogo hao.

Kwa upande wa Simba, hakuna ushindi mkubwa kama ule wa Yanga katika mechi tatu za mwanzo lakini Wekundu wa Msimbazi wamevuna pointi zote tisa wakiwa ugenini huku ikibidi kupagania hilo wakiwa pungufu katika kila mchezo kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu mfululizo.

Walianza kwa kuifunga Kagera Sugar 2-0, wakaishinda Pamba Jiji 2-1 na katika raundi ya tatu wakaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Black Stars.

Kwa jumla, Simba imefunga mabao sita na kufungwa mawili, ikiwa na tofauti ya mabao manne, hivyo tofauti yake na Yanga haipo kwenye pointi, bali namna ambavyo Yanga imekuwa na makali zaidi katika kutengeneza na kutumia nafasi zake kufunga.

Kinachofanya mwanzo wa Simba uwe na uzito ni historia yake katika misimu ya hivi karibuni. Msimu wa 2023-2024, ilianza kwa pointi tisa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar 4-2, Dodoma Jiji 2-0 na Coastal Union 3-0. Msimu uliofuata 2024-2025, ilifanya hivyo tena kwa kuifunga Tabora United 3-0, Singida Fountain Gate 4-0 na Tanzania Prisons 1-0.

Kwa maana hiyo, Simba imekuwa na uwezo wa kuanza ligi vizuri katika misimu kadhaa mfululizo. Msimu huu imefanya hivyo tena, ingawa safari hii kwa mabao machache zaidi. Jambo kubwa ni kwamba bado haijadondosha pointi.

Yanga naye si mgeni katika kuanza ligi. Msimu wa 2023-2024, ilianza kwa kuichapa KMC 5-0, JKT Tanzania 5-0 na Namungo 1-0, ikikusanya pointi tisa bila kufungwa bao hata moja. Msimu wa 2024-2025 ilishinda Kagera Sugar 2-0, KenGold 1-0 na JKT Tanzania 2-0, pia ikafikisha pointi tisa.

Msimu huu imefanya hivyo tena, lakini safari hii kwa nguvu kubwa zaidi kwenye safu ya ushambuliaji kama ilivyokuwa 2023-2024. Mabao 11 katika mechi tatu yanaifanya iwe mwanzo wake wenye uzalishaji mkubwa wa mabao.

Kwa takwimu za misimu mitano iliyopita, Yanga na Simba ndizo zimeonyesha uwezo mkubwa mkubwa zaidi katika raundi tatu za mwanzo. Yanga imekusanya jumla ya pointi 41 katika vipindi hivyo vitano, sawa na Simba ambayo pia ina pointi 41.

Katika msimu wa 2022-2023, Simba ilikuwa na pointi saba baada ya raundi tatu, wakati Yanga ilikuwa na saba pia. Msimu uliofuata, zote zilifikisha pointi tisa, hali iliyojirudia 2024-2025. Msimu wa 2025-2026, zote zilikuwa na pointi saba kabla ya kurejea kwenye pointi tisa kila moja msimu huu.

Kwa upande wa Azam yenyewe imeanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania, kabla ya kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya TRA United katika raundi ya pili na kumalizia kwa kuifunga Pamba 2-1. Kwa hiyo, katika michezo yake mitatu, Azam imepata ushindi mara mbili na sare moja, ikiambulia pointi saba.

Katika msimu wa 2023-2024, Azam ilianza kwa pointi tisa, lakini misimu ya 2024-2025 na 2025-2026 ilikuwa na mwanzo mgumu zaidi, ikiwa na pointi tano, hivyo pointi saba za msimu huu zinaweza kuwa ishara nzuri.

Singida Black Stars kwa upande mwingine, imeanza msimu kwa sura mbili tofauti. Katika mchezo wa kwanza iliifunga Fountain Gate 3-0, lakini ikashindwa kuendeleza kasi hiyo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar na baadaye kufungwa 2-1 na Simba.

Ina pointi nne, mabao matano ya kufunga na matatu ya kufungwa, ikiwa na tofauti ya mabao mawili. Tatizo kubwa linaloonekana mapema si uwezo wa kufunga, bali mwendelezo wa matokeo.

Historia ya Singida katika raundi tatu za mwanzo inaonyesha timu ambayo imekuwa ikibadilika sana. Msimu wa 2022-2023 ilianza kwa pointi saba, ikashuka hadi mbili katika msimu wa 2023-2024, ikarudi kwenye kiwango cha juu cha pointi tisa mwaka 2024-2025 na kupata saba msimu uliopita. Sasa ina nne. Kumbuka timu hiyo ilikuwa ikiitwa Ihefu kabla ya kujulikana Singida Black Stars huu ukiwa ni msimu wa tatu.

Ukiangalia tofauti ya mabao msimu huu, Yanga ndiyo inayotawala. Mabao 11 ya kufunga na mawili ya kufungwa yanaipa tofauti ya tisa. Simba ina tofauti ya manne huku Azam na Singida zikiwa na tofauti ya mawili kila moja.

Kwa lugha nyingine, Yanga imekuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuamua mechi kupitia safu yake ya ushambuliaji, wakati Simba imeonyesha uwezo wa kupata ushindi hata katika michezo ambayo haijafunga mabao mengi.

Takwimu za msimu uliopita pia zinaonyesha mabadiliko. Baada ya raundi tatu za 2025-2026, Simba na Yanga zilikuwa na pointi saba kila moja, Singida Black Stars ilikuwa na saba na Azam ilikuwa na tatu. Msimu huu, Simba na Yanga zimepanda hadi tisa, Azam imefika saba huku Singida ikishuka hadi nne.

Hivyo, kati ya vigogo hao wanne, Azam ndiyo imeonyesha ongezeko la pointi kubwa zaidi ukilinganisha na mwanzo wa msimu uliopita huku Simba na Yanga zikiongeza pointi mbili kila moja. Singida, badala yake, imepoteza pointi tatu ukilinganisha na ilipoanzia msimu uliopita.

WASIKIE MAKOCHA

Akizungumzia namna walivyoanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, kocha wa Simba, Steve Barker, amesema maandalizi mafupi ya msimu yamekuwa changamoto, lakini anaamini timu yake itaendelea kuimarika kadiri muda unavyokwenda.

“Haikuwa rahisi kwa sababu hatukuwa na maandalizi ya kutosha, lakini jambo jema ni kwamba tumekuwa tukiimarisha timu kadiri muda unavyokwenda. Hivyo naamini tutakuwa bora zaidi katika michezo ijayo,” amesema Barker.

Kwa upande wa Yanga, kocha Manqoba Mngqithi alisema ameridhishwa na namna wachezaji wake walivyofanya katika michezo mitatu ya mwanzo, ingawa bado anaona kuna maeneo ambayo timu inahitaji kuyafanyia kazi ili kufikia kiwango anachokihitaji.

“Bado siwezi kusema kama tupo kwenye kiwango ninachotaka, lakini naweza kusema kwamba tupo kwenye mwelekeo sahihi. Bado tuna kazi ya kufanya ili kuwa bora zaidi kama timu,” alisema Mngqithi.

Naye kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesema maandalizi yasiyoridhisha ndiyo yaliyochangia timu yake kuanza msimu kwa kusuasua, lakini ameona viashiria vya matumaini katika michezo miwili iliyofuata.

“Hatukuwa na maandalizi mazuri ya msimu, ndiyo maana hatukufanya vizuri katika mechi yetu ya kwanza dhidi ya Polisi. Hata hivyo, kumekuwa na viashiria chanya katika mechi mbili zilizofuata, hivyo naamini tutakuwa bora zaidi katika wiki mbili hadi tatu zijazo,” amesema Ibenge.

Kocha wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, amesema timu yake bado ipo katika hatua ya kujijenga baada ya mabadiliko yaliyofanyika ndani ya kikosi huku akisisitiza kuwa wachezaji wanahitaji muda zaidi ili kuzoea mfumo na falsafa yake ya uchezaji.

“Bado tunaendelea kujenga timu na kuwaunganisha wachezaji. Kuna vitu ambavyo tunahitaji kuviboresha, lakini muhimu ni kwamba tunazidi kuelewana na kila mchezo unatupa nafasi ya kujifunza na kurekebisha makosa yetu. Ninaamini tutakuwa bora zaidi,” amesema Kimoto.