Prime
Yanga mambo ni moto! Yatoa onyo kali
HABARI njema kwa Yanga ni kurejea kwa kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua, ambaye sasa yupo fiti na tayari kuendelea na majukumu yake ya kuipambania timu hiyo, huku mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara zikiwa zimebaki mechi tano tu msimu umalizike.
Ikumbukwe Pacome aliumia goti na kushindwa kuendelea na mchezo dhidi ya Singida Black Stars, akitolewa kipindi cha pili cha mechi hiyo ambayo Yanga ilishinda mabao 3-0 lakini sasa amerejea uwanjani kulipambania chama lake ambalo linaongoza Ligi Kuu Bara likiwa na pointi 60 mbili mbele ya Simba.
Kiungo huyo alikosekana mazoezini na uongozi wa klabu hiyo ulifafanua raia huyo wa Ivory Coast alikwenda kufanyiwa vipimo zaidi kuangalia hali yake kabla ya mchezo uliopita dhidi ya Namungo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moalin amesema afya ya nyota huyo imeimarika kwa kiwango kikubwa na tayari ameanza kushiriki mazoezi ya pamoja na wenzake yaliyoanza jana baada ya kikosi kurejea kambini.
Young Africans SC attacking midfielder Pacome Zouzoua (left) controls the ball under pressure from Tanzania Prisons defender Jeremiah Juma. PHOTO | COURTESY
Moalin amesema kurejea kwa Pacome ni jambo muhimu kwa timu katika kipindi hiki ambacho ushindani wa ligi umefikia hatua ya mwisho na kila mechi imekuwa na uzito wake.
“Pacome anaendelea vizuri, afya yake imeimarika na sasa yupo sawa, yupo mazoezini. Ameanza mazoezi na wenzake tangu jana na tunaendelea kumwangalia kwa karibu, kurejea kwake ni furaha kwetu kwa kuwa ni mmoja kati ya wachezaji mahiri zaidi kikosini,” amesema Moalin.
Mbali na kurejea kwa kiungo huyo, Moalin amesema benchi la ufundi lilitumia kipindi kilichopita kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kupumzika ili kurejesha nguvu zao kabla ya kuingia kwenye mechi za mwisho za msimu.
Amesema ratiba ya ligi imekuwa ngumu na yenye ushindani mkubwa, hivyo mapumziko hayo yalikuwa muhimu kwa wachezaji kuurejesha utimamu wa mwili na kujiandaa kwa changamoto zilizobaki. “Tuliwapa wachezaji muda mzuri wa kupumzika. Lengo lilikuwa kupumzisha miili yao na kuhakikisha wanarudi wakiwa na nguvu mpya kwa ajili ya mechi zilizobaki,” amesema.
Moalin ameongeza: “Yanga imejikita katika kumalizia kwa nguvu mechi tano zilizosalia za ligi huku kila mmoja ndani ya kikosi akitambua umuhimu wa kupata matokeo mazuri katika hatua hii ya mwisho ya msimu.”
Urejeo wa Pacome unapunguza idadi ya majeruhi walioko nje ya kikosi, ambapo kwa sasa wamebaki Dickson Job ambaye aliumia goti na Clement Mzize. Wawili hao watamaliza msimu wakiwa nje ya uwanja.
REKODI ZAKE
Pacome ni miongoni mwa mastaa muhimu ndani ya kikosi cha Yanga, hasa eneo la ushambuliaji, ambapo amehudumu kwa misimu mitatu mfululizo tangu atue akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, alikocheza pamoja na Stephane Aziz KI na Yao Kouassi ambao baadaye walikutana naye Jangwani.
Rekodi zake zinaendelea kumpa nafasi ndani ya kikosi cha Yanga, akifunga mabao saba msimu wake wa kwanza, 13 msimu wa pili na hadi sasa amefunga mabao saba. Aidha, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake unaomalizika mwishoni mwa msimu wa 2026/27.