Yanga, Simba wakitupwa hapa CAF kazi ipo
Muktasari:
- Droo hiyo itafanyika Jumatano, Oktoba 28, jijini Cairo, Misri, saa 9:00 alasiri kwa saa za Misri,(sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki) ambapo timu 16 zilizofuzu zitagawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja. Yanga na Simba zimewekwa Kapu la Pili, hivyo kila moja itakutana na timu moja kutoka kila kapu kati ya Kapu la Kwanza, la Tatu na la Nne.
YANGA na Simba zinasubiri kwa hamu kujua wapinzani wao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026/27, huku droo ikitarajiwa kuamua iwapo timu hizo zitapata njia yenye nafuu au kukutana na mtihani mgumu katika harakati za kusaka ubingwa wa Afrika.
Droo hiyo itafanyika Jumatano, Oktoba 28, jijini Cairo, Misri, saa 9:00 alasiri kwa saa za Misri,(sawa na saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki) ambapo timu 16 zilizofuzu zitagawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja. Yanga na Simba zimewekwa Kapu la Pili, hivyo kila moja itakutana na timu moja kutoka kila kapu kati ya Kapu la Kwanza, la Tatu na la Nne.
Kwa kuwa timu hizo mbili zipo kapu moja, haziwezi kupangwa kundi moja, lakini kila moja ina nafasi ya kukutana na baadhi ya vigogo wenye uzoefu mkubwa wa mashindano hayo.
Katika Kapu la Kwanza, kuna Esperance ya Tunisia, Zamalek na Pyramids FC za Misri. Esperance imetwaa ubingwa wa Afrika mara nne, huku Zamalek ikiwa na mataji matano. Pyramids nayo ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25 na imejijengea heshima katika soka la bara hili.
Kukutana na timu mojawapo kati ya hizo kungehitaji Yanga na Simba kuwa makini katika safu ya ulinzi, kutumia vyema nafasi za kufunga na kuhakikisha haipotezi pointi kirahisi nyumbani. Timu hizo zina uzoefu wa kucheza mechi zenye presha kubwa na zina malengo ya kwenda mbali katika mashindano.
Kwa Yanga na Simba, kundi lenye RS Berkane linaweza kuonekana kuwa na nafuu kwa kulinganisha na makundi ambayo yatakuwa na Esperance, Zamalek au Pyramids. Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa Berkane ni mpinzani mwepesi, kwani nayo ina uzoefu wa mashindano ya Afrika na uwezo wa kupambana na timu kubwa.
Katika Kapu la Tatu, timu zitakazoweza kuwaongezea ugumu zaidi ni MC Alger ya Algeria na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Kukutana na mojawapo ya timu hizo kungehitaji Yanga au Simba kujiandaa kwa ushindani mkali, hasa kutokana na uzoefu wao katika mashindano ya kimataifa.
Kwa upande mwingine, FC Nouadhibou ya Mauritania na Horoya AC ya Guinea zinaweza kuonekana kuwa na nafuu kwa kulinganisha na wapinzani hao wawili. Hata hivyo, hazipaswi kudharauliwa, kwani kufuzu kwao hatua hii kunamaanisha zimepita katika hatua za awali na zina malengo ya kuendelea kufanya vizuri.
Kapu la Nne pia linaweza kuwa na mitego yake. Club Africain ya Tunisia, Wiliete SC ya Angola, Colombe Sportive ya Cameroon na MAS de Fes ya Morocco ni timu ambazo hazipaswi kuchukuliwa kuwa rahisi kwa sababu tu zipo katika kapu la chini.
Club Africain ilifuzu baada ya kuiondoa TP Mazembe ya DR Congo kwa jumla ya mabao 2-1, huku Wiliete ikiandika historia kwa kuiondoa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, mabingwa watetezi, kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya mabao 1-1. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa hata timu zilizopo Kapu la Nne zina uwezo wa kushtua vigogo.
Kwa kuangalia uwezekano wa droo, kundi lenye RS Berkane, FC Nouadhibou au Horoya na Colombe Sportive linaweza kuwa miongoni mwa makundi yenye nafuu kwa Yanga au Simba. Hata hivyo, kundi litakalokuwa na Esperance, Zamalek au Pyramids, likiambatana na MC Alger au Orlando Pirates pamoja na Club Africain au MAS de Fes, linaweza kuwa mtihani mkubwa zaidi.
Yanga na Simba zimefika hatua hii baada ya kufanya vizuri katika mechi za mchujo, lakini hatua ya makundi itahitaji zaidi ya matokeo ya awali. Uwezo wa kupata pointi nyumbani, kuhimili presha ya ugenini na kutumia nafasi za kufunga utakuwa muhimu katika kuwania nafasi mbili za juu zinazofuzu robo fainali.
Kwa sasa, hakuna kundi linaloweza kuitwa jepesi au la kifo kabla ya droo kufanyika. Hata hivyo, macho ya mashabiki wa Tanzania yatakuwa Cairo wakisubiri kuona kama miamba hiyo miwili itaepuka baadhi ya vigogo au itakabiliwa na safari ngumu tangu mwanzo wa hatua ya makundi.
Timu zilizofuzu ni Al Hilal Omdurman (Sudan), Club Africain (Tunisia), Colombe Sportive (Cameroon), Esperance (Tunisia), FC Nouadhibou (Mauritania), Horoya AC (Guinea), MAS de Fes (Morocco), MC Alger (Algeria), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Petro Atletico (Angola), Pyramids FC (Misri), RS Berkane (Morocco), Simba (Tanzania), Wiliete SC (Angola), Yanga (Tanzania) na Zamalek SC (Misri).
MAKUNDI YA KIFO
Kundi A
Esperance
Yanga/Simba
MC Alger
MAS de Fes
Kundi B
Zamalek
Yanga/Simba
Orlando Pirates
MAS de Fes
Kundi C
Pyramids,
Yanga/Simba
MC Alger
Club Africain
MAKUNDI NAFUU
Kundi A
RS Berkane
Yanga/Simba
FC Nouadhibou
Colombe Sportive
Kundi B
Pyramids FC
Yanga/Simba
Horoya
Wiliete SC