Yanga Princess yaibuka mshindi wa tatu Ngao ya Jamii 2026
Muktasari:
- Mashujaa Queens ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Maimuna Hamis 'Mynaco', aliyetumbukiza mpira kimiani kwa mpira wa faulo na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
KIPA Molly Nabitaka ameibuka shujaa wa Yanga Princess baada ya kuokoa penalti moja na kuifanya timu hiyo kutwaa mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii kwa Wanawake kwa kuifunga Mashujaa Queens kwa mikwaju 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo.
Mashujaa Queens ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Maimuna Hamis 'Mynaco', aliyetumbukiza mpira kimiani kwa mpira wa faulo na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Yanga Princess ilirudi kwa kasi kusaka bao la kusawazisha, na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 59 baada ya kiungo mshambuliaji raia wa Ethiopia, Mesay Temesgen, alipofunga bao la faulo lililomwacha kipa wa Mashujaa hoi na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi dakika 90 zinamalizika.
Shughuli pekee ilikuwa kwenye mikwaju ya penalti ambapo presha ilikuwa kubwa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wa Mashujaa Queens, waliofunga ni Sabina Mbuga, Neema Paul, Zainab Dudu na Maimuna Hamis 'Mynaco'.
Hata hivyo, mambo yaliwaendea vibaya baada ya kipa wa Yanga kuokoa penalti ya Saada Magere, huku Tabea Munga na Blandina Ambrose wakikosa mikwaju hiyo.
Yanga Princess walionyesha umakini mkubwa kwenye upigaji ambapo Mesay Temesgen, Neema Charles, Agnes Pallangyo na Diana Mnally walipachika kimiani mikwaju yao kwa umakini mkubwa na kuipa Yanga ushindi huo muhimu.